Na Hamis Shimye, Zanzibar
WAKATI Uchaguzi Mkuu ukitarajiwa
kufanyika Oktoba 25, mwaka huu, mgombea urais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein
anazidi kuonekana kuwa ataibuka na ushindi wa kishindo katika uchaguzi huo.
Uchunguzi uliofanywa na UHURU,
katika visiwani vya Unguja na Pemba wiki hii, umebaini sababu kubwa inayomfanya
Dk. Shein kuibuka na ushindi ni utekelezaji mkubwa wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kwa zaidi ya asilimia 90.
Taarifa zaidi zilizopatikana katika
uchunguzi huo, zilieleza kuwa utekelezaji huo wa Ilani, unawafanya hata
wapinzani washindwe kueleza mambo watakayowafanyia Wazanzibar endapo watapewa
ridhaa kwenye uchaguzi huo, badala yake wanadai wakichaguliwa wataleta mamlaka
kamili.
UHURU lilibahatika kuweka kambi
katika maeneo mengi ya Pemba, hasa katika wilaya za Wete, Mkoani na Chakechake
na kubaini kuwa kuna uwezekano mkubwa nguvu ya CUF ikaondoka kwenye uchaguzi
huu, kutokana na utekelezaji wa mambo katika sekta zote kuanzia elimu, afya,
jamii hadi michezo kufanikiwa.
Katika uchaguzi uliopita wa mwaka
2010, CUF ilishinda majimbo yote 18, lakini wabunge na wawakilishi wa Chama hicho
wameshindwa kutekeleza mambo mengi katika majimbo yao, badala yake wamekuwa ni
watu kueneza chuki kati ya Wapemba na Waunguja.
Akizungumzia tatizo la wabunge hao
kushindwa kutekeleza lolote licha ya wabunge kwenye maeneo hayo kwa muda mwingi,
mmoja wa wananchi wa Pemba, Ahmada Saidy Ussi alisema CCM itapata ushindi na
nguvu CUF itaondoka.
Alisema tatizo kubwa la watu wa
Pemba ni uoga wa kukipigia kura CCM, kwani hivi sasa kuna propaganda zinatembea
kuwa Pemba hawahitaji barabara bali wanachotaka ni mamlaka kamili, ambayo
yatapatikana chini ya Maalim Seif Sharif Hamad.
"Awali tulikuwa tunalalamika
kuhusiana na kuwa nyuma kwa maendeleo. Dk. Shein ametekeleza mambo mengi kwa
kiasi kikubwa kuliko ilivyokuwa awali. Na hilo halifichiki na ndio maana tuna
msemo kuwa CCM wameleta maendeleo ili tuwapende,''alisema.
Kwa mujibu wa Ussi, ambaye ni mmoja
wa wanachama wa CUF, alisema hivi sasa Pemba hakuna kero yeyote kama ilivyokuwa
awali na ndio maana sera zao zimebakia kwenye mamlaka kamili na sio vinginevyo.
UHURU ilishuhudia kupoteza nguvu kwa
Maalim Seif, ambaye ni mgombea urais wa CUF toka 1995, hivyo kutoa nafasi kubwa
kwa Dk. Shein kuibuka na ushindi kwenye uchaguzi huo kutokana na muda mwingi
kuongelea suala la maendeleo kwa Zanzibar na sio vinginevyo.
Hilo limebainika hata kwenye maskani
za CUF, ikiwemo Radio One iliyoko eneo la Daraja Bovu, mjini Magharibi, Unguja,
ambao wanaamini huu ni wakati wa Maalim Seif kupumzika na kwamba anapoteza muda
ndani ya CUF.
Said Abdallah Said, alisema Seif
anapaswa kupumzika kwa kuwa hana jipya kwa siasa za hivi sasa ndani ya
Zanzibar, ambayo kwa kiasi kikubwa vijana ndio wameamka na wameonekana kuiunga
mkono CCM.
"Mimi ni CUF, lakini Maalim
tayari ameshapoteza mwelekeo, uchaguzi huu hatushindi na Dk. Shein atashinda,
amefanya mambo mengi sana hasa katika elimu, usambazaji wa nishati ya umeme na
upatikanaji wa maji safi na salama,'' alisema.
Alisema anampa nafasi kubwa Dk.
Shein kutokana na uwezo wake wa kushinda kwa kuwa moja ya kitu wanachokipigania
hivi sasa ni suala la mamlaka kamili pekee, ambayo kwa kiasi kikubwa linatolewa
ufafanuzi kila siku.
