Na Rashid Zahor, Kibaha
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli ameendelea kujisafishia njia ya kushinda uchaguzi mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya kupata idadi kubwa ya wananchi katika mikutano mitatu aliyoifanya mkoani Pwani.
Mbali na mikutano hiyo mitatu, aliyoifanya jana katika majimbo ya Kibaha Vijijini, Chalinze na Kibaha Mjini, mgombea huyo pia alifanya mikutano miwili katika majimbo ya Kibamba na Kawe mkoani Dar es Salaam.
Kama ilivyo kawaida yake, Dk. Magufuli pia alihutubia mikutano isiyo rasmi saba katika maeneo ya Kiluvya, Stendi ya Mbezi, Njia panda ya Mlandizi, Vigwaza, Goba, Samaki na Tegeta Kibaoni
Katika mikutano hiyo, wananchi wa majimbo hayo matatu ya mkoa wa Pwani walimuhakikishia Dk. Magufuli kumpigia kura nyingi ili awe rais wa tano wa Tanzania kama walivyofanya wenzao wa Dar es Salaam.
Mkutano uliofanyika Maili Moja, Kibaha na shule ya msingi ya Bunju A ndio iliyovunja rekodi ya mahudhurio, kutokana na wananchi kujitokeza kwa wingi huku baadhi yao wakiwa wamepanda juu ya miti na magari yaliyokuwepo kwenye eneo hilo.
Akihutubia katika mikutano hiyo, mgombea huyo alisema katika wagombea wote wanane waliojitokeza kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hakuna anayeweza kuwaletea maendeleo wananchi zaidi yake.
Aidha, amesema Jumapili ijayo ni siku muhimu katika historia ya Tanzania kwa vile ni siku ya mabadiliko, hivyo amewaasa Watanzania wasithubutu kumchagua mgombea urais mwenye sifa ya wizi na ufisadi.
Amesema tangu alipoanza kampeni Agosti, mwaka huu, katika mji wa Katavi, ametembea umbali wa zaidi ya kilometa 45,000 na hakuwahi kupata pancha hata siku moja, ishara inayodhihirisha wazi kuwa, Mungu amemteua kuwa rais wa Tanzania.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika katika viwanja vya Miembe saba, Chalinze, Dk. Magufuli alisema serikali imepanga kuufanya mji huo uwe wa kibiashara, hivyo wananchi wajiandae kimaendeleo.
Alisema serikali yake imepanga kujenga barabara za juu sita (flyovers), kuanzia Chalinze hadi Dar es Salaam na kuufanya mji huo uwe kituo cha kibiashara kutokana na mizigo mingi itakayokuwa ikisafirishwa kutoka bandari ya Bagamoyo kupita hapo.
Kutokana na kuwepo kwa mikakati hiyo, Dk. Magufuli aliwataka wananchi wa Chalinze wasikubali kuuza ardhi yao kwa walanguzi, ambao baadaye wataiuza kwa bei kubwa na kuwaacha nyuma kimaendeleo.
"Msikubali kuuza ardhi yenu kwa walanguzi. Ardhi ni mali. Maendeleo yanakuja, yananukia,"alisema Dk. Magufuli.
Alisema wananchi wa Chalinze wametoka mbali na kufika mbali na kusisitiza kuwa, maisha bora kwao yanakuja kutokana na mpango wa serikali wa kujenga viwanda vingi vitakavyotoa ajira kwa wananchi.
Dk. Magufuli aliutumia mkutano huo kukanusha madai yaliyotolewa na mgombea mmoja wa urais juzi kwamba, fedha za kuijenga upya bandari ya Tanga zimepelekwa katika ujenzi wa bandari mpya ya Bagamoyo.
Alisema ujenzi wa bandari ya Tanga utafanyika kama ulivyopangwa kwa vile fedha za ujenzi zipo kama ilivyo kwa ujenzi wa bandari mpya katika mikoa ya Tanga, Mwanza na Lindi.
Aliwataka wanasiasa kuepuka kuwachonganisha wananchi wa Tanga na Bagamoyo na kusisitiza kuwa, ujenzi wa bandari ya Bagamoyo hautokani na Rais Jakaya Kikwete kutoka katika mji huo.
Alisema ujenzi wa bandari ya Bagamoyo unatokana na mradi wa EPP na kujitokeza kwa wawekezaji wengi kutoka Arabuni kwa ajili ya kuundeleza mji huo.
