Thursday, 8 October 2015

MSIBWETEKE KWA KUAMINI CCM ITASHINDA KIRAHISI-DK MWINYI


WANANCHI wa visiwa vya Pemba na Unguja wametakiwa kutobweteka kwa kuamini kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitashinda uchaguzi mkuu bila ya kujitokeza kwa wingi kupigakura katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Pia, wameelezwa kuwa chini ya serikali ya CCM, Zanzibar imepiga hatua kubwa kimaendeleo, ikiwa ni pamoja na kulinda amani na umoja uliopo miongoni mwa wananchi wa visiwa hivyo.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk. Hussein Mwinyi, wakati akimnadi mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dk. Ali Mohamed Shein.

Dk. Hussein alisema chini ya utawala wa Dk. Shein, hali ya amani na utulivu imekuwa imara kiasi cha kuwafanya wananchi wafanye kazi zao kwa umakini mkubwa kwa kuwa hakuna tishio lolote la usalama.

"Sisi watu tuliopo katika mambo ya ulinzi na usalama, tunaamini huyu ndiye kiongozi bora. Zanzibar hivi sasa ina amani tele na amani hii inapaswa kuendelezwa zaidi kwa kuwa bila ya amani hakuna maendeleo,''alisema.

Dk. Mwinyi alisema Dk. Shein ameleta amani na mshikamano na ndio maana anaona hakuna kiongozi bora kama mgombea huyo wa CCM, ambaye anapaswa kupewa kura nyingi ili aviongoze tena visiwa hivyo.

Alisema Dk. Shein na Dk. John Magufuli ndio pekee watakaoweza kuivusha zaidi Tanzania kwa kuwa ni aina ya viongozi bora na wenye uwezo mkubwa.

Kwa upande wake, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, amewataka wanaCCM ndani ya Pemba na Unguja, kuanza kupamba mashina na matawi ya CCM kwa ajili ya kusherehekea ushindi.

Amesema kadri muda unavyozidi kusonga mbele, ndivyo ushindi kwa CCM katika uchaguzi mkuu mwaka huu, unavyozidi kuongezeka kutokana na kutekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi.

Balozi Idd alisema CCM imeweza kutekeleza vizuri Ilani ya CCM kuliko chama chochote Zanzibar, na ndio maana wanaomba tena ridhaa ya kuongoza.

"CCM haina ubaguzi kama wenzetu (CUF), ambao wameanza kuwabagua wabara. Nimepewa taarifa kuwa Pemba walikataa kumzika mwananchi mmoja eti kwa kuwa si mpemba.''alisema

Balodi Idd alisema analaani kitendo hicho kwa kuwa si cha umoja na mshikamano, kwa kuwa raia wote wana haki ya kuzikwa mahali popote.

Alisema wananchi wanapaswa kuwa makini na wasikubali kuchagua chama chenye ubaguzi na kusisitiza kuwa maendeleo ya kweli yataendelea kuletwa na CCM pekee.

'Kuondoka kwa Kingunge  hakuna athari kwa CCM'

NAIBU Katibu Mkuu wa Jumuia ya Wazazi, Najma Gigi amesema kuondoka kwa mwanasiasa mkwonge nchini, Kingunge Ngombale Mwiru ndani ya CCM hakuathiri chochote.

Amesema kuondoka kwake, kumetoa picha kamili ya kiongozi huyo jinsi alivyokuwa mbinafsi na ni kiongozi aliyepoteza mwelekeo.

Najma, alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari, ambapo alisema Mzee Kingunge alishaonyesha dalili mapema ni mgombea gani aliyekuwa akimuunga mkono.

Alisema wao kama jumuia ya wazazi, hawakuona ajabu kuondoka kwake kwa kuwa wanaamini amemfuata mtu wake, ambaye ni mgombea urais wa UKAWA, Edward Lowassa.

"Hajaleta mpasuko wowote ule, ameondoka kwa utashi wake. Mbona bado wapo wazee wengi ndani ya Zanzibar au Bara. Ameondoka mzee Hassan Moyo na hakuna chochote kilichotokea,'' alisema.

Najma alisema kama kuna watu wengine wenye ubinafsi kama wa Mzee Kingunge, ni vyema wamfuate kwa kuwa CCM ni ngome kuu na haiwezi kutetereka kutokana na kuondoka kwake.

Alisema wanaoondoka hivi sasa ndani ya CCM hawawezi kupunguza kitu chochote kwa kuwa Chama bado kina nguvu na uwezo wa kufanya mambo mengi zaidi.

No comments:

Post a Comment