Friday 9 October 2015

MAGUFULI KUBORESHA BIASHARA ZA MIPAKANI, SHIRIMA AFICHUA HONGO YA SHILINGI MILIONI 250





 Mgombea wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mwenyekiti wa chama cha Tanzania Labour Party (TLP) Ndugu Augustino Lyatonga Mrema mara baada  ya kukutana njia panda ya Himo.
 
Mwenyekiti wa chama cha Tanzania Labour Party (TLP) Ndugu Augustino Lyatonga Mrema akizungumza mbele ya mgombea wa urais kupitia CCM na kuwataka wananchi wa Vunjo kumpigia kura mgombea wa urais wa CCM Dk. John Pombe Magufuli kwani ni rafiki wa kweli kwa maendeleo ya Tanzania.
Wakazi wa Rombo Tarakea wakimsikiliza Mgombea wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. John Pombe Magufuli kwenye mkutano wa kampeni za CCM.
Mgombea wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. John Pombe Magufuli akimnadi mgombea ubunge jimbo la Vunjo kupitia CCM Innocent Shirima.
 Mgombea wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. John Pombe Magufuli akihutubia wakazi wa Mwanga kwenye mkutano wa kampeni za CCM ambapo aliwaahidi wananchi hao kuwa atatua tatizo la maji na barabara.
 Wananchi wa Mwanga mkoani Kilimanjaro wakifuatilia kwa makini mkutano wa kampeni za CCM
Mgombea wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. John Pombe Magufuli akimnadi mgombea ubunge wa jimbo la Mwanga Profesa Jumanne Maghembe kwenye mkutano wa kampeni za CCM zilizofanyika Mwanga
Mgombea ubunge wa jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka akilakiwa na wananchi wakati alipokuwa akiingia kwenye eneo la mkutano
Mgombea wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. John Pombe Magufuli pamoja na mgombea ubunge wa jimbo la Same Mashariki Mama Anne Kilango wakiwasalimu wakazi wa Same waliojitokeza kwenye mkutano wa kampeni za CCM Ndungu.

NA CHARLES MGANGA, ROMBO
 
MGOMBEA urais wa CCM, Dk. John Magufuli, amesema ataimarisha biashara za mipakani na nchi jirani ili wakazi wa maeneo husika na wafanyabiashara wanufaike zaidi.

Akihutubia mkutano wa kampeni katika eneo la Tarakea wilayani Rambo, jana, alisema hali hiyo itasaidia kuimarisha uchumi na kukuza utalii kwa wananchi wa maeneo ya mpakani na Watanzania wote. 

Alisema ushirikiano wa kibiashara kati ya Kenya na Tanzania, utaendelea kuimarishwa na serikali yake ya awamu ya tano.

Alisema kupitia hali hiyo, dhamira ya serikali yake ni kuzidi kufungua zaidi fursa kwa wawekezaji ambao wengi ni kutoka Kenya.

"Kenya kuna wawekezaji wengi nchini, serikali yangu itahakikisha inafungua fursa zaidi kuwekeza nchini," alisema Dk. Magufuli.

Kuhusu tatizo la maji lililopo katika baadhi ya maeneo wilayani hapa, Dk. Magufuli alisema inashangaza kuona hali hiyo ya ukame ikiendelea.

Alisema Rombo ni wilaya ya zamani, lakini haina maendeleo makubwa tofauti na Siha ambayo ni mpya.

"Inasikitisha sana, Siha ni wilaya mpya, lakini ina maendeleo makubwa kuliko Rombo, lakini haya yote yametokana na mbunge wa jimbo hilo,” alisema.

Alisema ugumu huo wa maisha hasa ukosefu wa maji unatokana na aliyekuwa mbunge wao, Joseph Selasini kususia vikao mbalimbali vya Bajeti kikiwemo kile cha Wizara ya Maji.

Ili kukabiliana na tatizo la maji, Dk Magufuli alisema akiwa rais, atahakikisha bwawa linatengenezwa kupunguza adha hiyo.

Alisema robo ya eneo la Ziwa Chala, liko Kenya huku robo tatu ikiwa Tanzania, hiyo itasaidia kuweka miundombinu kuwezesha watu kuondokana na uhaba wa maji.

