CHAMA cha Mapinduzi (CCM)
wilaya ya Monduli, kimetangaza vita dhidi ya mapandikizi na mamluki ndani na
nje ya CCM, wanaotumiwa na vyama vya upinzani.
Mapandikizi hayo yamekuwa
yakitumiwa kuhujumu mikakati ya CCM pamoja na kuwagombanisha viongozi na
wanachama.
Mjumbe wa Kamati ya Siasa
Mkoa wa Arusha, Paul Kiteleki, alisema hayo jana, wakati wa kikao cha viongozi
wa CCM kuanzia ngazi ya kata hadi wilaya, wakiwemo madiwani tisa walioshinda kwenye
uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana.
Wengine waliohudhuria
mkutano huo ni Lotha Sanare na Namelok Sokoine, ambapo ilielezwa bayana kuwa
kiama cha wasaliti kimefika.
“Hatuko tayari kuona CCM
Monduli ikisarambatika kwa sababu ya watu wachache. Mnavaa rangi za kijani,
lakini mnafanya kazi za UKAWA. Mbele yenu mnawaona Namelock na Lotha, makada
hawa walikuwa mahasimu wakubwa, lakini kwa sasa tofauti zimeisha na ni kitu
kimoja. Tunataka heshima ya CCM irejee,” alisema.
Aliweka bayana kuwa ndani
ya kikao hicho wapo wanachama, ambao walitumwa kurekodi kila kinachoendelea na
kumpelekea ‘Mzee’, ambaye hata hivyo hakumtaja jina.
Akitoa tamko kwa niaba ya
viongozi hao, Lotha, ambaye amejitosa kuwania nafasi ya uenyekiti wa CCM wilaya
ya Monduli, alimtaka aliyekuwa mbunge wa
jimbo hilo, Edward Lowassa, kuachana na siasa za Monduli na kumtaka atulie
nyumbani kwake.
“Hatutakiwi kuwaacha
wasaliti watambe ndani ya CCM. Lowassa tulimuamini na tukampa heshima, lakini
ameshindwa kuithamini na kukimbilia upinzani. Amechepuka mwenyewe, sisi
tumebaki njia kuu, hivyo nimuombe tu akae nyumbani kwake atulie, atuachie CCM yetu.
“Nimefarijika kumaliza
tofauti zetu na Namelock, ambazo zilisababishwa na watu wanaopenda kufitinisha.
Sasa tuna kazi moja tu ya kuimarisha CCM
Monduli,” alisema.
Naye Namelock alisema
alikaa na kutafakari kwa kina baada ya uchaguzi na kuona, hana sababu ya
kugombana na Lotha, hivyo alilazimika
kumfuata na kumuomba radhi kama kaka yake kwa kutumia njia za kabila lao la
kimasai.
“Nimetafakari nikaona
hakuna haja ya kugombana na kaka yangu. Tulikuwa na mgogoro mkubwa kipindi cha
kampeni za ubunge, lakini hakuwa na kinyongo, aliniombea kura,” alisema.
Baada ya kikao hicho,
wajumbe waliwasindikiza Namelok na Lotha katika ofisi ya Katibu wa CCM Wilaya
kurudisha fomu ya kuwania nafasi ya mwenyekiti na Namelock aliyekuwa
akirejesha fomu ya kuwania nafasi ya
ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC)
ya CCM.
No comments:
Post a Comment