Saturday, 19 December 2015

WAZIRI MKUU MAJALIWA AAGIZA MRADI WA MABASI WA DART UANZEKAZI IFIKAPO JANUARI 10

WAZIRI Mkuu Kassim Majalia, ametoa agizo kwa wasimamizi wa Mradi wa Mabasi Yaendayokasi (BRT), kuhakikisha mradi huo unakamilika ifikapo Januari, mwakani.

Majaliwa amesema anataka kuona mradi huo unaanza kazi Januari 10, mwakani, hata kama ujenzi wa baadhi ya vituo utakuwa haujakamilika.

Waziri Mkuu amesema hayo leo baada ya kufanya ziara ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya mradi huo katika Jiji la Dar es Salaam.

Aidha, amewaagiza watendaji wa TAMISEMI, ambao ni wamiliki wa mradi huo, kuusimamia vyema ili uanze kufanyakazi na kutoa huduma kwa wananchi haraka.

Tayari mabasi 120 yameshanunuliwa kwa ajili ya mradi huo na yameshafanyiwa majaribio na kuonyesha mafanikio.

Majaliwa pia amewataka wamiliki wa mabasi ya daladala, kuingia mkataba na Shirika la Usafiri la Dar es Salaam (UDA), ili waweze kuendesha mradi huo kwa ushirikiano.

Kuanza kwa mradi huo, kutayafanya mabasi ya daladala yaliyokuwa yakitumia njia hiyo kuhama na kwenda kutoa huduma katika maeneo mengine.

Katika ziara yake hiyo, Majaliwa alitembelea vituo vya Feri, Jangwani, Kimara na Morocco, ambapo aliagiza vituo hivyo vitumike kuanzisha mradi huo wakati vingine vikiendelea kumaliziwa.

No comments:

Post a Comment