Thursday, 27 August 2015

ASKOFU; MSIWACHAGUE WAGOMBEA WANAOTOA RUSHWA




Na Happiness Mtweve, Dodoma

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu la Kanisa Katoliki Dodoma, Beatusi Kinyaiya, amewaasa Watanzania kutokubali kupokea rushwa zinazotolewa na wagombea wa nafasi mbalimbali ili kuwashawishi wawachague wakati wa uchaguzi mkuu.

Alitoa mwito huo jana wakati wa ibada ya kuvishwa mkanda maalumu wa kichungaji unaotolewa na Papa Mtakatifu, iliyofanyika mjini hapa.

Alisema amesikia kuna baadhi ya viongozi wanawashawishi wananchi wakiletewa fedha za rushwa na wagombea wa nafasi mbalimbali, wazipokee na kuzitafuna, lakini kura wasiwape.

“Rushwa inapotosha wananchi na kuwafanya kuingia kwenye umasikini wa kupindukia,” alisema.

Askofu Kinyaiya alisema rushwa ni adui wa haki na inamnyima mtu stahiki yake, hivyo wakipokea watakuwa wametenda kosa la jinai na kumkosea Mungu, ambaye anataka haki itendeke kwa wote.

“Binafsi napingana kabisa na kauli hizo kwani  zinaendelea kuchochea vitendo hivyo vya rushwa kwa wananchi ambao wanatakiwa kuwasikiliza kwenye sera zao ndipo wakatoe maamuzi wakati wa kupigakura,” alisema.

Kwa upande wake, Balozi wa Papa nchini, Askofu Francesco Padili, alisema Tanzania ni nchi ya amani, hivyo wananchi waendelee kuilinda tunu hiyo.

Alisema waumini wa dini zote wana nafasi kubwa ya kulinda na kuisimamia haki ili nchi iendelee kuwa na amani na maelewano kwa kila mtu.

No comments:

Post a Comment