Sunday 20 September 2015

KIGOGO CHADEMA AJIUNGA NA CCM




Na Mwandishi Wetu, Dodoma
ALIYEKUWA Katibu Msaidizi wa CHADEMA Wilaya ya Chamwino, amebwaga manyanga na kujiunga na CCM.

Katibu huyo, Kijaji Mwigame, alijiunga na CCM juzi, wakati wa uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge wa CCM katika jimbo la Chilonwa, Joel Makanyaga, katika kijiji cha Itiso.

Mbali na Mwigane, kiongozi mwingine wa Chadema aliyejitoa ni Mhazini Msaidizi wa Wilaya hiyo, Yohana Mussa Josiah.

Akizungumza baada ya kujiondoa Chadema, Mwigame alisema alikuwa akitumika kugawa kadi kwa wanachama katika jimbo hilo na kwamba baada ya kutafakari kwa kina na kujiuliza kama mtoto anaweza kupigana na baba yake mzazi, alibaini kuwa hata ukimpiga bado baba ni baba tu.

“Namuombea mgombea wetu wa CCM kura za ndiyo kwani CCM ni baba na hivyo, lazima kiongoze tena katika uchaguzi huu,’’ alisema.

Alisema ameona amepotea hivyo ameamua kurudi CCM na kukihakikishia Chama kuwa katika kadi 6,000 alizozigawa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, atahakikisha kadi 3,000 zinarudi kabla ya uchaguzi zikiwa na wanachama wa CHADEMA.
“Nimeamua kurudisha juhudi zangu nyumbani na kuhakikisha kuwa CCM inashinda kwa kishindo na nitarudi na wanachama wengine wa Chadema kabla ya uchaguzi,”alisema.
Kwa upande wake, Mhazini Msaidizi wa CHADEMA Wilaya ya Chamwino, aliyehamia CCM, alisema baada ya kufikiri kwa muda mrefu aliona kuwa amepotoka kukihama chama hicho na kwenda CHADEMA.

Alisema baada ya kurudi CCM anajiona yupo katika njia nyeupe na yenye usalama kwani uwezo wa CCM kuongoza taifa bado ni mkubwa.

“Wengi wetu tunaimba tunataka mabadiliko, lakini mabadiliko ya kweli ni kumuweka madarakani Dk. Magufuli kwani ni kiongozi mwenye sifa, anayeweza kuongea na kusumbuka na matatizo ya wananchi pande zote, siyo kumuweka mgonjwa ambaye atashindwa hata kushuka jukwaani,’’ alisema.

No comments:

Post a Comment