Wednesday, 9 December 2015

TUTAULINDA UHURU NA AMANI YETU KWA NGUVU ZOTE- MAGUFULI

RAIS John Pombe Magufuli amesema serikali yake itahakikisha uhuru, amani na umoja, ambavyo ni tunu za taifa, hazichezewi na mtu, kikundi au taifa lolote.

Amesema serikali yake itaendelea kudumisha uhuru wa nchi na Mapinduzi ya Zanzibar, ambavyo ni tunu ambazo msingi wake ni Muungano na Utanzania uliodumu kwa zaidi ya nusu karne.

Amesema hayo kupitia taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari jana, ikiwa ni salamu zake kwa Watanzania, katika maadhimisho ya miaka 54 ya Uhuru wa Tanganyika, yanayoadhimishwa leo nchi nzima.

Hata hivyo, tofauti na ilivyozoeleka, maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika kwa kufanya usafi nchi nzima, ili kutekeleza kauli mbiu ya Uhuru na Kazi. Kauli mbiu hii ilianzishwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere, wakati Tanganyika ilipopata Uhuru kutoka kwa Wakoloni wa Kiingereza mwaka 1961.

Rais Magufuli amesema kaulimbiu hiyo ilikuwa na lengo la kutoa hamasa, moyo na uzalendo wa kufanya kazi miongoni mwa Watanzania kwa kutambua kuwa, uhuru hautakuwa na maana kwao kama hawatafanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kujenga taifa linalojitegemea.

“Watanzania katika miaka ile waliitikia wito huo kwa kufanya kazi za kuwaongezea kipato na katika kuunga mkono juhudi za serikali za kuwaletea maendeleo.

“Katika miaka ya hivi karibuni, moyo na uzalendo wa kufanya kazi miongoni mwetu umepungua sana. Kwa sababu hiyo, niliamua kutumia siku ya kumbukumbu za Uhuru wetu mwaka huu, kukumbushana na kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya UHURU NA KAZI kwa kufanya kazi hususan ya usafi wa mazingira.

“Madhimisho ya Uhuru mwakani yatasherehekewa kama kawaida,” alisema Rais Magufuli kupitia taarifa yake hiyo.

Aidha, Rais Magufuli aliwapongeza viongozi wa mikoa, wilaya na wa taasisi za umma, binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali, ambayo yamejitokeza katika kuhakikisha kuwa kazi ya usafi wa mazingira inafanikiwa.

Alitoa wito kwa halmashauri zote nchini kuhakikisha zinaweka mifumo na taratibu thabiti zitakazowezesha usafi wa miji kuwa endelevu kwa kuachana na visingizio, bali kujijengea uwezo na mamlaka ya kuhakikisha usafi katika miji yao unadumishwa.

Alisema uwezo wa utendaji wa viongozi hao wa mikoa na wilaya utapimwa pia kutokana na hali ya usafi wa miji yao hivyo ni wajibu wa kila kiongozi kuhakikisha eneo lake la utawala linakuwa safi.

“Naomba wananchi tushirikiane katika kuhakikisha kuwa nyumba na mazingira ya nyumba zetu yanakuwa safi na maji ya kunywa katika maeneo ambayo hayawekwi dawa yanachemshwa.

“Wananchi wajizuie kutupa taka hovyo na viongozi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji wahakikishe kwamba kila nyumba inakuwa na choo. Tutashinda vita dhidi ya maradhi kama kipindupindu ikiwa sote tutazingatia kanuni za afya. Kila mtu atimize wajibu wake,” alisema.

No comments:

Post a Comment