Thursday, 10 September 2015

KITUO CHATOA TAARIFA YA UPENDELEO, CHAMTUHUMU MAGUFULI, CHAMBEBA LOWASSA

Na Mwandishi Wetu
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu jana kilitoa tamko ambalo liliegemea upande mmoja. likimtaka mgombea urais kwa tiketi ya CCM, John Magufuli, afute kauli zake ambazo kituo hicho kimesema zinakiuka haki za binadamu.

Taarifa hiyo inayoonyesha kuandikwa Septemba 4, mwaka huu, na kutolewa jana kwa vyombo vya habari, inanukuu kauli ya Magufuli aliyoitoa kwenye viwanja vya Mashujaa, Mtwara, Septemba 2, mwaka huu, kuhusu polisi kuua jambazi mwenye silaha.

Akizungumza katika viwanja vya Mashujaa, Magufuli aliahidi kuwa akiingia madarakani, serikali yake haitamshitaki polisi atakayeua jambazi mwenye silaha, kwani vitendo vya majambazi kuvamia vituo vya polisi na kuua na kupora silaha vimekithiri.

Magufuli alihoji kwa nini majambazi hao hawavamii kambi za Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Jeshi la Kujenga Taifa au Kikosi cha Kutuliza Ghasia na kusema pengine ni kwa sababu  polisi wa kawaida wana nidhamu sana, hivyo kuwaonea na kuwaua.

Hata hivyo, taasisi hiyo ambayo ilitarajiwa isikae upande mmoja, haikuzungumzia kauli yoyote iliyotolewa na upande wa pili wa mgombea wa Chadema, Edward Lowassa, kuhusu madai kuwa CCM inajiandaa kuiba kura na hivyo kutilia shaka taarifa hiyo.

Mkurugenzi wa kituo hicho cha Sheria na Haki za Binadamu, Dk Helen Kijo-Bisimba, katika taarifa yake anarejea kauli nyingine ya Magufuli kwamba wananchi wasitoe hukumu ya jumla kama ilivyotokea Libya, ambako hivi sasa wananchi wanataabika.

Kauli zote hizi mbili kwa Kijo-Bisimba ni ukiukwaji wa haki za binadamu huku akijua pia kuwa Lowassa amekuwa akitoa kauli kama hizo, zikiwamo za kushinda asubuhi bila kueleza Oktoba 25, asubuhi atashinda kwa njia zipi wakati ndio kura zinapoanza kupigwa.

Baadhi ya watu walioiona taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi huyo, wanahoji iweje iandikwe Septemba 4, lakini isubiri na kutoka siku moja baada ya Lowassa, kukemewa na Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) kwa kufanya kampeni kanisani kinyume na kanuni na sheria za uchaguzi.

"Kwa nini tusiamini kwamba kituo hiki kimejiingiza kwenye siasa kwa kutaka kupunguza uzito wa kosa la Lowassa dhidi ya kukampeni kanisani na kutafuta mizania kwa Magufuli ili naye aonekane ana tuhuma nzito?" Alihoji Julius Sarakana.

Sarakana aliunga mkono kauli ya Magufuli kuhusu kuua jambazi mwenye silaha akisema polisi wanafunzwa kukabiliana na kupambana na mhalifu mwenye silaha.

"Hivi kama jambazi amekuelekezea bunduki na wewe unayo unafanyaje? Unasubiri akuue ili baadaye apelekwe mahakamani? Hata kama ni raia utakabiliana naye tu, hiyo ni vita tusindanganywe," alisema Sarakana.

Naye Susan Jongo wa Kariakoo alisema kama Kijo-Bisimba na timu yake waliona Magufuli hajatenda haki kwa nini wasipeleke malalamiko yao NEC siku hiyo au kesho yake.

"Mpaka wamesubiri 'mgombea wao' amebanwa na tuhuma ndipo nao wanatafuta mahali pa kufutia machozi," alisema.

Polisi kadhaa wameuawa katika vituo vya Polisi nchini baada ya majambazi kuvamia na kupora silaha kwa madhumuni ambayo mpaka sasa hayajulikani.

No comments:

Post a Comment