Akihutubia mkutano uliofanyika Maili Moja, Kibaha, Dk. Magufuli alisema kujitokeza kwa umati mkubwa wa watu ili kumuona na kumsikiliza, kumemfanya aone zimebaki siku chache kabla ya kuapishwa kuwa rais.
Alisema katika wagombea wote wanane wanaogombea kuchaguliwa kuwa rais wa Tanzania, hakuna anayeweza kuwaletea maendeleo Watanzania kama yeye.
Hata hivyo, aliwataka wananchi wajitokeze kwa wingi siku ya kupigakura, Jumapili, ili wampigie kura kwa wingi zitakazomwezesha kuingia Ikulu.
Aliwahakikishia wananchi hao kuwa azma ya serikali ni kuuendeleza mji wa Kibaha kama ilivyo kwa Dar es Salaam, ili kusaidia kupunguza msongamano wa magari.
Alisema Kibaha ni miongoni mwa maeneo yatakayopitiwa na barabara za juu zitakazojengwa kuanzia Chalinze hadi Dar es Salaam na baadaye kufika hadi katika mji wa Morogoro. Alisema ujenzi wa barabara hizo unatarajiwa kugharimu sh. trilioni 2.3.
" Lengo la serikali ni kuleta mabadiliko makubwa katika suala la ujenzi. Tayari nchi imeshaunganishwa kwa barabara za lami na hatua inayofuata ni ujenzi wa barabara za juu. Kibaha itakuwa mpya na ya maendeleo,"alisema.
Akihutubia mkutano uliofanyika Mlandizi, mgombea huyo alisema serikali yake itaanzisha mpango wa kujenga nyumba za walimu na kuboresha mishahara yao ili kuinua maisha yao na pia kuwafanya waipende zaidi kazi yao.
Aidha, aliwaahidi wananchi hao kuwa serikali yake itamaliza kabisa migogoro kati ya wakulima na wafugaji kwa vile hapendi kuziona jamii hizo zikiendelea kupigana na kuuana mara kwa mara.
Mgombea huyo alisema lengo la serikali yake ni kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya wakulima na wafugaji kwa vile jamii zote mbili zinahitajiana.
Akihutubia mkutano uliofanyika Bunju, Dk. Magufuli ambaye amekuwa kivutio kwa wananchi kutokana na uwezo wake wa kuzungumza lugha za makabila zaidi ya 10, alisema amezidi kufarijika kutokana na mkutano huo kuhudhuriwa na wananchi wengi.
Aliwapongeza wakazi wa Kawe kwa mahudhurio hayo, ambaye alisema yamedhihirisha wazi kwamba Watanzania wamepania kufanya mabadiliko ya kweli.
Dk. Magufuli pia alimpongeza Mzee Warioba kwa ujasiri wake wa kuacha kumpigia kampeni mwanawe, Kippi Warioba, anayewania ubunge jimbo la Kawe, badala yake akampigia kampeni yeye.
Alimwelezea Mzee Warioba kuwa ni mzazi wa aina yake, anayetaka mwanawe asimame mwenyewe.
Awali, wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Muhammed Seif Khatib, Sophia Simba, Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, walipewa nafasi ya kuwasalimia wananchi na kumuombea kura Dk. Magufuli huku wakielezea sifa zake.
Khatib alisema Dk. Magufuli anakidhi vigezo vyote vya kuwa rais wa nchi kutokana na uwezo, uchapakazi na uzoefu wa uongozi kwa zaidi ya miaka 20, akiwa mbunge na waziri.
Alisema mgombea huyo ni mzima kiafya, kiakili na kwamba hawezi kulinganishwa na wengine, ambao hawawezi kuzungumza mpaka wapatiwe asali walambe.
Naye Sophia aliwataka wanawake wajitokeze kwa wingi kupiga kura na kumchagua Dk. Magufuli kwa vile ndiye mgombea pekee mwenye sifa zinazotakiwa.
Alisema wapinzani hawana uwezo wa kuongoza nchi kwa vile wagombea wao hawana uwezo wa kuleta mabadiliko. Alisema Dk Magufuli ndiye mgombea pekee mwenye sifa hizo.
Kwa upande wake, Dk. Bilal alisema CCM ndicho chama pekee chenye sifa na uzoefu wa kuongoza nchi kutokana na kutoa marais katika awamu nne tofauti.
Aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi Jumapili kupiga kura na kumchagua Dk. Magufuli awe rais.
No comments:
Post a Comment