Wednesday, 9 December 2015

KIKWETE: SIJAMTUMA MTU KUKWEPA KODI

RAIS mstaafu Jakaya Kikwete na mkewe, Salma Kikwete, wakishiriki kufanya usafi leo Chalinze mkoani Pwani.


RAIS mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, amesema hajawahi kumuagiza mtu yeyote kukwepa kulipa kodi.

Amesema madai hayo yanayotolewa na baadhi ya wanasiasa nchini ni sawa na siasa za majitaka za watu walioshindwa.

Kikwete, ambaye kwa sasa amebaki na kofia ya Mwenyekiti wa CCM, amesema wakwepa kodi hawawezi kuacha kufanya hivyo, na kwamba wanapaswa kuendelea kushughulikiwa.

Alisema hayo leo wakati akiwahutubia wananchi baada ya kushiriki kufanya usafi nyumbani kwake Chalinze mkoani Pwani.




"Afadhali muendelee kunishambulia mimi, lakini mwacheni Rais Magufuli afanyekazi yake,"alisema Kikwete huku akishangiliwa na wananchi.


"Kwanza mimi sigombea tena urais," alisisitiza.

Alisema kamwe hakuwahi kufanya kitu hicho katika maisha yake na kuongeza kuwa, haamini iwapo hata mkewe, Salma Kikwete na mwanawe, Ridhiniwani Kikwete, wangeweza kufanya kitu hicho.
 

Amemtaka Rais John Magufuli kuendeleza mapambano dhidi ya wakwepa kodi na mafisadi na kuwataka wananchi wamwache rais huyo wa awamu ya tano afanyekazi.

Amesema CCM inamuunga mkono Rais Magufuli katika jitihada zake za kupambana na wahujumu uchumi na kuwataka wananchi nao wamuunge mkono.


No comments:

Post a Comment