Na Mwandishi Wetu, Bumbuli
MJUMBE wa Kamati ya Kampeni ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Mwigulu Nchemba, amewananga watu ambao wanatumia vibaya maneno ya Baba
wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, kuhusu mabadiliko.
Amesisitiza kwamba mabadiliko ya kweli si lazima yawe ya
vyama bali ni ya kiutendaji ambayo CCM imedhamiria kuyafanya.
Akihutubia katika mikutano mbalimbali ya kampeni ya
kumnandi mgombea ubunge wa Jimbo la Bumbuli kupitia CCM, January Makamba,
Nchemba alisema wanaonukuu maneno hayo ya Mwalimu Nyerere wananukuu sehemu ya
dhana ya mabadiliko aliyoyasema.
Wagombea wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (UKAWA), wamekuwa mara kwa mara wakinukuu maneno hayo, ambayo alisema
kama Watanzania watayakosa mabadiliko ndani ya CCM, watayatafuta nje ya chama
hicho.
Kwa mujibu wa Nchemba, wanaonukuu maneno hayo hawataji
mambo makuu manne aliyotaja Mwalimu, ambayo Watanzania wanatarajia.
Alitayaja mambo hayo kuwa ni Watanzania kuchukia rushwa
na kutaka anayewatambua Watanzania kwa Utanzania wao na wala sio kwa dini,
madhehebu au makabila yao.
Alisema CCM imemchagua mgombea urais Dk. John Magufuli
kupeperusha bendera kwa ajili ya malengo ya kuleta mabadiliko ndani ya CCM na
serikali, kutokana na rekodi yake katika miaka 20 ya utendaji kazi.
“Mabadiliko wanayoyatafuta Watanzania ni mabadiliko ya
utendaji na wala si mabadiliko ya vyama,” alisema na kuongeza kuwa wanaonadi na
kutumia maneno ya Mwalimu ni wale ambao walishindwa kusimamia utendaji ndani ya
serikali.
Akimtaja Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye,
Nchemba alisema kwa miaka 10 alikuwa
msimamizi mkuu wa utendaji wa serikali, lakini hivi sasa anakinyooshea kidole Chama na serikali yake
ambayo yeye aliwahi kuwa mtendaji wake mkuu.
Nchemba alihoji kuwa ni jambo la ajabu watu ambao
wametumia nguvu kubwa kwa miaka kadhaa kutaka kuteuliwa kuwa wagombea wa CCM na
kudai ndio chama bora, wawe ndio wanaokilaani hivi sasa.
Aliwataka Watanzania kuchagua watu watakaowatumikia kwa
malengo na sio watu ambao wameonyesha wazi wamekwenda kugombea waliko kwa
kutumia dili.
“Magufuli ndiye mgombea pekee ambaye ana rekodi ya
utendaji mzuri na ya kuchukia rushwa na kwamba ni mgombea pekee wa urais ambaye
ameonyesha nia ya dhati ya kupambana nayo,” alieleza.
Akimzungumzia mgombea ubunge wa jimbo la Bumbuli kupitia
CCM, January, aliwataka wakazi wa Bumbuli kumthamini na kumtunza kwa kuwa ni
hazina ya taifa.
Alisema January anathaminika Tanzania nzima na wananchi
hao watafanya makosa kama wakimwacha na kumchagua mtu ambaye hana hata anuani.
Kwa upande wake, January alifafanua kuhusu sh. milioni
50 zilizoahidiwa na serikali kwa ajili ya vijiji na kusema kuwa ahadi hiyo ni
ya kweli kwa sababu imefanyiwa kazi kitaalamu.
Aliwahakikishia wakazi wa Bumbuli kuwa watasimamia
wenyewe fedha hizo kupitia kamati za vijiji zitakazoundwa na vijiji vyenyewe
ili kuepuka fedha hizo kuangukia kwa watendaji ambao watazila.
No comments:
Post a Comment