MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete akiserebuke jukwaani kabla ya kuhutubia kampeni wakati wa uzinduzi wa kampeni |
BAADHI ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakiwa na mabango wakati wa uzinduzi wa kampeni |
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimezindua rasmi na kampeni kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu ambapo idadi kubwa ya wananchi walijitokeza kiasi cha kuweka historia kwenye viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam.
Rais Jakaya Kikwete na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa walikiri kuwa idadi hiyo ya watu waliojitokeza kwenye kumnadi Dk. John Magufuli ni kubwa kuliko iliyowahi kujitokeza kwenye mikutano yao.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Dk. Magufuli aliwahakikishia Watanzania kuwa watakapomchagua serikali yake ya awamu ya tano itakuwa ya viwanda.
Aidha, alisema ataunda mahakama maalum kwa ajili ya kuwashughulikia wezi na mafisadi wanaokula mali za wananchi.
Dk. Magufuli alisema serikali yake itaimarisha viwanda ikiwa ni pamoja na kujenga vingine vingi ili kuongeza ajira kwa vijana na kukuza uchumi wa nchi.
Alisema kuna viwanda vilibinafsishwa na kwamba baadhi havijaendelezwa, hivyo aliwataka waliopewa jukumu la kuviendeleza wafanye hivyo vyenginevyo wajiandae kuvirudisha.
Dk. Magufuli aliwahakikishia wananchi wajiandae na mabadiliko makubwa ya kiutendaji katika utawala wake.
Alisema utawala wake utakomesha vitendo vya rushwa na ufisadi na kwamba amejiandaa kwa hilo.
“Nitaunda mahakama maalumu kwa ajili ya kushughulikia mafisadi, wala rushwa na majizi ili yafungwe.
“Nataka wananchi wabaki salama waache kuibiwa na wachache hivyo nitaaifanya kazi hiyo ili mambo yaende,” alisema.
Alisema Watanzania wanataka elimu mzuri na kwamba katika utawala wake wanafunzi kuanzia shule ya awali mpaka kidato cha nne watasoma bure.
Dk. Magufuli alisema anafahamu tatizo kubwa la ajira lililopo kwa wananchi ambapo ameahidi kulipatia ufumbuzi ikiwa ni pamoja na kujenga viwanda.
Alisema utawala wake utahakikisha wafanyabiashara ndogo ndogo wakiwemo mama lishe, machinga na madereva wa bodaboda hawanyanyaswi.
“Wakati wa utawala wangu mgambo watafanya kazi nyingine na si kuwasumbua mama lishe,” alisema na kuibu shangwe na nderemo kutoka kwa wananchi.
Aliongeza kuwa aliomba kazi ya urais kwa ajili ya kuleta mabadiliko kwa Watanzania.
Dk. Magufuli alisema atadumisha umoja, mshikamano na ataondoa ukanda, ukabila.
Akizungumzia muungano wa Tanzania, alisema ataulinda na kuuenzi na kwamba dosari ndogo zilizopo atazimaliza.
Kuhusu suala la ulinzi na usalama, Dk. Magufuli alisema atahakikisha taifa linakuwa salama kwa kuviongezea nguvu vyombo vya ulinzi na usalama.
Alisema Jeshi la Polisi ataliboresha ikiwa ni pamoja na kuwapatia vitendea kazi na utaalamu wa kisasa.
Dk. Magufuli alisema Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), atahakikisha anaboreshea maslahi ya askari ikiwa ni pamoja na kuwajengea nyumba kwenye kambi zao.
Hata hivyo, alisema utawala wake utaheshimu mawazo ya vyama vingine na kuyafanyia kazi.
Mgombea huyo alisema wafanyabiashara wakubwa na wadogo kila mmoja atafanya kazi za biashara zake kwenye mazingira mazuri ikiwa ni pamoja na kulipa kodi.
Dk. Magufuli ambaye alitumia mkutano huo kueleza mambo mbalimbali huku msisitizo mkubwa ukiwa suala la ajira.
