NA LATIFA GANZEL, MOROGORO
HATIMAYE mtoto wa marehemu Celina Kombani, Goodluck
Milinga, ameibuka na ushindi katika kura za maoni za kuwania nafasi ya ubunge
katika jimbo la Ulanga Mashariki kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Milinga, ambaye ni mtoto wa kwanza wa Celina (aliyekuwa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma), aliibuka na
ushindi huo jana, katika uchaguzi wa kura za maoni wa CCM uliofanyika katika
jimbo hilo. Nafasi hiyo ilikuwa ikiwaniwa na watu wanane.
Akitangaza matokea hayo, Msimamizi wa Uchaguzi huo,
Hamza Mfaume alisema Milinga aliibuka kidedea kwa kupata kura 731, akifutiwa na
Azizi Jawadi aliyepata kura 134.
Wengine na kura zao katika mabano ni Thabit Dokodoko
(52), Agustino Matefu (41), Wencheslous Ikumla (39), Pontian Kipao (11),
Herrieth Mwakifulefule (tisa) na Daud Kitolelo (nane).
Mfaume alisema katika uchaguzi huo, kura zilizopigwa
zilikuwa 1,029, ambapo nne ziliharibika, hivyo halali zilikuwa 1,025.
Kwa upande wake, Milinga aliwashukuru wananchi wa jimbo
hilo kwa kumpa kura nyingi na kuwaahidi atatekeleza yote ambayo aliahidi na
hata yale aliyoahidi marehemu mama yake enzi za uhai wake.
Alisema akipata ridhaa ya kuongoza jimbo hilo,
atahakikisha anaboresha huduma za afya, barabara, mawasiliano ya simu, elimu na
makazi hususan nyumba za walimu.
“Wananchi wa Ulanga wamenipa ridhaa hii kwa sababu muda
wa kampeni zote za kura za maoni wakati mama akigombea, waliniona nafanya
mimi, nawajua watu kwa sura na majina na
wao wananijua hata utendaji wangu wa kazi,” alisema
Alisema atahakikisha analitendea haki jimbo hilo kwa
kufanyakazi kwa kasi kubwa zaidi kwa kuzingatia yeye ni kijana na anamudu kasi
hiyo.
Celina alifariki dunia Septemba 24, mwaka huu, nchini
India, alikokuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa saratani ya kongosho. Alikuwa
mgombea ubunge katika Jimbo la Ulanga Mashariki.
Aliongoza jimbo la Ulanga kwa vipindi viwili mfululizo
tangu mwaka 2005 hadi 2015. Pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake
Tanzania (UWT) wilaya ya Morogoro mjini.
No comments:
Post a Comment