Monday 4 April 2016

UJERUMANI YAIPATIA TANZANIA NDEGE YA DORIA




SERIKALI ya Ujerumani imetoa msaada wa ndege maalumu aina ya ‘Husky A-1C Aircraft’ kwa serikali ya Tanzania, kwa ajili ya kusaidia katika doria za kupambana na ujangili katika Hifadhi ya Akiba ya Selous.
Msaada huo wenye thamani ya Euro 200,000 (sh. milioni 498, 292,000),ulikabidhiwa mwishoni mwa wiki, kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe na Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Serikali ya Shirikisho la Ujerumani, Dk. Gerd Muller, katika hafla iliyofanyika Matambwe, ndani ya Pori la Akiba la Selous.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na maofisa wa ubalozi wa Ujerumani walioko nchini, wakiongozwa na Balozi Egon Konchanke, viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii,          Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mashirika ya Maendeleo ya Kimataifa ya FZS, WWF, GIZ na KFW.
Akizungumza katika hafla hiyo, Profesa Maghembe alisema ndege hiyo itasaidia jitihada za serikali za kupambana na ujangili, kwa kufanya doria katika anga ya hifadhi ya akiba ya Selous na kusaidia kutoa taarifa za kiuhalifu pale itakapobainika na kuchukuliwa hatua stahiki za kukabiliana na uhalifu huo.
“Ndege hii tunayoshuhudia mapokezi yake leo ni ukombozi kwa wanyamapori katika pori hili la akiba la Selous, kwani itasaidia na kuimarisha doria za kupambana na ujangili ndani na kuzunguka eneo zima la hifadhi,” alisema.
Profesa Maghembe aliishukuru serikali ya Ujerumani kupitia kwa Waziri Muller, kwa msaada huo na mingine, ambayo wamekuwa wakiitoa kusaidia uhifadhi wa wanamapori nchini.
Alisema misaada hiyo imekuwa na tija kubwa katika kuendeleza uhifadhi wa wanyamapori, ikilinganishwa na kipindi cha nyuma kabla ya kuwepo kwa misaada hiyo.
Waziri Maghembe alisema sera ya wanyamapori Tanzania inatambua ushirikiano wa wahisani na watu binafsi katika kuisaidia serikali kifedha na kitaaluma kwenye eneo la uhifadhi, hivyo amewaomba wadau mbalimbali kuendelea kuipa ushirikiano serikali katika jitihada zake za kuendeleza uhifadhi wa wanyamapori nchini.
Kwa upande wake, Dk. Muller alimueleza Profesa Maghembe kuwa serikali ya Ujerumani itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza uhifadhi hapa nchini.
Aliwapongeza askari wa wanyamapori kwa kazi nzuri wanayofanya ya kulinda wanyamapori katika mazingira magumu ya porini.
Dk. Muller alisema ipo haja ya kuendelea kuwalinda wanyamapori kwa nguvu zote kwa kuwa hawana hatia na kwamba, walikuwepo katika mazingira yao ya asili kabla hata ya binadamu kuwepo duniani.
Akizungumza kabla ya tukio la kukabidhiwa ndege, Meneja wa Pori la Akiba la Selous, Mabula Misungwi, alizitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili hifadhi hiyo kuwa ni ujangili, miundombinu mibovu ya barabara kwa ajili ya doria na vifaa, ikiwemo magari ya doria.

No comments:

Post a Comment