Thursday, 8 October 2015

DK SLAA: MAGUFULI NDIYE CHAGUO SAHIHI




NA WAANDISHI WETU
ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbrod Slaa, amesema kati ya wagombea wanane waliojitokeza kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, Dk. John Magufuli (CCM), ndiye pekee anayefaa.
Amesema Tanzania inahitaji kuwa na Rais mwenye uwezo wa kupambana na ufisadi na aliyedhihirisha kuyaweza mapambano hayo kwa vigezo halisi katika utumishi wake wa umma, ambapo kura inaangukia kwa Dk. Magufuli kwa asilimia 90.
Dk. Slaa aliyasema hayo usiku wa kuamkia jana, katika mahojiano maalumu yaliyorushwa na kituo cha televisheni cha Star cha jijini Mwanza.
Alisema kampeni si mahali pa kwenda kufanya ushabiki wala shamrashamra, bali ni mahali pa kusikiliza sera, kuwapima viongozi na kuangalia kiongozi gani ni bora kati ya waliojitokeza.
Aliongeza kuwa kiongozi yeyote ambaye anawaambia wananchi wasiende kusikiliza mikutano ya vyama vingine vya siasa, hafai kutokana na kutokujua maana ya demokrasia na kwamba, uwingi wa wananchi unaohudhuria mikutano ya CHADEMA kwa sasa sio halali.
Alisema awali wafuasi wa CHADEMA waliokuwa wakihudhuria mikutano mbalimbali ya hadhara walikuwa wakifanya hivyo kwa moyo wao na si kwa kubebwa na kusafirishwa kwenye magari kama inavyofanyika sasa.
Aidha, alisema ni vyema Watanzania wakafahamu kuwa Rais wa nchi anapochaguliwa, hakichaguliwi chama, hivyo Watanzania wanapoingia kwenye chumba cha kupigia kura Oktoba 25, mwaka huu, wanatakiwa wakumbuke wanamchagua kiongozi mkuu wa nchi bila kuangalia ni wa chama gani.
Aliongeza kusema hana hulka ya kumung’unya maneno na kwamba baada ya kusikiliza mikutano michache ya kampeni kwa wagombea wote na kwa vile mwenyewe ameendesha mapambano dhidi ya ufisadi, anamtaka rais ambaye atawaondoa Watanzania kwenye ufisadi, ambapo aliyejidhihirisha katika mapambano hayo ni Dk. Magufuli.
“Sasa hivi sina namna nyingine ya kusema nitoke nje ya mstari, kati ya hawa waliopo sina njia nyingine, lazima nichague mmoja ambaye ni Dk. Magufuli na kumbuka tunapochagua rais hatuchagui vyama. Kutokana na chaguo langu hilo, haina maana kwamba mimi ni CCM, mimi sasa hivi sina chama,” alisema Dk.Slaa.
Alisema Dk. Magufuli ana mapungufu yake kama walivyo binadamu wengine wote, lakini kwenye kigezo cha rushwa, anampa asilimia 90 na amewazidi wagombea wengine wa urais, akiwemo Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa.
Kwa mujibu wa Dk.Slaa, Dk. Magufuli amewazidi wagombea wengine kwa alama na vigezo halali, lakini anafahamu kuwa wale wenye ushabiki usio na maana hawawezi kukubaliana naye bali wataendelea na ushabiki wao.
Dk. Slaa alisema kama rais mtarajiwa anasimama jukwaani na kuzungumza dakika zisizozidi kumi, ni wazi hata zile hoja na sera za chama chake hawezi kuzifafanua vizuri kwa wananchi wanaopaswa kufafanuliwa.
“Kuna maeneo ameongea dakika mbili, kwingine ameongea dakika tatu. Tunatafuta kiongozi atakayekwenda kufanya maamuzi katika nchi na ndiyo maana nilikuwa mkali sana kwa mtu kama Askofu Gwajima kwamba ukuwadi wake ule hautusaidii,” alisema Dk.Slaa.
Kuhusu hoja alizoziibua Askofu Gwajima siku chache baada ya yeye (Dk. Slaa) kuzungumza na waandishi wa habari kwenye hoteli ya Serena juu ya uozo wa CHADEMA na mgombea wao Lowassa, Dk. Slaa alisema kiongozi huyo wa kanisa hakujibu hoja hata moja.
Alisema Gwajima ili kuokoa maslahi yake, alipotoka na kuanza kuzungumza masuala ambayo hayapo, hivyo yeye (Slaa) anamuweka pembeni na kuwaachia waumini wake wa Kanisa la Ufufuo na Uzima wamuhukumu kiongozi wa dini anayetoa siri za kondoo wake wanaoenda kuungama.
“Kwangu mimi yule si kiongozi wa dini, hafai kuwa kiongozi wa dini na ninampuuza. Ninawaachia waumini wake wamuhukumu wapendavyo,” alisema.
Alitumia fursa hiyo kuiombea roho ya Mchungaji Christopher Mtikila, ambaye alifariki mwishoni mwa wiki iliyopita kwa ajali ya gari maeneo ya Msoga mkoani Pwani na kusema alikuwa mpambanaji aliyechangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa demokrasia.
Hiyo ni mara ya pili kwa Dk. Slaa kujitokeza na kuzungumza na vyombo vya habari tangu alipotangaza rasmi kutokujihusisha moja kwa moja na siasa na kuahidi kuendelea kuwa mshauri wa masuala mbalimbali yenye maslahi na taifa.
Hatua hiyo imepongezwa na baadhi ya wananchi kuwa anatimiza ahadi yake ya kutanguliza uzalendo licha ya kupigwa vita vya maneno, matusi na wafuasi wa vyama vya upinzani, hasa CHADEMA, alichokuwa akikitumika kama mtendaji mkuu kwa miaka kadhaa.



No comments:

Post a Comment