Tuesday, 12 January 2016

DK. MWAKYEMBE AWASHUKIA WATENDAJI WABOVU MAHAKAMA ZA MWANZO





WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, amefanya ziara ya kushtukiza kwenye mahakama za mwanzo za Dar es Salaam na kushuhudia kikithiri kwa ubovu wa miundombinu ya mahakama hizo.
Pia, ametoa onyo kwa baadhi ya watendaji wa chombo hicho, watakaoshindwa kwenda na kasi ya serikali ya awamu tano, wajiandae kusaga meno.
Dk. Mwakyembe alifanya ziara kwenye mahakama za mwanzo za Ukonga, Buguruni pamoja na Ilala, ambako licha ya kuwepo katikati ya jiji, zimekosa miundombinu muhimu ya umeme na maji huku vyoo vikiwa kwenye hali mbaya.
Aidha, waziri huyo aliwataka wananchi kufika ofisini kwake kufikisha malalamiko pindi watakapobaini kuporwa kwa haki yao ya kisheria.
Ziara hiyo iliyoifanya jana, kuanzia saa mbili asubuhi, Dk. Mwakyembe, alipofika kwenye Mahakama ya Mwanzo Ukonga, alibaini watumishi wa mahakama hiyo kufanyakazi kwenye mazingira magumu.
Kwa mujibu wa Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Patricia Komba, licha ya jengo hilo kutolewa na wananchi ili kuendeshea shughuli za mahakama, limekosa miundombinu ya maji na umeme.
Pia, alisema kesi zinazofikishwa mahakamani hapo na polisi baada ya kufanyiwa upelelezi, wahusika wamekuwa hawafiki mahakamani kufuatilia mienendo ya kesi hizo.
“Polisi baada ya kufanya upelelezi na kuzifikisha mahakamani kesi husika, wamekuwa hawahudhurii tena. Pia mashahidi nao wamekuwa wakishindwa kujitokeza, hivyo kusababisha kesi kuchukua muda mrefu,” alisema Patricia.
Aliongeza kuwa kutokana na kuimarika mhimili wa kisheria, hakuna umuhimu wa kuendelea kuwepo kwa wazee wa mahakama, ambao hutumika kushughulikia kesi za kimila.
Alisema kuendelea kutumika kwa washauri hao wakati mwingine kunasababisha ucheleweshwaji wa kesi.
Alisema wazee hao wanaweza kuitwa mahakamani pindi yanapojitokeza mashauri yenye kuhusiana na masuala ya kimila.
Akiwa kwenye Mahakama ya Mwanzo Buguruni, Dk. Mwakyembe, alishuhudia chumba cha mahabusu kikiwa ndani ya ofisi ya mahakimu, makarani pamoja na ofisa wa ustawi wa jamii.
Pia, mahakama hiyo ina upungufu wa mahakimu, ambapo licha ya mwaka jana, kupokea mashauri 1,879, ina mahakimu watatu. Mashauri 609 yalitolewa hukumu huku mengine 1,075 yakiondolewa mahakamani.
Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Yairo Thomas, alisema uchakavu wa majengo ya mahakama hiyo unasababisha kuwepo kwa utunzaji hafifu wa majarada ya kesi.
Akizungumza na wananchi kwenye mahakama hizo, Dk. Mwakyembe, alisema wanapaswa kushirikiana na serikali katika kuwafichua watendaji waliopo kwenye mfumo wa mahakama wanaojihusisha na rushwa.
“Huu sio wakati wa kulalamika, kila mwananchi anapaswa kushirikiana na serikali katika kufichua maovu yanayofanywa na baadhi ya watendaji wa mahakama.
“Kama Rais Dk. John Magufuli angekuwa kiongozi mwenye kulalamika, tusingeweza kupiga hatua tuliyofikia sasa,” alisisitiza Dk. Mwakyembe.
Alisema mtumishi wa mahakama, ambaye hatoweza kwenda na kasi ya serikali ya awamu ya tano, ajiondoe.
Alibainisha kuwa, serikali ina mpango wa kuimarisha miundombinu ya mahakama, ikiwemo kuhakikisha kila kata inakuwa na mahakama ya mwanzo.
Kwa mujibu wa Dk. Mwakyembe, mahakama za mwanzo zilizopo kwenye kata ni 976, kati ya kata 3,673 nchi nzima.

No comments:

Post a Comment