"Jamani Selasini hatoshi. Ufike wakati tuseme wana-Rombo Selasini no. Huyu tutamtafutia kazi nyingine ya kufanya, hii ya kuwawakilisha bungeni ilishamshinda,"alisema Dk. Magufuli.

Aliwahimiza wananchi wa Rombo kumchagua Samora Kanje awe mbunge wa jimbo hilo kwa ajili ya maendeleo yaliyochelewa.

Akiwa Jimbo la Vunjo katika mkutano uliofanyika njiapanda Himo, Dk. Magufuli alimwagia sifa Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema kwa moyo wake wa kupigania haki za wananchi.

Alisema Mrema akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, alisimama kidete katika haki za msingi za Watanzania. 

"Jamani mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. Hakika Mrema ni mtu mzuri sana hata kama yuko upinzani, "alisema Dk Magufuli.

Alisema hata kama Mrema asipokuwa mbunge wa Vunjo, ameahidi kumtafutia sehemu kwa ajili ya kulinda heshima yake

"Sitamuacha Mrema kabisa, amefanya kazi yenye rekodi nzuri nchini, kwanza anajua kushukuru," alisema.

Aliwaomba wananchi kuachana na James Mbatia kwani aliwahi kumfanyia fitna Mrema akiwa NCCR Mageuzi, akachukua nafasi hiyo.

Alisema haikutosha anataka kuchukua na Jimbo la Vunjo, hivyo kuwataka wakazi hao kumkataa.

"Huyu Mbatia hafai kupewa ubunge, kama mkishindwa kumpa Innocent Shirima, basi mpeni Mrema," alisema.

Aidha, Shirima alitoboa siri nzito kuwa Lowasa na Mbatia walitaka kumpa kiasi cha sh. milioni 250 ili aliache jimbo hilo.

Alisema mbali ya fedha hizo, alipewa ahadi ya kuwa Mkuu wa Wilaya, lakini aligoma kwa sababu amelelewa na kukulia ndani ya CCM.

"Baada ya kuwekewa fedha mezani, niliwaomba wanipe muda, lakini nikazima simu," alisema.

Akiwa njiani kwenda Mwanga, Dk. Magufuli alipita jirani na mkutano wa kampeni wa Mrema ambapo, Mwenyekiti huyo wa TLP, aliwataka wananchi kumchagua Dk. Magufuli awe Rais ajaye.

Akiwa Mwanga, Dk. Magufuli aliahidi kushughulikia mgogoro wa ardhi kati ya wananchi na hifadhi ya Mkomazi. 

Alisema serikali yake itatenga maeneo ya kutosha kwa ajili ya wafugaji, wakulima na wavuvi kama njia mojawapo ya kuondokana na migogoro.

Alisema kwa kuwa mikoa 22 aliyofanya kampeni Watanzania wameamua atakuwa Rais, atalinda haki za wote.

Katika maeneo ya Tarakea, Himo na Mwanga, wanachama wa vyama vya Chadema, NCCR Mageuzi na CUF walijiunga CCM.

Akiwa, Jimbo la Same Mashariki, Dk. Magufuli aliwaahidi wananchi kukiboresha kiwanda cha Tangawizi kiweze kuongeza uzalishaji.

Pia, alisema serikali yake itaboresha skimu ya umwagiliaji ili wananchi waweze kufanya kilimo chenye tija.

Hata hivyo, Dk. Magufuli alimwagiza Mkuu wa Polisi Wilaya ya Same, kuwasaka na kuwakamata wanaofanya uharibifu wa miundombinu inayoharibiwa kwa makusudi na kikundi kinachodaiwa ni cha wapinzani.

Katika mkutano huo, uliofanyika Ndungwi, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Same, Kapongo Sonda, alikihama chama hicho na kujiunga CCM. 

Alisema Chadema ya sasa imekuwa ya kupokea mafisadi tofauti na zamani wakati Dk. Wilbroad Slaa akiwa Katibu Mkuu.

Dk Magufuli aliwataka wananchi wa Same kumchagua Anne Kilango Malecela kuwa mbunge.

"Hapa hii barabara ya kuja jimboni Same Mashariki, nitaweka lami kwa heshima ya John Malecela, ambaye ana historia kubwa katika nchi na wilaya hii," alisema.

No comments:

Post a Comment