NA RHODA EZEKIEL, KIGOMA
NAIBU Waziri wa Fedha, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya
Ushindi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwigulu Nchemba, amewataka wananchi
kuhakikisha wanamchagua mgombea urais wa CCM katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25,
mwaka huu.
Amesema hawapaswi kuchagua mgombea wa upinzani, ambaye
anakabiliwa na tuhuma za kashfa, badala yake wamchague Dk. John Magufuli,
kiongozi mchapakazi, mwadilifu na aliye na uchungu na ukombozi wa Watanzania,
atakayetatua kero zao.
Mwigulu alitoa rai hiyo juzi mjini Kigoma, wakati wa sherehe
za uzinduzi wa kampeni za wabunge na
madiwani wa CCM mkoani humo, zilizofanyika kwenye viwanja vya Kahabwa.
Alisema atahakikisha anazunguka nchi nzima kumnadi
mgombea urais wa CCM kwa kuwa ndiye pekee anayefaa kwa kila sifa na utendaji
wake umeonekana kwenye wizara mbalimbali alizowahi kuziongoza.
Mwigulu alisema Watanzania wanatakiwa kuzitendea haki
nafsi zao na kufanya maamuzi ambayo hawatayajutia baadaye, ambapo Dk. John
Magufuli ndiye jibu sahihi katika hilo.
Alisema Magufuli ni mgombea ambaye Chama kilifanya uamuzi
sahihi kumteua awe mgombea urais na ambaye Watanzania wanamuhitaji kwa sasa ili
awatatulie shida zao na kuwaondoa mafisadi na watendaji wazembe kazini,
wanaorudisha nyuma maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.
Aidha, aliwaonya wananchi kupuuza vitisho na kudanganywa
na wanasiasa ambao wanatumia siasa za kisanii ili kupata kura, na ambao ni
mafisadi na hawafai katika jamii huku akiwaita kuwa hawawezi kufanya kitu
kutokana na kuwa dhoofu kisera na afya.
Katibu wa Jumuia ya Wazazi Taifa, Abdallah Bulembo,
akizungumza kwenye sherehe hizo, alisema mgombea urais wa UKAWA, Edward
Lowassa, ni msanii miaka yote.
Alihoji alikuwa wapi miaka yote kujichanganya na
wananchi, kuona kero zao na kwamba kama anataka kuona kero za wananchi, aende
gerezani akaone wananchi wanapata kero zipi au aende bandarini kubeba mizigo na
wananchi.
Bulembo alisema wananchi wanatakiwa kuwa makini na
wagombea wenye uchu wa madaraka kama Lowassa, kwa kuwa hawafai na wataipoteza
nchi, kwa kuwa wanataka kuingia ikulu kutafuta ulaji, hawawezi kufanya kazi
kama iliyofanywa na CCM kwa kipindi cha tangu uhuru.
Alisema Lowassa alipokuwa CCM, UKAWA walikuwa wakimwita
fisadi asiyefaa hata kuitwa waziri mkuu mstaafu, lakini sasa wanamwona ni mgombea
urais anayefaa kuongoza baada ya kupewa pesa ili kukiuza chama chao.
No comments:
Post a Comment