Tuesday, 25 August 2015

KIKWETE: WAPINZANI HAWATAAMBULIA CHOCHOTE




Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, akizungumza kwenye uzinduzi huo alisema wapinzani kamwe hawawezi na hawatakuja kuing’oa CCM madarakani.

Alisema sera thabiti na ilani yenye kutekelezeka inayotumiwa na CCM ni ngao imara ambayo wana CCM wanajivunia kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania kwa miaka mingi ijayo.

Alisema kuzinduliwa kwa kampeni za Chama jana ni mwanzo wa safari ya kuelekea Ikulu kwa Dk. Magufuli na Samia Suluhu Hassan, ambao ana uhakika ya kuwakabidhi kijiti cha uongozi wa nchi kama ilivyo desturi tangu awamu ya kwanza ya nchi hii.

Rais Kikwete alisema Dar es Salaam imemezwa na haijawahi kutokea, kutokana na wingi wa watu waliofika viwanjani hapo na kwamba hali hiyo imevunja rekodi kwenye uzinduzi wa kampeni za marais wote waliopita kuanzia Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na yeye katika awamu zote mbili.

“Leo tumeanza safari. Kamwe hawawezi na hawatakuja kuweza kutushinda. Sina chembe ya shaka… Oktoba nitakabidhi kijiti kwa Dk. Magufuli kama nilivyokabidhiwa na Mzee Mkapa na viongozi waliotangulia,” alisema Rais Kikwete.

Aidha, alisema vyama vya upinzani vilivyoko chini ya kundi linalojiita UKAWA havina sera wala ilani na kwamba kila mara huwasikiliza waongeapo kwa lengo la kujua ni kitu gani cha kipekee wanacho kwa ajili ya Watanzania, lakini huwa hapati.

Alisema kitendo cha kuchukua makapi kutoka chama tawala kwa ajili ya kuwasaidia kuingia ikulu ni ishara kuwa bila CCM upinzani nchini hauwezi kukua huku akisema hata waliohama hivi karibuni hawaeleweki sababu ya kuhama kwao.

“Nilimsikiliza aliyehama jana (juzi), sikumuelewa anachokizungumza kabisa. Anazunguka tu… Sijui kwa kweli, lakini kwa kuwa wameamua sisi tuko imara hapa kazi tu,” alisema.

Alisema anawashangaa waliokuwepo kabla kwenye vyama hivyo kwa kuwa wanadharauliwa bila kujitambua kwa kitendo cha waliohamia kusema wamekwenda kwa ajili ya kusaidia kuongoza kwa maana kuwa waliopo hawawezi uongozi bila msaada wa mtu husika.

“Naona wameamua kudanganywa, kama wameamua hivyo sawa, kwa sababu mtu ukukibali mwenyewe kudanganywa shauri yako,” alisema.

Alisema CCM hawakubahatisha kumchagua Dk. Magufuli kupeperusha bendera yake katika uchaguzi wa mwaka huu kwa kuwa uchapakazi wake ni silaha tosha dhidi ya wapinzani.

Alisema miaka 20 ya uongozi wa Magufuli kwenye wizara mbalimbali umekuwa ya mafanikio na kwamba hata kipindi alichokuwa naye wakati wa uongozi wake kwa awamu mbili, Dk. Magufuli amekuwa mtendaji zaidi kuliko muongeaji.

“Alipokuwa wizara ya ardhi, kazi ilionekana aliondoa usumbufu wa upatikanaji wa ardhi, pia kwenye wizara ya mifugo na uvuvi na sasa ujenzi wote ni mashahidi wakiwemo viongozi wetu wastaafu waliotangulia kuzungumza kabla yangu…,” alisema.

Pia, alisema kitendo cha kumchagua Dk. Magufuli kukiwakilisha Chama kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, kumerahisisha kampeni za chama kwa kuwa ni msafi asiye na uchafu wowote hivyo.

Alisema kumchagua mtu aliye na mashaka kwenye usafi wake ni kukipa mzigo Chama wakati wa kampeni kwa kuwa inapasa kumsafisha kwanza mtu kwa kumuondoa makando kando, kabla ya kuomba kura kwa wananchi jambo ambalo ni sawa na kazi mara mbili.

