Tuesday, 25 August 2015

JAJI WARIOBA AMWAGA DOZI



Waziri Mkuu mstaafu na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, alipopewa nafasi ya kuzungumza viwanjani hapo alisema CCM imejipanga na Dk. Magufuli na Samia wanatosha kwa kuwa ni viongozi wachapakazi, wazalendo na waadilifu wasio na chembe ya ufisadi ndio maana hawana makundi ya matajiri.

Warioba alisema viongozi mafisadi ndio wanaokuwa karibu na matajiri, lakini kutokana na uadilifu wa Dk. Magufuli hana kundi hilo.

“Miaka 20 iliyopita nilipewa heshima ya kuchunguza rushwa na vyanzo vyake,  ufisadi mkubwa nchini unafanywa katika miradi ya barabara na wasimamizi wake ndio wanaokuwa matajiri nchini. Magufuli angechukua hata shilingi moja angekuwa tajiri wa fedha haramu, lakini ni msafi.

 “Magufuli kundi lake ni Watanzania, mzalendo amefanya mabadiliko makubwa,  hivyo timu hii ni safi yenye sera na malengo tutajibu hoja zao kwa uhakika,” alisema.

Alisema kwa sasa Dk. Magufuli na Samia wanatoka na Ilani yenye kurasa 236 ikieleza dhamira ya CCM katika kutatua matatizo ya wananchi na mipango ya serikali kwa miaka mitano ijayo.

Aliongeza kuwa: “Leo siongei, lakini tutakutana huko mitaani tuelezane na tunawahakikishia tutajibu hoja zao zote kwa kuwa tunajiamini na wagombea wetu wanatosha,” alisema.

Aliwahakikishia wana CCM kuwa atakuwa bega kwa bega na wagombea hao na kuwaeleza wananchi ukweli.

Jaji Warioba alisema wanaouliza kwa nini Dk. Magufuli, wajue mkutano mkuu ulisikiliza maoni ya wana-CCM na wananchi ya kuwa na viongozi waadilifu.

“Magufuli ni mchapakazi kweli na hana masihara wala utani kwenye kazi anapokuwa ofisini au ‘site’ na ni mfundishaji mzuri wa wananchi katika kusimamia haki zao,” alisema.

Alisema Magufuli ni kiongozi mkali asiyetaka kazi za hovyo na matunda ya kazi zake yanaonekana.

No comments:

Post a Comment