Alisema serikali yake, itajenga viwanda vingi ili kutoa ajira kwa wananchi na vijana.
“Tutaimarisha viwanda kwa kiasi kikubwa, tutavijenga vingi. Tutaleta wawekezaji ili waje kuwekeza.
“Kama kutakuwa na maofisa watakao wacheleweshea wawekezaji vibali basi watafute pa kuishi,” alisema.
Alisema viwanda vikijengwa vitaongeza ajira kwa asilimia 40 na kutatua tatizo la ajira lililopo.
Kuhusu sekta ya kilimo, Dk. Magufuli alisema sekta hiyo itaendelezwa kwa kuleta vitendea kazi vingi ikiwemo pembejeo.
Alisema atahakikisha kilimo kinawakomboa wananchi wengi na kuongeza ajira kupitia sekta hiyo.
Dk. Magufuli akizungumzia sekta ya mifugo, alisema Tanzania ni ya pili kwa mifugo mingi baada ya Ethiopia.
Hivyo alisema atahakikisha utawala wake unajenga viwanda vingi vya mifugo ikiwemo vya nyama na maziwa ili viweze kuliongezea taifa mapato na kunyanyua uchumi wa wananchi.
Kuhusu sekta ya madini, Mgombea huyo alisema atahakikisha yanawanufaisha Watanzania.
Dk.Magufuli alisema katika sekta ya maji atahakikisha asilimia 85 ya vijiji na asilimia 95 mijini wanapata maji safi na salama.
Kuhusu sekta ya afya, alisema ataboresha sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kujenga zahanati, vituo vya afya na hospitali kwenye maeneo yote nchini.
Alisema ataziimarisha hospitali zilizopo ili ziendelee kutoa huduma bora na kwamba ikiwezekana ziwe zinapokea wagonjwa kutoka nje ya nchi.
Dk. Magufuli alisema kuhusu sekta ya elimu, watatekeleza sera za mfumo mpya wa elimu na kuwa itatolewa bure kuanzia elimu ya awali mpaka kidato cha nne.
Mgombea huyo alisema serikali yake itajenga nyumba za walimu na kuboresha maslahi yao.
“Matatizo ya walimu nayafahamu kwani mimi pia ni mwalimu, mke wangu ni mwalimu hivyo nitaboresha maslahi yao,” alisema.
Alisema atahakikisha wanafunzi wa vyuo vikuu wanapata mikopo kwa muda muafaka ambapo wote watapata mikopo wakiwa chuoni.
Hata hivyo, alisema atajenga hosteli za wanafunzi.
Akizungumzia maslahi ya wafanyakazi, mgombea huyo alisema kila mmoja atapata haki yake kwa wakati na iliyoboreshwa.
Kuhusu gesi na mafuta, Dk. Magufuli alisema atasimamia vizuri sekta hiyo ili iweze kuwanufaisha wananchi.
Dk. Magufuli alisema sekta ya barabara itaboreshwa ambapo mikoa yote itaunganishwa na barabara za lami.
Alisema msongamano katika jiji la Dar es Salaam, unashughulikiwa na utamalizika.
Kuhusu sekta ya reli, alisema zitajengwa reli kwenye maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Dar es Salaam-Tabora-Kigoma, Mtwara-Mbamba bay.
Akizungumzia sekta ya maliasili, alisema atahakikisha anawatunza tembo na kuwaongezea maslahi watumishi wa idara hiyo.
Dk. Magufuli alisema serikali yake itakuwa rafiki wa wawekezaji ambapo itawakaribisha ili kuwekeza hapa nchini.
Akizungumzia walemavu alisema atasimamia haki zao ili waweze kuishi vizuri.
Mgombea huyo alisema atalinda uhuru wa vyombo vya habari na amewataka waandishi kusimamia haki zao na kuhusu wasanii na wana michezo alisema ataanzisha mfuko maalum ili kulinda haki zao.
No comments:
Post a Comment