Thursday, 10 September 2015

NEC YAPIGA MARUFUKU KAMPENI NYUMBA ZA IBADA




NA RACHEL KYALA
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesisitiza kuwa haitasita kuvichukulia hatua vyama vya vyama siasa vitakavyoendesha kampeni katika nyumba za ibada na kuwatumia viongozi wa dini.
Aidha, imeonya kuwa kufanya hivyo ni kukiuka kanuni za maadili ya uchaguzi ambayo NEC ilikubaliana na vyama vyama vyote na kutia saini makubaliano hayo.
Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam, kwenye mkutano wa kubadilishana uzoefu wa masuala ya uchaguzi baina ya Tume za Uchaguzi za nchi za Afrika Mashariki.
“Nasisitiza kuwa tume haitasita kuvichukulia hatua kali ikiwemo kuvifutia kampeni vyama ambavyo viongozi wake wanafanya hivyo,” alisema.
Aliwataka Watanzania kuiamini tume na kuondokana na dhana kuwa inapendelea chama fulani cha siasa kwa kuwa inafanya kazi kwa uhuru kama ilivyoapa na inavipa nafasi sawa kwa vyama vyote vya siasa.
“Uchaguzi utafanyika kwa amani na haki iwapo tu kila chama kitazingatia kanuni na taratibu zilizowekwa, hivyo nawataka wananchi kupuuza kauli za uchochezi ikiwemo suala la kuibiwa kura, mshindi atapatikana kwa jumla ya wingi wa idadi ya kura halali atakazopigiwa,” alisema.
Jaji Lubuva, aliziambia tume hizo toka nchi jirani za Kenya, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Rwanda na Burundi kuwa NEC inaamini uchaguzi utakuwa wa haki na amani kwa kuwa kampeni zinaendelea vizuri.
Alivionya vyama vya siasa kuacha kutumia lugha za matusi na uchochezi katika kampeni za uchaguzi zinazoendelea.
Naibu Katibu Mkuu wa Jumuia ya Afrika Mashariki, Charles Njoroge, akifungua mkutano huo, alizitaka tume hizo kushirikiana katika kila jambo ikiwemo vifaa na usimamizi wa uchaguzi.
“Uchaguzi ni sekta muhimu kwa mustakabali wa kila taifa, Tanzania ni nchi kubwa, naamini mkutano huu utasaidia katika uchaguzi ujao ili kudumisha amani, ulinzi na usalama na kuleta matokeo chanya,” alisema.

No comments:

Post a Comment