Friday, 28 August 2015
MBOWE AZIDI KUKABWA KOO
Kibajaj, Mabula, Anjelina watikisa Mwanza
Shughuli zasimama, wafuasi waitosa UKAWA
NA PETER KATULANDA, MWANZA
MWENYEKITI wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, amezidi kushukiwa kutokana na kuwasaliti viongozi wenzake na wanachama kwa kumkaribisha Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa.
“Hatua hiyo inaendelea kuitafuna CHADEMA licha ya Lowassa kuendelea kuigiza sinema ya kudandia daladala kwa madai ya kufanya ziara kusikiliza kero za wananchi.”
“Ili kuepuka laana ya kulibwaga taifa mikononi mwa mtu mwenye kashfa, CCM imewaletea Watanzania mgombea ambaye hakutoa rushwa Dk. John Magufuli, kuleta mabadiliko ya utendaji katika serikali, hivyo wananchi wampe kura nyingi za ndiyo.”
Hayo yalisemwa na aliyekuwa mbunge ambaye kwa sasa anatetea nafasiu yake, Livingstone Lusinde, juzi wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM jijini Mwanza, zilizofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Mbugani na kuhudhuriwa na umati wa watu.
“Kweli pesa ni mbaya ilimuuza Yesu, leo imenunua chama kizima kizima. Mbowe alikuwa anasema ufisadi, leo hasemi kwa sababu fisadi mkubwa anaye, hata nyimbo za ufisadi walizokuwa wakipiga CHADEMA leo ni marufuku,” alisema Lusinde maarufu kama Kibajaji.
Alidai tamaa ya kiongozi huyo ni sawa na ya Yuda Isakariote aliyemuuza Yesu ili auawe, hivyo Lowassa naye atakufa kifo cha mende kisiasa na ndio sababu ya kumvuta Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, kuwa kama spea.
“Viongozi wa CHADEMA walizunguka Tanzania wakisema Lowassa fisadi, wakamkaba koo hadi akajiuzulu uwaziri mkuu, lakini fisadi huyo huyo kawanunua, hatuna tatizo na tajiri kama fedha zake ni halali…tunataka rais msafi na asiye na chembe ya kashfa wala mtu wa kuuguza uguza,” aliongeza kusema.
Kibajaji alisema anaamini watu wa Mwanza waliofurika uwanjani hapo walikwenda kwa mapenzi ya CCM na kuwa hiyo ni tofauti na waliojaa kwenye mkutano wa UKAWA uliofanyika viwanja vya Furahisha hivi karibuni ambao walikwenda kuangalia afya ya mgombea wa CHADEMA kama inafaa endapo watampa uongozi.
Alisema majembe waliyolichagua Nyamagana na Ilemela (wagombea ubunge Stansalus Mabula na Angelina Mabula) wanatosha kuwang’oa Ezekia Wenje na Highness Kiwia, hivyo wananchi wa majimbo hayo wawape kura nyingi za ndiyo wawatumikie, waachane na wababaishaji walioenda kutalii bungeni na kutafuta mitaji ya kufungua maduka jijini Dar se Salaam.
Akimzungumzia wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha, Kibajaji alisema mwaka 2010 alisababisha CCM ichukiwe na kunyimwa kura hadi baadhi ya vijana wakachoma ofisi ya CCM ya Kkata ya Isamilo, baada ya kukamatwa walishitakiwa na kufungwa jela.
Alisema yeye pia anastahili kwenda gerezani kwa kudharau na kutukana polisi waliokuwa wakimpa jeuri wakati akiwa kiongozi wa wizara hiyo.
MABULA NOMA
Akizungumza na wananchi hao, Mabula alisema kuchaguliwa kwake kupeperusha bendera ya CCM, kumempa jukumu ambalo tayari alishaanza kulitekeleza wakati akiwa Meya wa jiji la Mwanza.
