Friday, 23 October 2015

MWANZA WASEMA NDIO KWA MAGUFULI



Na Rashid Zahor, Mwanza

KILA kona ilikuwa ni Magufuli, Magufuli, Magufuli. Wengine walisikika wakimwita 'rais, rais, rais'. Pia wapo waliomwita 'baba mwenye nyumba'. Lakini jina maarufu zaidi lilikuwa la 'mzee wa hapa kazi tu.'

Hayo yote yalijidhihirisha Jumamosi ya Oktoba 17, mwaka huu, siku ambayo msafara wa mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, uliwasili Jijini Mwanza kwa ajili ya mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika Jumapili ijayo.

Kabla ya msafara wa Dk. Magufuli kuwasili Mwanza, Jiji hilo lilianza kutawaliwa na pilikapilika na shamrashamra za mapokezi yake kuanzia mapema asubuhi. Shamrashamra hizo zilianza kwa waendesha bodaboda waliokuwa wamezipamba pikipiki zao kwa bendera za Chama, kuziendesha kwa mbwembwe katika barabara mbalimbali za Jiji la Mwanza.

Kilichovutia zaidi, katika maeneo ya katikati ya jiji, vijana wengi walionekana kuwa na furaha kubwa huku wakisalimiana kwa salamu ya 'Hapa Kazi tu'. Salamu hiyo ilikuwa na tafsiri za aina mbili tofauti. Ya kwanza ni kuashiria kaulimbiu ya mgombea urais wa CCM, ambaye ni mchapakazi asiye na mfano. Ya pili ni kwamba walichokuwa wakikijali vijana hao ni kazi  inayowaingizia kipato.

Nyimbo za CCM, hasa ule wa kikundi cha Tanzania One Theatre (TOT), 'Hatunywi sumu hatujinyongi', zilisikika katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mwanza na kuifanya siku ya jana ionekane kuwa maalumu kwa ajili ya Dk. Magufuli na chama chake.

Kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza, wananchi walifurika kuanzia saa nne asubuhi, wakiwa wamevalia sare za CCM. Wananchi hao pia walianza kujipanga kwenye barabara ya kutoka mjini kwenda uwanja wa ndege wa Mwanza kuanzia saa nne asubuhi.

Ndege iliyombeba Dk. Magufuli ilitua kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza saa 8:23 mchana na kupokewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Anthony Diallo na Katibu wa CCM Mkoa, Miraji Mtaturu, na baadaye kuanza safari ya kwenda mjini.

Wingi wa watu waliofurika kwenye uwanja huo na wale waliojipanga barabarani, wakiwa wamesimama kando ya barabara, ulimfanya Dk. Magufuli kusimama juu ya gari lake kuanzia uwanja wa ndege hadi kwenye viwanja vya  Furahisha.

Kwa upande mwingi, polisi wa usalama barabarani na wale wa kawaida, walilazimika kufanya kazi ya ziada kuwazuia wananchi kulisogelea gari la Dk. Magufuli, lakini walijikuta
wakizidiwa nguvu na kuwalazimisha walinzi wa mgombea huyo kushuka na kuwaondoa wananchi hao mbele ya gari hilo.

Pengine kituko kilichowaacha hoi wale wote waliokuwa kwenye msafara wa mgombea huyo ni kitendo cha mama mmoja Mama mmoja kujitokeza ghafla mbele ya gari la Dk. Magufuli na kuanza kupiga push-up. Ilibidi walinzi wa mgombea huyo washuke kwenye gari na kumwondoa ili msafara  uendelee.

Katika baadhi ya maeneo, kina mama walitandika kanga kwenye barabara ili gari la Dk. Magufuli lipite juu yake. Wengine walikuwa wakisafisha barabara kwa mafagio na kupiga deki kwa maji. Polisi walikuwa na kazi ngumu ya kuwazuia.

