SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amewateua wabunge 15 kwenye
Kamati ya Kudumu ya Kanuni za Bunge, itakayokuwa na jukumu la kufanyia
marekebisho ya nyongeza ya nane ya kanuni za kudumu za bunge.
Pia, kamati hiyo itakuwa na jukumu la kuaninisha
majukumu ya kamati zingine za bunge na serikali kwa kuzingatia muundo wa baraza
la mawazili lililopo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa
jana na Ofisi ya Bunge, kamati hiyo itaongozwa na Spika, ambaye ni Mwenyekiti,
Makamu Mwenyekiti wake ni Naibu Spika, Dk. Tulia Atson pamoja na Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, Geogre Masaju na kiongozi wa kambi ya upinzani.
Wajumbe wengine ni Makame Kassim
Makame, Mbunge Jimbo la Mwera, Tundu
Lissu, Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Jasson Rweikiza, Mbunge wa Jimbo
la Bukoba Vijijini, Dk. Charles Tizeba, Mbunge wa Jimbo la Buchosa na Ally
Saleh Ally, Mbunge wa Jimbo la Malindi.
Wengine ni Magdalena Sakaya, Mbunge
wa Jimbo la Kaliua, Salome Makamba, Mbunge wa
Viti Maalumu, Dk. Jasmine Bunga, Mbunge wa Viti Maalumu,
Zainab Katimba, Mbunge Viti
Maalumu, Balozi Adadi Rajab, Mbunge wa Jimbo la Muheza pamoja na Kangi Lugola, ambaye
ni Mbunge wa Jimbo la Mwibara.
Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa,
Spika atakamilisha uteuzi wa wajumbe katika kamati zingine za Bunge kabla ya
kuanza kwa mkutano wa pili wa bunge, Januari 26, mwaka huu, ili kutoa fursa kwa
kamati zote kuchagua viongozi wake na kuandaa mpango kazi kwa mwaka 2016/17.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 116 (3) ya
Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Aprili, 2013, Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano amepewa mamlaka ya kuteua wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa
namna, ambayo itawezesha kila mbunge kuwekwa kwenye kamati mojawapo.
No comments:
Post a Comment