Thursday, 8 October 2015

DK SHEIN AAHIDI KUANZISHA MAONYESHO YA BIASHARA


Na Hamis Shimye, Zanzibar

MGOMBEA wa Urais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein amesema katika miaka mitano ijayo, watajenga eneo la maonyesho ya biashara visiwani humo.

Amesema sehemu ya kujengwa kwa eneo hilo la biashara tayari imeshapatikana, lengo likiwa ni kuwavutia wafanyabiashara wa nje waje kuonyesha bidhaa zao.

Mbali ya kuwavutia wafanyabiashara hao, alisema jengo hilo pia litawasaidia wafanyabiashara wa Zanzibar kutangaza biashara zao kwa watu mbalimbali.

Dk. Shein, ambaye ni mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia CCM, aliyasema hayo jana kwenye mikutano yake ya kampeni, ambapo alisisitiza kuwa amejipanga vyema kuwaendeleza wafanyabiashara wadogo wadogo.

Alisema wafanyabiashara hao ndio wanaofanya biashara kwa wingi, hivyo serikali haiwezi kuwatupa au kuwanyanyasa, badala yake
itawajengea uwezo madhubuti.

Dk. Shein alisema serikali imeanza kuzungumza na watu mbalimbali ili kuhakikisha wanatimiza azma ya ujenzi wa eneo hilo la maonyesho.

"Tayari tuna eneo la ujenzi na tumeanza mazungumzo na watu mbalimbali ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika, ikiwemo mifuko ya hifadhi ya jamii na benki mbalimbali,''alisema.

Aidha, Dk. Shein alisema katika miaka mitano ijayo, atazidishi ushirikiano na sekta binafsi ili kuwasaidia wafanyabiashara wadogo wadogo.

Dk. Shein alisema miongoni mwa mambo wanayotarajia kuyafanya ni pamoja na kuandaa mpango mkakati wa kuwaendeleza wafanyabiashara hao, ambao ni wengi.

Wakati huo huo, Dk. Shein amesema anajivunia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma ya majisafi na salama, ambao hivi sasa maji hayo yanapatikana kwa wingi katika eneo nzima la Pemba na Unguja.

Haroun: Serikali imetekeleza mambo mengi ya msingi

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Ajira na Utumishi wa Umma, Haroun Ali Suleiman, amesema Rais Dk. Ali Mohamed Shein ameweza kutekeleza mambo mengi ya msingi aliyoyaahidi katika miaka mitano iliyopita.

Haroun alitoa kauli hiyo jana, katika mkutano wa hadhara wa kampeni za urais, kwa ajili ya kumnadi mgombea wa CCM,
Dk. Shein.

Alisema Dk. Shein ni rais mtekelezaji, ambapo ameweza kutatua tatizo la ajira kwa kiasi kikubwa, ikiwemo kuwawezesha vijana pamoja na kuandaa mipango mbalimbali ya ajira.

Waziri huyo alisema kupitia uwezeshaji wa vijana na kina mama, watu wengi wamenufaika kwa kupata mikopo iliyowawezesha kujikwamua kiuchumi.

"Tumpe kura nyingi Dk. Shein pamoja na wabunge, wawakilishi na madiwani wa CCM ili waweze kuleta maendeleo visiwani hapa, kwa kuwa chini ya uongozi wa Dk. Shein, mengi yamefanikiwa,''alisema.

Kwa upande wake, aliyekuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa tiketi ya CCM, Balozi Amina Salum Ali, alisema Zanzibar imeweza kupaa kiuchumi kwa asilimia saba katika uongozi wa Dk. Shein.

Alisema mafanikio ya kiuchumi yaliyopatikana Zanzibar kwa kiasi kikubwa yamechagizwa na uongozi imara wa Dk. Shein, ambaye amekuwa mwaminifu na mwadilifu katika kusimamia maendeleo.

Amina alisema Dk. Shein na mgombea urais wa Muungano, Dk. John Magufuli, wanapaswa kupewa kura nyingi za ndio kwa kuwa ni watu sahihi wa kuiletea maendeleo Tanzania.






No comments:

Post a Comment