Thursday 8 October 2015

PINDA APOKEA WANACHAMA 205 KUTOKA CHADEMA


MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amepokea kadi tisa kati ya 205 zilizorejeshwa na wanachama wa CHADEMA katika kata ya Mamba, wilaya ya Mlele kwenye jimbo la uchaguzi la Kavuu.

Ametoa kauli hiyo jana wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wakazi wa jimbo la Kavuu, kwenye mikutano mitatu ya hadhara iliyofanyika katika kata za Mamba, Mwamapuli na Usevya.

Pinda alikuwa  mbunge kwenye jimbo hilo ambalo limegawanywa na kupata majimbo matatu ya Nsimbo, Katavi na Kavuu. Wakati huo lilikuwa likijulikana kama jimbo moja la Katavi.

Alisema katika kipindi hiki cha kampeni, uongozi wa wilaya umepokea wanachama 126 kutoka kata ya Chamalendi, 15 kutoka Kasansa, ambao wanane kati yao ni wenyeviti wa vitongoji, tisa kutoka Mamba na 62 kutoka Majimoto. Wanachama hao wametoka vyama vya CHADEMA na ACT- Wazalendo.

Alisema anastaafu akiwa na amani moyoni mwake kutokana na juhudi ambazo serikali ya awamu ya nne imezifanya kwenye mkoa wa Katavi.

Dk. Shein aipongeza Serikali ya Marekani

RAIS  wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein amepongeza hatua za Serikali ya Marekani ya kuahidi na kuendelea kuiunga mkono Tanzania, ikiwemo Zanzibar, katika uendelezaji wa awamu ya pili ya miradi inayofadhiliwa na Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC).

Aliyasema hayo jana Ikulu mjini Zanzibar, wakati alipofanya mazungumzo na Balozi wa Marekani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mark Childress.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alimueleza balozi huyo wa Marekani kuwa, hatua hizo zinaonyesha dhahiri uhusiano mwema na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Marekani, hali ambayo itaimarisha na kukuza zaidi uimarishaji wa sekta za maendeleo kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar.

Dk. Shein alisema azma ya Marekani ya kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika kuendeleza awamu ya pili ya Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC), ni heshima kubwa kwa Tanzania kwani ni miongoni mwa nchi chache zilizopata bahati za kuendelea katika awamu hiyo ya pili ya MCC.

Balozi Childress alimuhakikishia Dk. Shein kuwa awamu ya pili ya Mfuko wa MCC itatekelezwa na nchi yake na tayari fedha zake zimeshatengwa.

No comments:

Post a Comment