Tuesday, 12 January 2016

SERIKALI YADHIBITI ULANGUZI WA ARDHI, YAANDAA UTARATIBU WA BEI ELEKEZI




SERIKALI imetangaza kuandaa waraka wa bei elekezi wa uuzaji wa ardhi, tofauti na utaratibu holela unaotumika kwa sasa.
Imesema utaratibu wa sasa unawafanya wananchi wa kipato cha chini kushindwa kuwa na haki ya kumiliki ardhi, hivyo kutoa mwanya kwa wenye uwezo kujilimbikizia maeneo makubwa.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi, amesema baadhi ya watu wamekuwa wakiuziwa viwanja kwa bei ya juu na kuwafanya masikini kushindwa kujenga nyumba kwa ajili ya makazi na familia zao.
Lukuvi aliyasema hayo mjini hapa jana, wakati alipofanya ziara kubaini kero zinazowakabili wananchi mkoani Pwani, ambapo pia alielezwa mambo mbalimbali.
Alisema baadhi ya watu wameifanya ardhi kama kitega uchumi kwa kujinufaisha na kununua mashamba kisha kuyagawa viwanja na kuuza kwa bei kubwa, jambo ambalo halipaswi kuachwa.
“Ardhi isigeuzwe kitega uchumi ama biashara wakati ni huduma na huduma haipaswi kutozwa gharama kubwa. Utashangaa eneo kama Kibaha kiwanja kinauzwa sh. milioni 10. Hali hii hatuwezi kukubali iendelee,” alisema Lukuvi.
Alieleza kuwa watu wanaomiliki ardhi kwa muda mrefu na kufanya kama rehani kwa ajili ya kukopa fedha katika benki na taasisi za fedha nao wamekuwa ni tatizo kubwa.
Lukuvi alisema kuanzia sasa watahakikisha wanawafuatilia watu hao ili wanapoomba fedha, lazima waendeleze maeneo ambayo wameyakopea na si kufanya sehemu ya kujichukulia mtaji na kuendeleza biashara zingine.
Aidha, alisema kwa watu waliochukua ardhi na kuiweka akiba, hawapaswi kufanya hivyo kwa kuwa serikali ndiyo yenye uwezo wa kuweka akiba na si mtu binafsi.
Kwa upande wa halmashauri, alizitaka kutofanya ardhi kama sehemu ya mapato kwani kazi yao ni kupanga miji pamoja na kutoa huduma kwa wananchi.
“Msifanye ardhi kama sehemu ya kujipatia mapato kwani baadhi ya halmashauri zimekuwa zikiwanyang’anya ardhi wananchi na kupima kisha kuuza viwanja kwa bei kubwa, ambapo wananchi wa kawaida wanashindwa kununua,” alieleza Lukuvi.
Alisema halmashauri ambayo itafanya hivyo, inapaswa kuwalipa kwanza fidia wananchi kabla ya kuviuza na kwa wale waliochukuliwa maeneo yao, wanapaswa kulipwa fidia.
Katika hatua nyingine, Lukuvi alisema ifikapo Juni, mwaka huu, hatatambua ofa, hivyo halmashauri zinatakiwa kutoa hati zitakazotambulika kwani, baadhi waliomba hati tangu mwaka 2013, lakini hawajapewa na kuanzia sasa hati zitakuwa zikitoka mapema zaidi.
Ofisa Ardhi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Edward Mbala, alisema viwanja 3,050 vilipimwa licha ya wamiliki wengi kutopata hati zao.
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Halima Kihemba, alisema atahakikisha changamoto zote zilizoonekana wakati wa ziara ya Lukuvi zinafanyiwa kazi ili kuondoa malalamiko.

No comments:

Post a Comment