Friday, 9 October 2015

VIGOGO WA NCCR-MAGEUZI KUMNG'OA MBATIA, WABAINI NJAMA ZAKE ZA KUKISAMBARATISHA CHAMA


NA WAANDISHI WETU
LICHA ya jitihada za kujaribu kuficha hali tete na msuguano mkubwa uliopo ndani ya Chama cha NCCR-MAGEUZI, mambo ni magumu kwa James Mbatia.
Mbatia, ambaye ni Mwenyekiti Taifa wa chama hicho, anatuhumiwa kutumia madaraka yake vibaya na kuvuruga Katiba kwa kuendesha vikao visivyokuwa halali.
Aidha, Makamu Mwenyekiti wa NCCR-MAGEUZI (Bara), Leticia Mosore, ambaye Mbatia alitangaza kuwa amesimamishwa na baadaye kutimuliwa, amesema maamuzi hayo yamefanyika kibabe na kwamba, bado anaendelea na wadhifa huo.
Kiongozi mwingine wa juu wa chama hicho, ambaye hakupenda kutajwa jina gazetini, amesema kuwa njama za Mbatia kukimaliza kabisa NCCR haziwezi kufanikiwa kwa kuwa wanachama wenye mapenzi ya kweli wapo.
Pia amesema siku za Mbatia za kuongoza chama hicho zinahesabika na kwamba, vitendo vya hujuma alivyofanya vinatosha.
Akizungumza Dar es Salaam, jana, Leticia alisema kikao kinachodaiwa kumvua nafasi hiyo ni batili kwa sababu kilikuwa ni cha kutathimini mwenendo wa kampeni.
Alisema kikao hicho kilichofanyika Septemba 22, mwaka huu, kimekiuka Katiba ya NCCR ibara ya 27 (3) kifungu kidogo C.
Alinukuu ibara hiyo kuwa “Makamu Mwenyekiti wa Taifa ataondolewa kwenye madaraka baada ya mapendekezo ya Halmashauri Kuu ya Taifa kwa Azimio la Mkutano Mkuu wa Taifa kwa zaidi ya nusu ya kura za wajumbe halali waliohudhuria na kupiga kura,” alisisitiza.
Alibainisha kanuni za NCCR toleo la mwaka 2002 zimeweka utaratibu wa kufuatwa katika kumwajibisha kiongozi au mwanachama ambazo zinaitiwa Kanuni za Nidhamu na Usuluhishi.
Kwa mujibu wa kanuni hizo, alisema mashtaka au malalamiko dhidi ya mwanachama au kiongozi, lazima yawakilishwe katika kikao cha utendaji cha ngazi husika kupitia kwa katibu wa ngazi hiyo lakini hatua hizo hazikufuatwa.
Alisema, Mbatia amekiuka taratibu na kanuni za chama ambako kikao alichodai kimefanya maamuzi hayo sio halali kwa mujibu wa katiba na kanuni.
Leticia, alisisitiza kuwa kikao hicho kilikuwa cha tathmini ya uchaguzi kwa sababu wagombea wa NCCR wamekuwa wanyonge ndani ya UKAWA kwa kwa kutelekezwa na Mbatia.
Alisema, Mwenyekiti huyo hajawahi kufanya kampeni kwenye majimbo yeyote yanayowaniwa na NCCR badala yake amezindua kampeni kwenye jimbo analogombea la Vunjo.
“Masikitiko yangu makubwa ni pale ninapoona Mbatia hadi sasa ameshindwa kutembelea majimbo yetu ya ngome ya chama ikiwemo mkoa wa Kigoma na hata kampeni hazikufunguliwa kwenye majimbo hayo.
“Badala yake amefungua kampeni zake Vunjo tu… ameshindwa hata kuona kuwa majimbo hayo yanahitaji msaada,” alisema.
Pia, alisema Kamati ya Nidhamu iliyoundwa kumjadili hana imani nayo kwa kuwa ina baadhi ya wajumbe ambao wamekuwa watiifu kwa Mbatia.
“Kwa tafsiri hiyo bado naendelea na nafasi yangu na Katiba inanitambua… nilichaguliwa na mkutano mkuu hivyo wadhifa wangu utakoma kwa hiyari au kufuata utaratibu kwa mujibu wa Katiba,” alisisiza.

HUJUMA DHIDI YA NCCR
Akijibu tuhuma zilizotolewa na Mbatia kuwa anakihujumu chama hicho na kutumiwa na viongozi wa CCM, alisema Watanzania wanapaswa kupima kuwa aliteuliwa ubunge wa Viti Maalum na Rais Jakaya Kikwete hivyo, kama wakutumika ni yeye aliyezawadiwa cheo hicho.
Alisema ana haki ya kukutana na viongozi na wanachama hivyo kama kuna njama za kumdhuru Mbatia, vyombo vya usalama vifanye kazi na atashirikiana navyo pindi atakapohitajika.
Alisisitiza kutoridhishwa na mwenendo wa ushirikiano wa UKAWA kwa sababu NCCR imepewa majimbo machache 12 na kati ya hayo sita yameingiliwa na CHADEMA hivyo, uhakika wa kushinda ni mdogo.
Kuingiliwa kwa majimbo hayo, alisema ni njama za CHADEMA katika kukidhoofisha NCCR huku Mbatia akiwa kimya hivyo, atapigania maslahi ya chama.

ASHUKIWA KAMA MWEWE
Kiongozi mwingine wa NCCR alisema Mbatia amekisaliti chama hicho hivyo siku zake za kubakia ndani ya chama hicho zinahesabika.
Alisema Mbatia amekuwa akipigania maslahi yake binafsi na sio ya chama hivyo, wao kama viongozi wamelibaini na watahakikisha heshima na maslahi ya chama yanalindwa.
“Kipindi kilichopo ni cha uchaguzi hivyo kina mambo mengi yanayotokea…tupo katika wakati mgumu kutokana na CHADEMA kutumia nguvu kubwa kukiua chama chetu kwa kumtumia Mbatia. “Tutapigana kilinda chama hiki na hapo ndio tutajua kati ya Mbatia na Leticia nani ana uchungu na chama na nani yupo kwa maslahi binafsi,” alisema.
Aliongeza kuwa, Mbatia amesahau Katiba na kanuni za chama zikiwemo kutambua nguvu ya kikatiba iliyokuwanayo Halmashauri kuu ya chama hasa kwenye kipindi hichi.
“Tunafahamu anaogopa kuitisha mkutano wa halmashauri kuu, nikiwa kiongozi wa chama taifa, najua kikao kilichotumika kumsimamisha Leticia si halali na sikushirikishwa zaidi ya kusoma kwenye vyombo vya habari… kikao halali ni halmashauri kuu,” alisistiza.
Septemba 22 mwaka huu, Mbatia alitangaza kumvua madaraka Makamu Mwenyekiti huyo kwa madai ya kuhusika na njama za kumdhuru na kutoa lugha za kashfa dhidi yake.

No comments:

Post a Comment