NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi, Hamad Masauni, amewataka maofisa uhamiaji kutotumia nafasi ya kukamata
wahamiaji haramu kinyume na matakwa ya serikali pamoja na sheria za nchi.
Aliyazungumza hayo katika
ofisi kuu ya Uhamiaji, Zanzibar, iliyoko eneo la Kilimani, alipofanya ziara ya
kikazi ili kujionea shughuli za utendaji wa ofisi hiyo.
Alisema serikali chini ya
Idara ya Uhamiaji, itapambana na wahamiaji waliopo nchini bila vibali ama
kufuata kanuni na sheria zinazoruhusu ukaazi wao na si vinginevyo.
Alisema wageni wote wenye
vibali vinavyowaruhusu kuwepo nchini, hawatabugudhiwa kwa namna yoyote ile, na
kwamba yeyoye atakayebainika kunyanyasa wageni hao wenye vibali, atachukuliwa
hatua za kinidhamu.
“Tanzania kama ilivyo kwa
nchi nyingine duniani kote, tunapenda wageni, tunajua kwamba watalii na
wawekezaji waliopo nchini wana mchango mkubwa katika kuinua uchumi wa taifa
letu, hivyo hatuwezi kuwafukuza ama kuwanyanyasa kama wako nchini kihalali,”
alisema Masauni.
Aidha, amewataka maofisa
wa uhamiji kutotumia zoezi hilo la kubaini wakaazi haramu kwa manufaa yao na
yeyote atakayebainika kutumia zoezi hilo kinyume na agizo la serikali,
atashughulikiwa kwani serikali haijapanga kuonea wala kunyanyasa mtu yeyote.
Naibu waziri huyo
aliongeza kuwa sheria zilizopo nchini ni kwa ajili ya manufaa ya nchi, hivyo ni
lazima kila mtu aziheshimu na kuwa serikali haina lengo la kutumia sheria hizo
kukandamiza wageni.
Pamoja na hayo, Masauni
alisema serikali ya awamu ya tano imejipanga kutatua kero za wananchi, hivyo
Idara ya Uhamiji itaendelea kuwatumikia wananchi kwa weledi wa hali ya juu na
kuhakikisha kero zote za awali zinatatuliwa.
No comments:
Post a Comment