NA MWANDISHI WETU
CHAMA cha UPDP kimezindua kampeni zake za urais huku
kikionya wananchi kuepuka viongozi wanaoweza kulipeleka taifa kwenye maafa
makubwa.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni hizo juzi katika
viwanja vya Garden, Kilwa Kivinje, wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, mgombea urais
wa chama hicho, Fahmi Dovutwa, alisema kuna viongozi wanajaza mafuta kwenye
pikipiki na magari ili kushawishi watu waende kwenye mikutano yao.
Alisema kilichomsukuma kugombea urais ni kutaka
kuwakomboa watu dhidi ya dhuluma mbalimbali wanazowafanyia wananchi ikiwemo
uporaji wa ardhi.
Dovutwa, ambaye alianza kwa mtindo wa kuruhusu maswali,
alisema bado anainadi Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho iliyotengenezwa tangu
2005.
Akijibu maswali ya wananchi ambao walimuuliza kuhusu
kuchelewa kuzindua kampeni huku zikiwa zimebaki siku chache za kupigakura,
alisema kila mmoja ana namna ya kuwafikia wananchi na si lazima kuzunguka
majimboni.
"Wananchi hawapo katika majimbo, wapo kwenye vituo
vya kupigiakura na si wagombea wote wataweza kufika katika kila kituo cha
kupigia kura.
"Kuna namna
nyingi za kuwafikia wananchi, ikiwemo kupitia vyombo vya habari na keshokutwa
naenda kushiriki mdahalo wa wagombea urais na hapo wananchi watanielewa
zaidi,"aliongeza.
Akizungumzia sera, alisema watashughulikia maeneo muhimu
ya ardhi, elimu na maslahi ya wafanyakazi, ambao wamekuwa wakibaguliwa kwenye
malipo kinyume na katiba.
Alisema sera ya chama hicho ni ardhi ambayo ndio msingi
wa maendeleo na kwamba watapambana kutetea ardhi zilizoporwa kutoka kwa
wananchi.
Dovutwa alisema uongozi ni wito hivyo hawezi kusubiri
hadi apate mamlaka, bali anaanza kusimamia na kulitekeleza hilo kabla hajaingia
madarakani.
Alisema ametoa fomu kwa kila ofisi za UPDP nchi nzima na
kila mwenye malalamiko ya ardhi, aende akajaze na atashughulikia malalamiko
yote bila gharama zozote.
Alisema endapo atapewa ridhaa, atashughulikia kwa
ufanisi zaidi na kurudisha haraka ardhi zilizoporwa kwa wananchi.
Pia, atainua kilimo kwa sababu ndio kiwanda mama na
kuhakikisha wakulima wanainuka kiuchumi, ikiwemo kuruhusu vyama vya ushirika
huru ili kila mtu akauze mazao yake anapoona panamfaa.
Aliongeza kuwa tatizo la mkulima si kulima kwa trekta
bali ni uhakika wa soko la mazao.
Akizungumzia kuhusu elimu, alisema endapo ataingia
madarakani ataweka mfumo wa elimu ya pamoja kwa kuunganisha msingi na
sekondari.
"Nitaweka hadi darasa la 10 baada ya hapo mtoto
anaenda chuo kikuu, lakini pia nitahakikisha mitaala inabadilishwa hasa kwenye
msingi, maana wanachofanya mitaala ya sasa ni uozo, hasa kwenye masomo
yanayohusu afya ya uzazi,"aliongeza.
Alisema wanafunzi wa darasa la tatu wanafundishwa mambo
yanayochochea vitendo viovu hali inayotishia usalama wa taifa.
Aliahidi neema kwa wenyeviti wa serikali za mitaa, ambao
alidai wana haki sawa kama wafanyakazi wengine wa serikali na wamo kikatiba kwa
kuwa inatambua serikali kuu na serikali za mitaa.
Katika mkutano huo, Dovutwa alimnadi mgombea ubunge wa
Kilwa Kusini, Fatuma Machalala na mgombea udiwani wa kata ya Kivinje Singino,
Ismail Namiwa.
Kwa nyakati tofauti wagombea hao walisema wanakubalika
kwa sababu hawafanyi siasa za matusi jukwaani bali kuhamasisha maendeleo
tofauti na wagombea wa vyama vingine.
Fatuma alisema UKAWA wamekuwa wakitapatapa na kuwatuhumu
wao kwamba wanatumika na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
"Eti kwa sababu hatutukani jukwaani, basi ndio
tunatumiwa, wengine wanasema tunatumiwa kugawa kura, sisi hatuna habari,
tunaendeleza sera za kutetea wananchi, hatuna ubabe," aliongeza
No comments:
Post a Comment