Friday, 28 August 2015

WAKATAENI WANASIASA WATOA RUSHWA-SAMIA


Mgombea Mwenza wa Urais kwa tiketi ya CCM, Mama Samia Suluhu, akiwasikiliza kina mama waiokuwa wakichota maji katika eneo la mtaa wa madukani, Longido mkoani Arusha.
Katibu Mkuu wa UWT, Amina Makilagi, akimtambulisha mke wa aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Arusha, aliyehamia Chadema, wakati wa mkutano wa kampeni wa Mgombea Mwenza wa Urais kwa tiketi ya CCM, Mama Samia Suluhu Hassan kwenye Uwanja wa Madukani, Longido mkoani Arusha
BAADHI ya kinamama wa jamii ya kimasai wakiwa na mabango yenye picha ya mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, wakati mgombea mwenza, Samia Suluhu Hassan alipokwenda kuhutubia mkutano wa hadhara wilayani Monduli mkoani Arusha
WANACHAMA wa CCM wakipunga mikono hewani kushangilia wakati mgombea mwenza wa urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan alipohutubia mkutano wa kampeni wilayani Monduli mkoani Arusha.
MGOMBEA mwenza wa urais kwa tiketi ya CCM, Samia Suluhu Hassan akihutubia mkutano wa kampeni wilayani Monduli

MGOMBEA mwenza wa urais kwa tiketi ya CCM, Samia Suluhu Hassan akihutubia mkutano wa kampeni wilayani Monduli
NA EPSON LUHWAGO, ARUSHA
WANANCHI wametakiwa kuwaepuka wanasiasa wanaopita na kuwarubuni kwa fedha na pombe ili kuwachagua katika nafasi za uongozi.
Tahadhari hiyo ilitolewa na Mgombea Mwenza wa Urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, kwa nyakati tofauti katika mikutano ya kampeni kwenye mikoa ya Kilimanjaro na Arusha, alipokuwa akiomba kura ili wananchi waichague CCM.
Alisema kuna wanasiasa ambao wamekuwa wakipita sehemu mbalimbali kuwarubuni watu kwa kuwapa fedha, pombe na zawadi ndogo ndogo ili wawachague.
Katika mikutano hiyo, Samia alisema wananchi hawana budi kujihadhari na watu hao kwa kuwa nia yao si njema na wamekuwa wakiwafanya wajinga.
“Ni lazima muwe na akili kichwani, mtu akija akakupa pesa au pombe wewe pokea, lakini usimpe kura yako kwani itakusababishia mateso ya miaka mitano. Ukimchagua hatakuwa nawe miaka mitano kwani umempa ubunge au udiwani kwa manufaa yake. Chagueni wagombea wa CCM ili waweze kuwaletea maendeleo,” alisema katika mkutano wa kwanza wa kampeni Hedaru mkoani Kilimanjaro.
Akiwa Tarakea wilayani Rombo, Machame, Masama Moshi Mjini na Marangu alisema wananchi wasikubali kurubuniwa kwa vitochi (pombe ya mbege) ili kuwachagua wanaotoa rushwa hiyo.
“Muache kurubuniwa na vitochi na visenti vya wapinzani hao kwani hawana nia njema na nyinyi. Watu hao wanawaona nyinyi ni watu duni ndiyo maana wanafanya hivyo.
“Jiulizeni thamani yenu ni pombe? Mna thamani kubwa sana kuliko hivyo ambavyo wanawadhania. Wakataeni kwani mkiwapa kura na kuwa madarakani wanawadharau na wanakwenda huko kutania badala ya kuwa nanyi kufanya shughuli za maendeleo,” alisisitiza.
MAKILAGI AKANDAMIZA
Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Amina Makilagi, amewataka wananchi wa Kilimanjaro na Arusha kuacha kuwachagua watu walioihama CCM na kwenda upinzani.
Alisema baadhi ya wanachama wa CCM waliokuwa wakigombea udiwani, ubunge na urais, walijitoa katika Chama na kujiunga na upinzani kwa madai kuwa hawakutendewa haki.
Kutokana na kitendo hicho, Amina alisema watu hao si wa kuaminiwa hata kidogo kuwa viongozi na ni sawa na wanaume wanaokimbia nyumba zao badala ya kutatua matatizo yanayowakabili.
”Hivi jamani mwanamume kamili anaikimbia nyumba anapopata matatizo? Huyo si mwanamume na hawezi kuaminiwa kuwa kiongozi hata siku moja. Watu wa namna hiyo ambao wamekuwa wakijiengua CCM na kukimbilia upinzani hawana sifa ya kuwa viongozi. Wakija wapuuzeni.
“Mwanamume kamili daima hukaa nyumbani na kushirikiana na wenzake ili kutatua matatizo waliyo nayo kwa pamoja,” alisema.
Amina aliwataka wananchi wa mikoa ya Arusha na Kilimanjaro waichague CCM ikiwa pamoja na kuyarejesha majimbo ambayo yalichukuliwa na upinzani katika uchaguzi uliopita.
Alisema wananchi hao wanapaswa kuwachagua madiwani, wabunge na rais kutoka CCM ili kutengeneza mnyororo mzuri wa uwajibikaji na kuleta maendeleo kwa wananchi.
“Ukichagua Rais wa CCM, Mbunge wa CCM na Diwani wa upinzani unakuwa umeharibu. Hapo ni sawa na kuwa na redio ya betri tatu halafu unaweka mbili na sehemu iliyobaki kuweka gunzi la mhindi. Redio hiyo itaimba kweli?,” alihoji.
Alisema iwapo wananchi katika majimbo hayo watawachagua madiwani kutoka CCM, ni dhahiri kwamba wataunda mabaraza ya madiwani katika halmashauri ambayo yatakuwa kiungo kikubwa baina ya chama na serikali na hatimaye kuchochea maendeleo katika maeneo yao.
Kwa mujibu wa Amina, iwapo madiwani wa halmashauri watatoka CCM ni dhahiri watakuwa watendaji katika wilaya, hivyo kuharakisha upatikanaji wa huduma.

No comments:

Post a Comment