Friday 16 October 2015

MBUNGE WA LUDEWA, DEO FILIKUNJOMBE AFARIKI DUNIA



ALIYEKUWA mbunge wa Jimbo la Ludewa kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Deo Filikunjombe, amefariki dunia.

Filikunjombe alifariki dunia juzi katika ajali ya helkopta iliyotokea ndani ya Pori la Akiba la Selous, eneo la Kilombero mkoani Morogoro.


Filikunjombe ni mmoja wa abiria wanne waliokuwa ndani ya chopa hiyo ambao wamethibitishwa kupoteza maisha.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jerry Silaa,Meya wa Manispaa ya Ilala anayemaliza muda wake, baba yake, Kepteni William Silaa, ndiye aliyekuwa rubani wa chopa hiyo ambaye naye amepoteza maisha.

“Kwa masikitiko makubwa nimepokea taarifa rasmi kutoka kwa timu ya uokoaji imefanikiwa kufika eneo la ajali na kukuta abiria wote na rubani wamepoteza maisha,” ilisomeka sehemu ya taarifa ya Jerry Silaa.

“Nimepoteza Baba na rubani mzuri wa nchi yetu Capt.William Silaa,nimepoteza rafiki na kiongozi wangu Deo Filikunjombe. Nawapa pole wote waliopoteza ndugu zao. Nawaombea marehemu mapumziko ya amani.”

“Nawashukuru wote walioshirikiana na familia kusaidia uokozi. Namshukuru Mhe.Rais Jakaya Kikwete, Dr.John Pombe Magufuli, IGP Ernest Mangu, Katibu Mkuu MU Dr.Meru, Kampuni ya Everest Aviation ,Wabunge, MaDC, Maafisa wa TCAA na wote walioshiriki kuwatafuta wahanga wa tukio hili,” ilimaliza sehemu ya Taarifa ya Silaa.

Filikunjombe anakuwa mbunge wa tatu wa CCM kupoteza maisha, zikiwa ni siku chache kabla ya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Mbunge wa kwanza kupoteza maisha alikuwa Selina Kombani, wa Jimbo la Ulanga, aliyefuatiwa na mbunge wa Handeni, Dk. Abdalla Kigoda.


Mungu ailaze roho yake mahali pema, AMEN

No comments:

Post a Comment