"Sisi tuna ushabiki tu, lakini
hoja ya msingi hivi sasa hatuna. Hebu niambie wewe (mwandishi wa habari) hoja
yetu nini? Kama nchi tayari tunayo tena tuna katiba yetu na yenye kueleza kila
kitu. Sasa mamlaka kamili tunayoyataka ni yapi?'' alihoji.
Licha ya kauli za watu hao, UHURU
ilibaini sababu kubwa zinazomfanya Dk. Shein kuibuka na ushindi, mbali na wingi
wa wanachama wa CCM ni kupandisha uchumi wa Zanzibar kutoka asilimia sita mwaka
2010 hadi asilimia 7.4 mwaka huu.
Pia, ameweza kuinua kiwango cha
ukusanyaji mapato ya ndani ambayo yameongezeka kutoka sh. bilioni 184.4 hadi
kufikia sh. bilioni 360.4, sawa na ukuaji wa asilimia 98.7.
UHURU pia ilibahatika kupata taarifa
kuwa chini ya uongozi wa Dk. Shein wa miaka mitano iliyopita, mgombea huyo,
ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, amepunguza mfumuko wa bei, ambao ulikuwa
unakwamisha maendeleo ya haraka visiwani humo.
Taarifa zinaeleza kuwa mfumuho huo,
umepungua kutoka asilimia 14.7 mwaka 2010 hadi asilimia 5.6 mwaka 2014, huku
pia akiimarisha pato la Zanzibar kufikia dola za Kimarekani 939, ambazo ni zaidi
ya sh. milioni moja kwa mwaka 2015.
Katika suala la kilimo, ambalo kwa
Pemba ndio kama kitega uchumi kikuu, wakulima wameonekana kunufaika na sera
mbalimbali za Dk. Shein ikiwemo kuwapatia ruzuku za pembejeo za kilimo.
Inaelezwa kuwa kuwepo kwa ruzuku
hiyo ya pembejeo, kumesaidia kuongezeka kwa mazao hasa mpunga, mbogamboga na
mifugo, ambapo zaidi ya wakulima 360,000 wamefaidika na hata kuamini mtu sahihi
ni Dk. Shein.
Katika visiwa vya Pemba, jambo
linalompa heshima zaidi Dk. Shein na hata kusifiwa na aliyekuwa Waziri Kiongozi
wa Zanzibar, awamu ya sita (2000 hadi 2010), Shamsi Vuai Nahodha ni kupandisha
zao la karafuu.
Nahodha alisema wiki hii katika
mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja Gando, uliopo Wilaya ya Wete,
Kaskazini Pemba kuwa Dk. Shein ndio mtu sahihi kutokana na kupandisha zao la
karafuu, ambalo walikuwa wanahangaika nalo na hivi sasa limekuwa juu.
Inaelezwa kuwa huko nyuma, pishi
moja ya zao la karafuu ilikuwa inauzwa kwa kiasi kisichozidi sh. 8,000, lakini
Dk. Shein amepandisha zao hilo hadi kuwa sh. 25,000 na kusababisha
wafanyabiashara kunufaika na zao hilo.
Pia, hivi sasa karafuu inaelezwa
kuwa inauzwa kwa sh. 22,000 kwa daraja la pili na makonyo ni sh. 15,000. Jambo
hilo ndio linalotoa mwangaza kuwa ushindi wa Dk. Shein ndani ya Pemba ni
mweupe.
Mbali na kuboresha zao hilo, pia
ameboresha idara ya kilimo Zanzibar na ameweza kuwagawia wananchi miche ya
karafuu bure ili kulifanya zao hilo kuimarika zaidi na kila mwananchi
ameonekana kufurahia wazo hilo la Dk. Shein katika kukipa hadhi kilimo.
Aidha, imeelezwa kuwa kupanda kwa
bei hiyo maradufu kumeondoa uuzwaji wa zao hilo kwa njia ya magendo kupitia
Mombasa nchini Kenya, ambao ulikuwa unawakosesha wananchi wa Pemba na Unguja
kunufaika na zao hilo.
Dk. Shein katika miaka yake mitano,
ameweza kuongeza usambazaji wa maji safi na salama kutoka asilimia 75 (2010)
hadi asilimia 90 kwa mwaka 2015, ambapo maeneo yote ya mjini na vijijini
yanapata maji safi na salama.
Kufanikiwa kwa Dk. Shein katika
uongozi wake wa miaka mitano ndiko kunakompa nguvu zaidi ya kuibuka na ushindi
wa zaidi ya asilimia 60, kama utafiti wa CCM uliotolewa hivi karibuni
unavyoeleza.
No comments:
Post a Comment