Alisema uhuru wa Watanzania ulishakombolewa kupitia vyama vya ASP na TANU na kazi ya ukombozi wa maendeleo inaendelea kufanywa na CCM.
“Nchi hii imeshakombolewa na ASP na TANU, hivyo wanaodai vyama vyao ni vya ukombozi ni wapumbavu na malofa,” alisisitiza.
Mkapa, alisema Dk. Magufuli ana sifa ya kuelewa, kueleza na kutekeleza itikadi ya CCM, kupenda ushirikiano na kuwa mfano wa tabia nzuri.
Alisema hakuna timu madhubuti na imara kama ya Magufuli, hivyo utekelezaji wake wa ilani utakuwa maridhawa.
Akishangiliwa na maelfu ya wananchi, Rais Mkapa, alisema Magufuli, amekidhi sifa zilizokuwa zikihitajika kwa mgombea wa CCM.
Katika hotuba yake aliyotumia dakika 12, Rais Mkapa, alisema atatumia kipindi cha kampeni hizo za uchaguzi mkuu kuwaeleza wananchi sababu ya kuwataka waendelee kukichagua Chama.
Aliwaomba Watanzania, kuitumia haki yao ya msingi ya kupiga kura katika kuwachagua wagombea wa CCM kwa kuwa ndio wenye uwezo na sifa ya kuongoza serikali makini.
MZEE MWINYI ASEMA
WALIOJIENGUA NI CCM B
Kwa upande wake Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, alisema wanachama waliohama CCM na kujiunga na vyama vya upinzani ni CCM B.
Alisema hakuna haja ya kuwachagua wapinzani kwa sababu CCM A ipo imara na itaendelea kuwatumikia Watanzania.
“Dhamira yao imejulikana kwa kwenda kuanzisha CCM ya pili sasa kuna CCM A na B, hivyo Watanzania hampaswi kuipigia kura CCM B wakati CCM A ipo imara,” alisema.
Kauli hiyo ya Mzee Mwinyi, iliamsha hamasa na shangwe kwa wanachama na wapenzi wa CCM waliofurika Jangwani, kushuhudia uzinduzi huo wa kampeni.
Alisema wapinzani hawana sifa ya kuwafanya wachaguliwe kwa sababu wao ni CCM B wasiokuwa na viwango.
“Mtu hawezi akamwacha fundi akamfuata mwanafunzi… hao CCM B hawana viwango vya kuchaguliwa,” alisisitiza Mzee Mwinyi.
Alisema hakuna sababu ya kuelezea maendeleo makubwa yaliyofanywa na CCM kwa kuwa yanadhihirika kila mahali na katika kuunga mkono harakati hizo wananchi wanapaswa kuhakikisha wanaichagua CCM na kuiweka madarakani.
Awali kabla ya kuwahutubia wananchi kwenye viwanja hivyo vya Jangwani, Mwinyi alionyesha kushangazwa na umati wa wananchi waliofurika katika viwanja hivyo.
“Mkusanyiko wa wana CCM ni hatari,” alisema kwa mshangao rais huyo mstaafu huku akibainisha wazi haijapata kutokea kwenye viwanja hivyo.
SAMIA SULUHU AAHIDI? NEEMA KWA WANAWAKE
Kwa upande wake, Mgombea Mwenza, Samia Suluhu Hasan, alisema CCM imeandika historia kwa kumchagua mwanamke wa kwanza kuwa Makamu wa Rais na kuahidi atatumia busara, uzoefu na jitihada zote kuhakikisha anamsaidia Dk. Magufuli kutekeleza ilani ya uchaguzi.
Alisema akiwa mama atasimamia uwezeshaji wanawake kwa kuwajengea uwezo kupitia vikundi mbalimbali ikiwemo VICOBA na kusimamia huduma bora za afya hasa afya ya uzazi.
Samia alisema anafahamu changamoto zilizopo katika vifaa vya maabara na umuhimu wa mabweni kwa wasichana na jinsi gani mimba za utotoni zilivyo kero na hatari kwa taifa, hivyo atahakikisha sekta hizo zinaboreshwa.
“Pamoja na jitihada zilizopo wanawake ni wahanga wa maji safi na salama nitafanya kazi hiyo chini ya Ilani ya CCM kuwapa huduma za uhakika,” alisema.
Alisema ana uzoefu na anajua kila hatua ya utendaji kazi ofisi ya Makamu wa Rais “nitaimarisha Muungano na kuwa salama dawa ni mazungumzo kero zilizopo nitazifanyia kazi na kudhibiti zisiibuke nyingine,” alisema.
Dk. SHEIN AAHIDI KUWANYOA
WAPINZANI
Akihutubia viwanjani hapo, Rais wa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Zanzibar), Dk. Ali Mohammed Shein, alisema CCM katika uchaguzi wa mwaka huu itawanyoa wapinzani pande zote.
“Hatutaacha panki katika kuwanyoa wapinzani mwaka huu, tutawanyoa pande zote,” alisema.
Alisema uongozi wa dola haujaribiwi, hivyo hakuna sababu ya kuwachagua viongozi wapenda sifa wasio na uwezo katika kuongoza.
Aidha, aliwataka Watanzania kuelewa kuwa Wazanzibari hawataacha kumuunga mkono Dk. Magufuli kwa sababu za kihistoria za waasisi wa nchi.
“’Mti na jicho’ dola haijaribiwi, Wazanzibar tutawaunga mkono hadi tone la mwisho CCM ni Chama cha viongozi mahiri, Magufuli amefanya kazi kubwa alipoaminiwa na serikali hasa wizara alizoziongoza ikiwemo ujenzi. Mwaka 2015 ni Magufuli na Samia tu,” alisema.
Dk. Shein alisema Samia hakuletwa kujaribiwa, CCM imemleta kwa uhakika kutokana na uzoefu mkubwa na uwezo alionao katika uongozi.
“Ya Zanzibar tuachieni wenyewe tunayaweza nako hatutawaacha tutawanyoa kisawa sawa kama kawaida yetu,” alisema Dk. Shein na kushangiliwa na umati uliokuwa viwanjani hapo ambapo alisem haujawahi kutokea.
No comments:
Post a Comment