“Tungemchagua mtu mchafu, ingetupasa kumuondoa makando kando yake kwanza kabla ya kumuombea kura kwa wananchi, ni kazi kwelikweli,” alisema Kikwete.

Alisema Dk. Magufuli ni mtu sahihi, uhakika atakayeliletea taifa maendeleo na kwamba Mungu amempa shani yake kwakuwa wakati wa kutafuta wadhamini wa kumpitishi fomu yake ya ugombea kura za maoni alipata vikwazo vingi kutoka kwa viongozi wa chama wilaya.

“Huyu ni mtu wa uhakika, kwa kiswahili cha kwetu Bagamoyo… Tunasema Mwenyezi Mungu ana shani yake ya kumpa mtu anayemtaka. Sasa Magufuli kapewa shani yake kipindi hiki, ni zamu yake kwa kuwa aliniambia alipata changamoto kubwa kwenye mchakato wa kura za maoni.

Kuna viongozi wa wilaya walikataa kumsainia udhamini eti kisa walitakiwa kumsainia mtu fulani tu akija mwingine basi nafasi hiyo hakuna. Aliniambia kuwa ilimbidi kwenda kwenye ngazi ya matawi yeye mwenyewe na dereva wake. Hakuwa na kundi Magufuli,” alisema.

Aidha, kwenye hotuba yake iliyojaa maneno matamu kwa wanachama wa CCM, alisema hoja ya Rais kuwa tajiri hata CCM wala Watanzania hawataki rais masikini,  bali wanahitaji Rais mwenye fedha ambazo zina ufafanuzi mzuri wa alikozipata.

“Hatutaki Rais masikini, tunahitaji Rais mwenye fedha zake ambazo zina ufafanuzi usio na shaka juu ya zinakotoka,” alisema huku akishangiliwa kwa nderemo na vifijo na wanachama, wakereketwa na wapenzi wa CCM waliokuwa viwanjani hapo.

Alisema anaamini Tanzania akiiacha kwenye mikono ya Dk. Magufuli itakuwa salama na itajengwa na kuwa na maendeleo endelevu kwakuwa Magufuli ni kiongozi wa vitendo mwenye hamu ya kuijenga Tanzania akiwa yeye ni kiongozi wa taifa hili.

Kwa upande wa Mgombea Mwenza, Dk. Kikwete alisema Samia Suluhu Hassan, alimfahamu kwa muda mrefu na kwamba ni mchapakazi atakayekuwa msaada mkubwa kwa Dk. Magufuli kwenye kulijenga taifa hili kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Alisema ni mwanamke ambaye alisimamia kidete suala la Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar ambapo alimsaidia Makamu wa Rais, Mohammed Gharib Bilal, kuhakikisha kero za Muungano zinatatuliwa.

Aliuambia umati wa waliohudhuria ufunguzi huo kuwa zawadi ya kuwaachia makamu wa Rais mwanamke ambayo itakuwa historia iliyojiandika kwenye nchi hii tangu Uhuru, itajibu maswali ya Watanzania waliokuwa wakimuuliza mara kwa mara kuwa ‘Shemeji utatuachaje?’.

“Samia ni mchapakazi, nimemfahamu kwa muda mrefu na utendaji kazi wake mmeuona akiwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katibu ambapo alichapa kazi akamsaidia kwa kiasi kikubwa Mzee Sitta hata wakati ambao hakuwepo yeye aliendelea na wakakamilisha kazi kwa mafanikio,” alisema.

Rais alikamilisha hotuba yake fupi ambayo aliitoa huku akishangiliwa muda wote na waliohudhuria uzinduzi huo kwa kusema Tanzania hakuna chama kama CCM ambacho ni imara chenye sera thabiti na ilani makini inayolenga kumgusa kila mwananchi.

Kabla ya kushuka jukwaani alimkabidhi Dk. Magufuli na Mgombea Mwenza wake, Samia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambayo itwaongoza kwenye uongozi wao kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka huu.

No comments:

Post a Comment