Friday 16 October 2015

PEMBA YATIKISIKA



MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya (CCM), Dk. John Magufuli, ametikisika ngome za upinzani visiwani Pemba, huku akiahidi   akichaguliwa kuwa rais, atakuwa kiongozi wa wananchi wote bila kubagua.

Akizungumza katika mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika Gombani ya Kale, Chake Chake, Pemba, Dk. Magufuli alisema hakuomba nafasi hiyo kufanya majaribio, bali amedhamiria kufanyakazi kwa bidii na kuwatumikia Watanzania.

 “Sikuomba nafasi hii kwa majaribio, nimedhamiria kufanyakazi na ninyi na mapokezi yenu ni ishara kubwa kuwa mmenikubali kuwa rais wenu,” alisemaDk.Magufuli.

Alibainisha kuwa akichaguliwa, moja ya malengo ya uongozi wake ni kuulinda Muungano wa Tanzania, ambao aliueleza kuwa una umuhimu wa kipekee.

“Tanzania ni moja na yenye watu wamoja, ndio maana wametapakaa kote kila kona ya Tanzania wakiishi kwa amani, bila kubugudhiana,” alieleza Dk. Magufuli, huku akisalimia wananchi kwa lugha mbalimbali za Tanzania.

Aliwaeleza maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano huo kuwa akichaguliwa atashirikiana bega kwa bega na mgombea urais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, ambaye alimwelezea kuwa mtu makini na mchapakazi.

“Nimefanya kazi na Dk. Shein akiwa Makamu wa Rais… ananifahamu na ninamfahamu na amefika hata kijijini kwangu. Nitaendelea kumheshimu na naahidi kushirikiana naye katika kudumisha Muungano wetu na kuleta maendeleo ya nchi yetu,” alisema.

Alisema alifurahi alipoomba kugombea nafasi hiyo kuwa atapata nafasi ya kufanyakazi na Dk. Shein,  ambaye anamwamini kuwa mtu anayeleta matumaini kwa wananchi.

Katika kuimarisha muungano, alieleza kuwa ataendelea kuzifanyia kazi kero za muungano ambazo alisema zimebaki nne tu na kwamba kwa kuwa mgombea mwenza wake ni Samia Suluhu Hassan, ambaye alikuwa waziri anayeshughulikia muungano, haitakuwa tatizo kuzipatia ufumbuzi.

Kwa hivyo aliwataka wananchi wa Pemba warejeshe mshimakamano wao kwa kuwachagua yeye na Dk. Shein kushika madaraka na hakuna wakati mwingine kwao kufanya mabadiliko wananchi wa Pemba, ila hivi sasa kwa kuwachagua wagombea hao wa CCM.

Aliwataka wananchi wa Unguja na Pemba kutokubali kuchonganishwa na kutengenishwa na wanasiasa ambao wengi wao wamewekeza biashara, makazi na maisha yao Tanzania Bara na kwengineko.

“Sitawaangusha kabisa, ninaomba mnichague niwe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naamini wafuasi wa CUF watanichagua pia kwa kuwa wananipenda mimi Magufuli na Dk. Shein.

“Nimefurahi kwa mapokezi yenu makubwa kisiwani Pemba na makaribisho ya Pemba ni aina yake kwa kuwa nimepokewa na hata wafuasi ya CUF, ahsanteni Pemba,” alisema Magufuli.

Akizungumza katika mkutano huo, mgombea urais wa Zanzibar, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. Ali Mohamed Shein, aliwataka wananchi wa Zanzibar kumchagua Dk.Magufuli kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu ndiye mgombea anayefaa kushika wadhifa huo.

Dk. Shein aliueleza umati wa wananchi hao kuwa uamuzi wa kumteua Dk. Magufuli kugombea nafasi hiyo ni sahihi kwa kuwa Dk. Magufuli ni mtu makini, mchapakazi, anayeiependa nchi yake na Watanzania wenzanke.

"Chama Cha Mapinduzi kilimteua Dk. Mafuguli kutokana na sifa zake na tukishirikiana sote tutaijenga Tanzania kwa mafanikio makubwa zaidi,"alisema Dk. Shein.

 Katika mkutano huo aliwasuta wanaohubiri kuvunja Muungano kwa kueleza kuwa hakuna mtu wala kikundi cha watu wanaoweza kuvunja Muungano huo ambao umedumu kwa miaka zaidi ya hamsini sasa.

'Tulishirikiana katika kutafuta Uhuru wetu, tukafanikiwa na baadaye tukaamua kuungana wananchi wa Tanganyika na Zanzibar na leo ni nchi moja," Dk. Shein alieleza.

Katika mkutano huo Dk. Shein aliwatahadharisha baadhi ya watu ambao wamedhamiria kufanya vurugu wakati wa uchaguzi na kuonya kuwa wasithubutu kufanya hivyo, kwani serikali haitawavumilia.
Alisisitiza kuwa baadhi ya watu hao wanafahamika kwa majina.

No comments:

Post a Comment