Wingi wa wananchi waliokuwa wamesimama barabarani, ulimfanya Dk. Magufuli asimamishe msafara wake eneo la Pansiasi na kuwahutubia. Lakini badala ya kumsikiliza, wananchi hao walilipuka mayowe ya 'rais, rais, rais'.

Kutokana na kuwepo kwa wingi wa wananchi barabarani, kuanzia uwanja wa ndege hadi uwanja wa Furahisha, Dk. Magufuli alilazimika kuwaeleza ukweli wananchi hao kwamba
hajawahi kupata mapokezi makubwa tangu alipoanza mikutano yake ya kampeni, kama ilivyokuwa kwa Mwanza.

Hali hiyo ilimfanya Dk. Magufuli awaahidi wananchi hao kuwa, kutokana na kufurahishwa na mapokezi hayo, ataligeuza Jiji la Mwanza na kulifanya liwe Geneva ya Afrika kimaendeleo.

Msafara wa Dk. Magufuli uliwasili viwanja vya Furahisha saa 9:23, alasiri na kuwafanya wananchi walipuke mayowe ya kumshangilia. Viwanja hivyo vilijaa pomoni na hakukuwa na sehemu ya kusimama. Wananchi wengi walilazimika kusimama mbali na viwanja hivyo huku wengine wakiwa wamepanda juu ya soko la Rock City Shooping.

Wakati mkutano wa Dk. Magufuli ukiwa unaendelea, baadhi ya wananchi walikuwa wakikimbia mchakamchaka pembeni mwa viwanja, huku wengine wakiwa wamebeba mfano wa jeneza lililokuwa na rangi za CHADEMA.

Wakizungumza na Uhuru kuhusu mapokezi hayo, baadhi ya wakazi wa Mwanza walieleza kuwa, mkusanyiko huo haujawahi kutokea katika Jiji hilo tangu kampeni kwa ajili ya  uchaguzi mkuu zilipoanza Agosti, mwaka huu.

"Huu mkutano ni zaidi ya ule uliofanywa na Lowassa (Edward, mgombea urais kwa tiketi ya UKAWA). Mkutano huu umejaa watu wa kila aina, vijana, wazee na kina mama. Alipokuja Lowassa, waliokuwepo mkutanoni ni vijana, kina mama walikuwa wachache sana,"alisema Andrew Suka, mkazi wa Nyakato.

Baadhi ya vijana waliohudhuria mkutano huo walisikika wakisema kuwa, walifika kwenye uwanja wa Furahisha wao wenyewe na kwa matakwa yao, bila kusombwa kutoka maeneo mengine kwa kishawishi cha aina yoyote.

Kutokana na wananchi wengi kuhamasika kumsikiliza mgombea huyo, shughuli katika jiji la Mwanza, zilisimama kwa muda, huku maduka na ofisi nyingine zikifungwa.
Msafara wa Dk. Magufuli, uliongozwa na zaidi ya pikipiki 1,000, kutoka uwanja wa ndege mpaka Furahisha.

Wananchi waliokuwa maeneo ya Kona ya Jeshi, Ilemelala, Sabasaba, Butuja, Iloganzala na Pasiansi walifunga barabara kushinikiza mgombea huyo awahutubie na bila ya ajizi alikubali kufanya hivyo.

MAGUFULI ANENA

Akihutubia mkutano huo, Dk. Magufuli, alikiri kuwa tangu alipoanza kufanya mikutano ya kampeni, hajawahi kupata mapokezi makubwa kama aliyoyapata katika Jiji la Mwanza.

"Mwanza mmefunika kweli kweli. Sijawahi kupata mapokezi makubwa na ya aina yake kama haya. Nadhani mnaweza kuongoza Afrika," alisema Dk. Magufuli.

"Sijawahi kuona watu wakijitolea kutembea kwa miguu umbali wa kilometa 12 kutoka uwanja wa ndege hadi mjini. Nina deni kubwa la kufanya kwenu, nalo ni kuwafanyia kazi. Hapa kwangu kazi tu," alisema Dk. Magufuli huku akishangiliwa na wananchi kwa mayowe mengi.

Kutokana na mapokezi aliyoyapata Mwanza na yale aliyoyapata Zanzibar, Dk. Magufuli alisema sasa ana uhakika wa kushinda urais kwa asilimia 99 na kwamba ana imani kubwa atakuwa Rais wa Tanzania.

"Mmekusanyika hapa bila kubagua vyama. Mmekuja kwa umoja wenu. Hapa wapo CUF, CHADEMA na CCM, kwangu wote ni sawa kwa sababu nikichaguliwa kuwa rais, nitakuwa rais wa Tanzania," alisema.

Mgombea huyo wa urais wa CCM, aliwahoji wananchi hao iwapo kuna mgombea mwingine wa urais kutoka vyama vya upinzani, aliyewahi kupata mapokezi kama aliyoyapata yeye na kujibiwa hakuna.

Katika hotuba yake iliyokuwa ikikatizwa mara kwa mara kwa mayowe ya wananchi, Dk. Magufuli alisema serikali yake imepania kufanya mabadiliko ya kweli ya kwenda mbele na pia kuwaondolea umasikini wananchi.

Aliwaahidi wananchi hao kuwa serikali yake itanunua meli mbili za abiria kwa ajili ya usafiri wa Ziwa Victoria na meli nyingine mbili kwa ajili ya kubeba mizigo. Pia aliahidi kujenga barabara ya Usagara/Kisesa kwa kiwango cha lami pamoja na kupanua zile za maeneo ya mjini.

Mgombea huyo pia aliahidi kujenga daraja refu kuliko yote nchini kutoka Kidongo hadi Busisi na kuongeza kuwa michoro ya daraja hilo itaanza kufanyiwa kazi mwaka huu.
Pia aliahidi kurejesha serikalini kiwanda cha ngozi kilichoko mjini Mwanza, iwapo mmiliki wake atashindwa kukiendeleza kabla hajaapishwa kuwa rais.

Siku iliyofuata, Agosti 18, mwaka huu, Dk. Magufuli alifanya mikutano mitatu ya kampeni katika majimbo ya Magu, Kwimba na Misungwi. Pia alifanya mikutano 20 isiyo rasmi, kutokana na wananchi kuzuia msafara wake kwa lengo la kutaka kumuona na kusikiliza sera zake.

UTEUZI WA WAZIRI MKUU

Katika mkutano wake wa kwanza uliofanyika kwenye uwanja wa Sokoni, Magu, Dk. Magufuli alisema serikali yake ya awamu ya tano, iweze kutekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi ya CCM, atalazimika kuteua waziri mkuu mchapakazi.

Dk. Magufuli alisema waziri mkuu huyo ndiye atakayekuwa kiongozi na msimamizi mkuu wa shughuli za serikali, hivyo anapaswa kuwa mchapakazi hodari na makini ili awe mfano wa kuigwa na mawaziri wengine.

Alitoa ahadi hiyo siku chache baada ya kuahidi kuwa baraza la mawaziri atakaloliunda baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, linakuwa na mawaziri wanaofanana naye kiutendaji

Alisema hatakuwa tayari kuwateua mawaziri ambao kazi yao itakuwa ni kukaa tu ofisini na kuandika madokezo, badala yake atateua mawaziri wachapazi na atakuwa akifuatilia utendaji wao wa kazi kwa karibu.

Alisema kabla  hajamteua mtu kuwa waziri, atamuuliza kwanza iwapo ataiweza kazi hiyo na kwamba iwapo atasema anaweza,  atamtaka atiesaini fomu maalumu ya makata. Alisisitiza kuwa, iwapo hawezi, anapaswa kusema mapema kabla ya uteuzi.

"Nataka kama ni waziri wa maji, atembelee miradi ya maji, sio kukaa ofisini. Na kama ni waziri wa elimu, atembelee wanafunzi aone matatizo yanayowakabili. Serikali yangu itakuwa ya kazi tu," alisema Dk. Magufuli katika mkutano huo uliofanyika Jumanne iliyopita, Kisarawe mkoani Pwani.

Aidha, Dk. Magufuli alisema hatakuwa na huruma na mtendaji yeyote wa serikali, ambaye atashindwa kutekeleza maagizo yake kwa wakati. Alisema iwapo atatokea mtendaji wa aina hiyo, atamtimua kazi mara moja.

MIKUTANO ISIYO RASMI

Kabla ya kuhutubia mkutano huo wa kampeni, Dk. Magufuli alilazimika kuhutubia mikutano isiyo rasmi 20 kutokana na msafara wake kusimamishwa na wananchi wakati ulipokuwa ukipita katika maeneo mbalimbali.

Katika mkutano uliofanyika Magu, Dk. Magufuli aliwaahidi wananchi wa wilaya hiyo, serikali yake itazishughulikia changamoto zinazowakabili, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa maji.

Alisema tayari hatua za awali za kuanzisha mradi wa maji katika wilaya hizo zimeshaanza, ikiwa ni pamoja na kupatikana kwa mshauri elekezi, ambaye ameanza kufanya upembuzi yakinifu.

"Hili suala la maji niachieni mimi, nitajitahidi kulibeba. Katika kazi zangu huwa sikubali kushindwa. Nataka kuibadili Magu,"alisema mgombea huyo huku akishangiliwa na wananchi hao.

Aidha, aliahidi kuwa serikali yake itajenga barabara ya Magu/Kwimba kwa kiwango cha lami, ikiwa ni pamoja na za maeneo mengine ya eneo hilo, ili ziweze kutumika kwa ajili ya malori, mabasi na magari madogo.

Dk. Magufuli pia aliahidi kuinua kilimo cha pamba na kupandisha bei ya zao hilo ili wananchi wa wilaya hiyo na zinginezo zinazolima pamba nchini waweze kunufaika kimaisha.

Alisema Tanzania imejaliwa kuwa na raslimali nyingi, zikiwemo bahari, maziwa, mifugo na madini, hivyo wananchi wake hawapaswi kuendelea kuishi wakiwa masikini.

Hata hivyo, Dk. Magufuli aliwaeleza wananchi hao kuwa, ili yote hayo yaweze kufanikiwa, wanapaswa kumpigia kura kwa wingi yeye, wabunge na madiwani wote wa CCM ili waweze kufanyakazi kwa ushirikiano.

"Kama watatokea watu kuwahonga siku ya kupiga kura, kuleni kwa mafisadi lakini kulala kwa Magufuli,"alisema.

Mgombea huyo aliwaambia wananchi hao kuwa mikoa yote aliyotembelea hadi sasa, imemuhakikishia ushindi wa kishindo, hivyo kumfanya awe na uhakika mkubwa wa kuwa Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Ngudu, wilayani Kwimba, Dk. Magufuli aliwaahidi wananchi kuwa, atakapochaguliwa kuwa rais, atamwagiza waziri wake wa kilimo kushughulikia suala la bei ya pamba.

Alisema lengo la serikali yake ni kuhakikisha kuwa, wakulima hawauzi pamba nje ya nchi, badala yake itajenga viwanda kwa ajili ya kutengeneza nguo hapa hapa nchini.

Mgombea huyo pia alisema serikali yake itatilia mkazo uanzishaji wa viwanda vya ngozi ili viatu navyo viweze kutengenezwa nchini.

WANANCHI WAVAMIA MSAFARA

Msafara wa Dk. Magufuri ulianza safari ya kwenda Magu saa 2.30 asubuhi, lakini ulifika huko saa saba mchana kutokana na kusimamishwa mara 18 na wananchi waliokuwa na kiu ya kumuona na kumsikiliza.

Alianza kusimamishwa katika eneo na Mabatini, ambapo wananchi walilizingira gari lake na kulilazimisha kusimama ili waweze kumuona na kusikiliza sera zake.

Masafara wake ulisimamishwa tena eneo la Nyakato, ambako wananchi walijipanga barabarani huku wakipunga hewani bendera na mabango ya Dk. Magufuli na kuimba wimbo wa 'rais, rais, rais.'

Moja ya vituko vilivyomvutia Dk. Magufuli akiwa eneo hilo ni mmoja wa kinamama kutoka nyumbani kwake akiwa amejifunga taulo kiunoni na kanga begani na kulisogelea gari lake. Huku akiwa anacheka, mgombea huyo alimzawadia mama huyo kofia yenye nembo ya CCM.

Msafara wa Dk. Magufuli ulisimamishwa tena eneo la National, ambako kundi la vijana lilifunga barabara na kuanza kupiga push-up. Ilibidi Dk. Magufuli asimamishe msafara wake na kuwahutubia.

Hali iliendelea kuwa hivyo wakati msafara huo ulipofika katika eneo la Igoma, ambako umati wa vijana ulilizingira gari lake na kuimba 'Baba mwenye nyumba,' 'rais, rais, rais.'

Wananchi hao waliendelea kuusimamisha msafara wa Dk. Magufuli katika maeneo ya Kisesa, Nyanguge, Duguye, Kahangala na Ilungu.

Katika mikutano hiyo, ambayo haikuwa rasmi, Dk. Magufuli aliwataka wananchi hao kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi mkuu, uliopangwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu, na kuwapigia kura wagombea wote wa CCM.

Dk. Magufuli pia alitumia fursa hiyo kuinadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM, hasa katika masuala yanayohusu elimu bure ya msingi na sekondari, mikopo ya sh. milioni 50 kwa wanawake na vijana na dhamira yake ya kufuta ushuru ili kuwapa wananchi unafuu wa maisha.

Akiwa njiani kwenda Ngudu, wilayani Kwimba, Dk. Magufuli alilazimika kusimamisha tena msafara wake katika maeneo ya Kabila, Maligisu, Kadashi, Mantare na Sumvua, ambako mamia ya wananchi walifurika barabarani, wakiwa na shauku ya kumuona na kumsikiliza.

Msafara wa Dk. Magufuli uliendelea tena kusimamishwa katika maeneo ya Nyamilama na Gungumalwa, ambako aliwahutubia wananchi kabla ya kwenda Jimbo la Misungwi, wilaya ya Misungwi, ambako alihutubia mkutano wake wa mwisho wa kampeni juzi.

Katika mkutano huo, Dk. Magufuli aliwahakikishia wananchi wa wilaya hiyo kuhusu kuwapatia huduma ya uhakika ya maji safi na salama, ujenzi wa barabara za kiwango cha lami na kuimarisha vivuko vilivyopo, vilivyonunuliwa na serikali ya awamu ya nne.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa makala hii baada ya ujio na mkutano wa Dk. Magufuli mjini Mwanza, umebaini kuwa mgombea huyo ndiye anayekubalika zaidi na wananchi wa mikoa ya kanda ya ziwa kuliko wagombea wa vyama vingine.

Kinachowavutia zaidi wananchi wa kanda hiyo kutoka kwa Dk. Magufuli, ni rekodi yake ya utendaji wa kazi, akiwa waziri katika wizara ya ujenzi, ardhi na maendeleo ya makazi na wizara ya uvuvi.

Kingine kinachomfanya Dk. Magufuli awe kivutio kwa wananchi hao ni kutokuwa na kashfa ya aina yoyote kwa muda wote aliokuwa waziri na kuwa kwake mstari wa mbele kupambana na wala rushwa na mafisadi.

Aidha, msemo wa 'hapa kazi tu' na kuinadi kwake vyema Ilani ya Uchaguzi ya CCM, hasa katika masuala yanayohusu elimu ya bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne, mikopo ya sh. 50,000 kwa vijana na wanawake na azma yake ya kufuta ushuru kwa wajasiriamali ni mambo mengine, ambayo yamemfanya Dk. Magufuli aonekane kuwa mkombozi wa wanyonge.


No comments:

Post a Comment