Na Rashid Zahor, Geita
WAKATI zimesalia siku tatu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amezidi kujihakikishia ushindi wa kishindo katika mikoa ya kanda ya ziwa.
Baada ya kufunga kazi Jijini Mwanza kwa kupata mapokezi mazito na ya aina yake, Dk. Magufuli aliendelea kudhihirisha kuwa ni mtu wa watu na anakubalika, baada ya kupata mapokezi mengine ya aina hiyo katika mji wa Geita.
Maelfu ya wananchi walifurika katika mikutano yake minne iliyofanyika Jumanne iliyopita katika majimbo ya Buchosha, Geita Vijijini, Nyang'wale na Sengerema huku wengine kwa mamia wakisimamisha msafara wake barabarani kwa lengo la kutaka kumuona na kumsikiliza.
Mgombea huyo, ambaye amekuwa kivutio cha aina yake kwa wananchi, kutokana na kuinadi kwake vyema Ilani ya Uchaguzi ya CCM, alijikuta msafara wake ukisimamishwa mara 20 na bila ajizi alisimama na kuwahutubia.
AWATAHADHARISHA WANANCHI
Katika mkutano wake wa kwanza uliofanyika mkoani humo katija jitongoji cha Nyehunge, kilichoko Jimbo la Buchosa, Wilaya ya Sengerema mkoani Geita, mgombea huyo aliwataka Watanzania wasikubali kuuziwa mbuzi kwenye gunia kwa kisingizio cha kuuchukia umasikini.
Alisema baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakijinadi kuwa wanauchukia umasikini, lakini ndio walioifilisi nchi na kuifikisha mahali ilipo na kuwafanya wananchi wake wawe masikini.
Alisema wanasiasa wa aina hiyo hawapaswi kupewa uongozi wa nchi kwa sababu hawana uwezo wa kuiletea nchi maendeleo zaidi ya kutaka kujinufaisha wao binafsi.
Akihutubia mkutano huo huku manyunyu ya mvua yakinyesha, Dk. Magufuli alisema wapo wanasiasa wanaodai kuwa serikali haijafanya lolote kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita, wakati baadhi yao walikuwa mawaziri wakuu wa serikali mbili tofauti na pia washauri wakuu wa rais.
"Hawa ndio waliotucheleweshea maendeleo. Wanadai kwamba serikali haijafanya lolote, wakati waliwahi kuwa viongozi wa serikali. Na wanadai kwamba wanauchukia umasikini," alisema mgombea huyo na kuzielezea kauli hizo kuwa ni sawa na kuwauzia wananchi mbuzi kwenye gunia.
Alisema binafsi licha ya kuwa waziri kwa miaka 20, hakuwahi kupokea rushwa ama kutaka kutajirika, japokuwa wizara yake ilikuwa ikihusika kutia saini mikataba yenye fedha nyingi kuliko wizara zingine.
Alisema umasikini wa Watanzania na kiu ya kuwaletea maendeleo ni miongoni mwa mambo yaliyomshawishi na kumfanya ajitose kuwania urais wa Tanzania kwa lengo la kuwaletea maendeleo.
Dk. Magufuli alisema baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani wamekuwa wakijinadi kuwa watatoa kila kitu bure kwa wananchi, lakini hawaelezi watatumia njia zipi kuzifanya huduma hizo ziwe za bure.
Aliwataka wananchi iwapo watapewa pesa na wapinzani siku ya kupiga kura, Jumapili ijayo, wazipokee na kuzila, lakini kura zao wazielekeze kwa wagombea wote wa CCM.
"Msichague watu wasiokuwa na uchungu na wananchi. Mabadiliko ya kweli ni kufanyakazi na kuwasaidia Watanzania walio masikini,"alisema mgombea huyo huku akishangiliwa na wananchi hao, ambao hawakujali manyunyu ya mvua yaliyokuwa yakiwanyeshea.
Alisema ishara zinazotolewa na wapinzani za kuzungusha mikono hewani kama watu wanaoendesha baiskeli au pikipiki, haziwezi kuwaletea mabadiliko. Alisema shida ya Watanzania sio vyama vya siasa, bali wanataka maendeleo.
Aidha, Dk. Magufuli alisema uamuzi wake wa kufanya kampeni kwa kutumia barabara umelenga kufika katika maeneo mengi nchini na pia kushuhudia kero zinazowakabili wananchi ili aweze kuzitafutia ufumbuzi.
Aliwaahidi wananchi wa Bushosa kuwa atakapoapishwa na kuwa rais wa Tanzania, atatoa kipaumbele kwa ujenzi wa barabara ya Kamanga hadi Sengerema kwa kiwango cha lami.
Katika mkutano wake wa pili uliofanyika kijiji cha Nkome, Jimbo la Geita Vijijini, Dk. Magufuli aliwahakikishia wananchi kwamba atapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa mwaka huu kutokana na kukubalika kwake.
Dk. Magufuli alisema katika mikoa 31 aliyotembelea kwa ajili ya kufanya kampeni, wananchi walimuhakikishia kumpigia kura nyingi ili aweze kuwa rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"Ushindi wa mwaka huu ni wa tsunami. Kote nilikokwenda wananchi wanasema ni Magufuli. Wapinzani wataisoma namba. Wao ni wasindikizaji tu," alisema Dk. Magufuli.
AWAONYA WAVUVI
Katika mkutano huo, Dk. Magufuli pia aliwataka wavuvi katika jimbo hilo na mkoa wa Geita, kujiepusha na uvuvi wa kutumia sumu aina ya thiodan kwa vile unasababisha kutoweka kwa samaki kwenye Ziwa Victoria.
Alisema samaki mmoja aina ya sangara anakuwa na mayai zaidi ya milioni moja na nusu, hivyo anapouawa kwa sumu ni sawa na kupoteza idadi hiyo ya samaki.
Aliwataka wavuvi hao kutunza mazalia ya samaki kwa kuwa iwapo wataendelea kuwaua kwa sumu, watakosa kazi ya kufanya siku zijazo na hivyo kudumaza maisha yao.
"Japokuwa nimekuja kuwaomba kura, lakini lazima niwaambie ukweli. Tumepewa ziwa hili na Mungu, lazima tulitumie vizuri," alisema.
Kabla ya kufika Bushosa, msafara wa Dk. Magufuli ulisimamishwa katika vitongoji vinane, kutokana na wananchi kuwa na kiu ya kumuona na kusikiliza sera zake. Kitongoji cha kwanza ni Kamanga-Kivukoni, ambako msafara wake ulianza saa 3.30 asubuhi.
Msafara wa Dk. Magufuli pia ulisimamishwa katika vitongoji vya Nyamatongo, Katungulu, Kasenyi, Nyamazugo, Ruchili, Bukokwa na Kalebezo.
Akiwa Kalebezo, Dk. Magufuli alisema amefurahi kufika tena katika kitongoji hicho kwa sababu ndiko alikobatizwa katika Kanisa la Kalebezo.
AZURU MAKABURI YA BABU NA BIBI YAKE
Aidha, mgombea huyo wa urais wa CCM pia alitembelea kwenye makaburi ya babu na bibi yake mzaa wa baba, eneo la Katoma, wilayani Geita Vijijini na kufanya ibada ndogo ya kuwaombea dua.
Dk. Magufuli alifika nyumbani kwa babu yake saa 6.30 mchana na kupokewa na baba yake mdogo, Sylvester Magufuli, kabla ya kupelekwa kwenye makaburi hayo, ambako aliongoza ibada ndogo ya kuwaombea dua.
Akizungumza kwenye eneo hilo, Sylvvester alisema makaburi hayo ni ya babu na bibi wa mgombea huyo pamoja na ndugu zake wengine, waliofariki dunia miaka mingi iliyopita.
Alisema asili ya ukoo wa Dk. Magufuli ni Katoma, ambako ndiko baba yake alikozaliwa kabla ya kuhamishia makazi yake Chato.
"Tumezoea kumuona ndugu yetu kwenye tv na kumsikiliza kwenye redio, leo tumefurahi kumuona yeye mwenyewe,"alisema na kuongeza kuwa wanamuombea dua kwa Mungu ili aweze kuchaguliwa kuwa rais wa awamu ya tano ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa upande wake, Dk. Magufuli alisema amefarijika kufika tena katika eneo hilo kwa sababu ndiko alikozaliwa na kukulia na pia ndiko ukoo wake ulikoanzia.
Dk. Magufuli alitumia fursa hiyo kuwatambulisha ndugu zake kwa wanahabari kabla ya kuingia kwenye nyumba ya familia, iliyoko umbali wa mita 30 kutoka barabara itokayo Kamanga kwenda Sengerema.
Mgombea huyo alisema jina la Pombe alipewa na bibi yake, aliyemtaja kwa jina la Anastazia, siku alipoivisha pombe yake.
Alisema babu yake, marehemu Michael, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 1.3 baada ya kumuuguza kwa muda mrefu akiwa Dar es Salaam na baadaye kumrejesha Katoma.
"Kwangu siku hii ni ya pekee. Nilipojua kwamba nitasafiri kwa kutumia njia hii, niliona ni lazima nipite hapa kwa sababu ndiko maisha yangu yalikoanzia,"alisema Dk. Magufuli na kusifu maendeleo yaliyopatikana katika kijiji hicho, ikiwemo nishati ya umeme.
Aliwaomba wakazi wa kijiji hicho wamuombee dua kwa Mungu ili aweze kushinda kiti cha urais, katika uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, unaotarajiwa kufanyika nchi nzima Jumapili.
USHINDI WA TSUNAMI
Akihutubia mkutano uliofanyika kijiji cha Nkome, Jimbo la Geita Vijijini,mgombea huyo alisema mikutano aliyoifanya katika mikoa yote nchini, imemuhakikishia kupata ushindi wa tsunami katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Alisema kote alikokwenda, wananchi wamemuhakikishia kumpigia kura kwa wingi kutokana na kuvutiwa na sera zake, hivyo kumuhakikishia ushindi wa kishindo, ambao ameufananisha na tsumani.
Aidha, mgombea huyo alisema serikali yake itaboresha uvuvi wa samaki katika Ziwa Victoria kwa kuwakopesha wavuvi zana za kuvulia samaki.Alisema lengo la serikali yake ni kuona wavuvi wanafanya biashara na kutajirika, tofauti na ilivyo sasa.
Aidha, alisema serikali yake imepania kufufua viwanda vyote vilivyokufa ili kuongeza ajira kwa vijana na pia kuongeza bei ya zao la pamba ili wakulima waweze kunufaika na kilimo cha zao hilo.
Aliyataja malengo mengine ya serikali yake kuwa ni kuongeza thamani ya matunda yanayolimwa hapa nchini kwa kujenga viwanda vya juisi ili kuondokana na ununuzi wa juisi kutoka nje ya nchi.
"Haiwezekani tukaendelea kuagiza juisi kutoka nje. Ninaposema serikali yangu itakuwa ya viwanda, hiyo ndio dhamira yangu,"alisema.
MSUKUMA ANAVYOKUBALIKA
Katika mkutano huo, Dk. Magufuli alimtambulisha kwa wananchi mgombea ubunge wa CCM katika jimbo jipya la Geita Vijijini, ambaye alishangiliwa kwa mayowe mengi na wananchi, ikiwa ni ishara tosha ya kukubalika kwake.
Msukuma, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita, ni miongoni mwa watu walioleta maendeleo makubwa katika wilaya hiyo kutokana na kuwanunulia wananchi gari la wagonjwa (ambulence) na kumiliki mabasi yanayotoa huduma ya usafiri kati ya wananchi wa jimbo hilo na mengine ya mkoa huo.
Mgombea huyo wa ubunge pia amekuwa akisaidia miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo na hivyo kumfanya awe kipenzi cha wananchi, waliomhakikishia Dk. Magufuli kwamba watampa kura za kishindo.
Siku iliyofuata, Dk. Magufuli alifanya mikutano miwili katika majimbo ya Nyang'hwale na Sengerema, ambako pia alipata mapokezi ya kihistoria, ikiwa ni pamoja na kuhutubia mikutano midogo 10 kutokana na kusimamishwa na wananchi.
AIPIGA STOP NYANG'HWALE
Akiwahutubia wakazi wa jimbo la Nyang'hwale, huku mvua kubwa ikinyesha, aliionya Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’wale mkoani Geita, iachane na mpango wake wa kutaka kukopa shilingi milioni 700 kutokana katika Benki CRDB, kwa vile utawaumiza wananchi.
Alisema mpango huo hauna tija kwa wananchi wa wilaya hiyo mpya, kwa vile itaibidi halmashauri hiyo iwakamue wananchi kulipa riba ya mkopo huo na kuchelewesha maendeleo yao.
Halmashauri hiyo ilikuwa ikitarajia kukopa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kulipa fidia ya ardhi na mali za wananchi wanaopisha ujenzi wa makao makuu ya wilaya na pia nyumba za watumishi.
"Nasema huo mpango wa kukopa fedha CRDB achaneni nao, kama mmekosa fedha za kulipa fidia, subirini zimebaki siku tano, orodheshani majina ya wananchi hao mimi nitaleta fedha mlipe,” aliwaeleza.
Aliamsha shangwe na kushangiliwa kwa nguvu na wananchi hao, aliposema riba ya ya asilimia 18 itakayolipwa kutokana na mkopo huo ni kubwa, hivyo watawakamua na kuwaumiza wananchi.
“Sitaki kuwaingilia, lakini wananchi wanahitaji madawa hospitalini, kwenye zahanati, madawati shuleni na huduma nyingi mbalimbali, kama mmekosa fedha mimi nitakapokuwa rais nitawalipa, hiyo ndiyo kazi yangu ya kwanza hapa,” alisisitiza.
Dk. Magufuli pia aliahidi atakapochaguliwa kuwa rais wa awamu ya tano, atajenga nyumba za wafanyakazi wa halmashauri hiyo kupitia Wakala wa Ujenzi wa Nyumba za serikali (TBA), chini ya Wizara ya Ujenzi, ili mapato ya wilaya hiyo yatumiwe kuhudumia wananchi badala ya kulipa fidia ya mkopo usiokuwa na tija au ulazima kama huo.
Dk. Magufuli, aliyewasili mkoani hapa juzi, akitokea Mwanza na kupokewa kwa shamrashamra na maelfu ya wananchi wa Geita vijijini na mjini, pia alipata mapokezi makubwa na ya heshima kuliko mgombea yeyote wa urais katika majimbo ya Nyang’wale na Sengerema.
Akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano uliofanyika kwenye uwanja wa Mnadani, Dk Magufuli alisisitiza kuwa ahadi ya ujenzi wa barabara za Sengerema- Kamanga, Sengerema-Nyehunge hadi Nkome kwa kiwango cha lami, iko pale pale.
Pia, alisema atakaopingia Ikulu, ataagiza na kusimamia mradi wa maji kutoka katika Ziwa Victoria, unaoendelea kutekelezwa mjini Sengerema, uende haraka na kuondoa kabisa kero ya upungufu wa maji unaoukabili mji huo mdogo.
Awali, wagombe ubunge wa majimbo ya Nyang'hwale (Hussein Nassoro) na Sengerema (William Ngeleja), walimweleza Dk. Magufuli kwamba wananchi wa majimbo hayo wana imani kubwa kwake hivyo watampa kura nyingi.
Kwa upande wake, Hussein alisemaa changamoto kubwa zilizopo jimboni kwake ni uhaba wa maji safi na salama na umeme katika baadhi ya vijiji. Dk. Magufuli aliahidi kuzishughulikia kero hizo baada ya kuingia Ikulu.
Akiwa katika ziara ya wilaya hizo, Dk Magufuli alizuiwa na wananchi wa vijiji vya Kasamwa, Busolwa, Ngoma, Nyanchenche, Tunyeye, Balatogwa na Mtaa wa Ntatukara, Nyapande, Busisi, Kigongo (wilayani Misungwi) na kulazimika kuwasalimia kabla ya kupokewa tena kwa shangwe na mamia ya wananchi aliporejea Jijini Mwanza.
Katika mikutano yote minne iliyohutubiwa na Dk. Magufuli mkoani Geita, baadhi ya wafuasi wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), walieleza wazi kuridhishwa na mgombea huyo, lakini walisema tatizo lao kubwa ni kwa baadhi ya wabunge.
"Hatuna wasiwasi na Magufuli kwa sababu tunamfahamu kuwa ni jembe. Tatizo letu lipo kwa baadhi ya wabunge walioshindwa kutuletea maendeleo licha ya kuwa wabunge kwa zaidi ya miaka 10 na pia kuwa mawaziri,"alisema Athony Charles, mfuasi wa CHADEMA, alipozungumza na Uhuru.
Charles alisema wanaridhishwa na uteuzi wa Magufuli kuwania urais kupitia CCM na kwamba hawana imani na mgombea wao kwa sababu ameonyesha udhaifu mkubwa katika mikutano yake ya kampeni.
Mwanachama mwingine wa CHADEMA, Betty Mkutya, alisema anavutiwa na Magufuli kwa sababu amefanyakazi nyingi za kuiletea nchi maendeleo, isipokuwa tatizo lao lipo kwa wabunge.
No comments:
Post a Comment