Kada huyo machachari jukwani anayemnyima usingizi Wenje, alichaguliwa kuwa Meya baada ya aliyekuwa Meya wa jiji hilo, Josephat Manyerere, (CHADEMA) kukataliwa na madiwani wa chama chake 13 na wa CCM sita.
Alibainisha vipaumbele endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo kuwa ni elimu, afya, ardhi, miundombinu ya barabara na kukuza uchumi wa wana Nyamagana na kuboresha na kuwezesha wafanyabiashara ndogon wakiwemo machinga na mama lishe.
“Nimeipokea Ilani ya CCM nimeisoma na kuielewa, niko tayari kuisimamia na kitekeleza kwa vitendo, vipaumbele vyangu ni hivyo, nitaboresha elimu, kuongeza zahanati na vituo vya afya kila kata sababu tunataka watu wawe na afya bora,” alisema Mabula.
Aliahidi kusimamia sekta ya ardhi na kuhakikisha wananchi wanaoishi makazi yasiyopimwa wanapimiwa maeneo yao ili wapate hati, kuwezesha machinga, wajasiriamli na mama lishe kupata mikopo, kujenga barabara za mawe kwenye maeneo yenye miinuko, kuboresha huduma za maji na umeme.
ANGELINA MABULA ATOA SALAM
Naye mgombea Ubunge wa Ilemela kwa tiketi ya CCM, Angelina Mabula, alisema mwaka 2010 wana CCM walifanya makosa kukinyima kura na kuchagua wapinzani, lakini kabla ya miaka mitano walianza kujuta na kubaini walichagua wababaishaji, mwaka huu wasirudie kosa hilo, wachague wagombea wa CCM.
“Ukiingia kwenye chumba cha mtihani kutahiniwa halafu matokeo yakatoka umeshindwa na mtu ambaye hukukaa naye kutahiniwa, lazima ujute na kujiuliza imekuwaje, mwaka huu msifanye makosa kushindisha watu ambao hamjakaa nao pamoja kutahiniwa, chagueni wagombea wote wa CCM,” alisema.
WAFUASI WAIKIMBIA CHADEMA
Katika hali isiyotegemewa na vyama vya upinzani, wafuasi 48 wa Chadema, CUF na ACT Wazalendo wakiongozwa na Samson Boroyi aliyekuwa Katibu Mwenezi wa CHADEMA wilayani Ilemela, walivitosa vyama hivyo na kuhamia CCM.
Wanachama hao walijiunga na CCM wakati wa mkutano huo ambapo walisema wamejiunga na CCM kutokana na imani kubwa kwa Dk. John Magufuli.
“Nilipokuwa na Wenje tulichangisha fedha nyingi kwa mama ntilie na wauza vitumbua, lakini alichukua zote akeenda kufungua biashara Dar es salaam, mie nilipouguliwa na mama mzazi na kulazwa Bugando alininyima hata sh. 100, huyo hafai kuwa kiongozi wa watu tena, tummwage anajali maslahi yake binafsi kuliko tuliompandisha juu,” alieleza Boroyi.
Mwingine ni Vedasto Kang’anga, maarufu kama Dogo Janja aliyekuwa ACT Wazalendo Mkuyuni wilayani Nyamagana ambaye alidai viongozi wa vyama vya upinzani hawana dhamira ya kweli ya kuwaletea wananchi maendeleo, wanasaka tonge, ndiyo maana CHADEMA wamekaribisha mafisadi ili wanufaike na fedha zao.
“Ubishi kuwa CCM ni chama bora haukunisaidia kitu toka nilipokuwa nikifanya kazi na Maalim Seif Sharrif Hamad na Lwakatare, lakini sasa nimeamini vyama vingine vinasaka tonge na nyie wananchi wa Mwanza acheni ubishi, CCM ndiyo chama bora kuliko vingine, tumchagueni Dk. Magufuli, Stanslaus Mabula na Angelina Mabula na madiwani wote wa CCM,” alisema Kang’anga na kushangiliwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment