TAARIFA za
watu wanaodaiwa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi
wa Elimu ya Juu (HESLB), zitawasilishwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), hivyo kuwanyima
fursa ya kupata mikopo katika taasisi za fedha.
Hatua hiyo
inatokana na HESLB kutia saini mkataba na Kampuni ya CreditInfo Tanzania,
utakaowezesha taarifa za wadaiwa wa mikopo ya elimu ya juu kufikishwa katika
Kitengo cha Uratibu wa Taarifa za Mikopo kilichoko BoT.
Kampuni ya CreditInfo
ina leseni iliyotolewa na BOT kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.
Hivyo, mnufaika wa
mikopo ya elimu ya juu, ambaye ataomba mkopo kutoka taasisi yoyote ya fedha
hapa nchini, taasisi husika itakuwa na uwezo wa kuhakiki kama mwombaji huyo ni
mnufaika wa mkopo wa elimu ya juu na kama ana nidhamu ya kurejesha
mikopo.
Kwa mujibu wa mkataba
huo, HESLB itawasilisha orodha ya wadaiwa wa mikopo ya elimu ya juu kwa
CreditInfo, ambayo itahakikisha taarifa za wakopaji kwa taasisi zote za
kifedha, zikiwemo benki, ili taasisi hizo zijiridhishe kabla ya kutoa mikopo
mipya kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu.
“HESLB ina
furaha kufanya kazi na CreditInfo kama mdau mpya. Tunawasihi wanufaika wa
mikopo ya elimu ya juu waanze kulipa madeni yao ili wawe na hadhi ya kukopesheka
na taasisi za kifedha,” alisema Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Jerry Sabi,
wakati wa hafla fupi ya kutia saini mkataba huo.
Kwa upande
wake, Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Davith Kahwa, alisema lengo la kampuni
hiyo ni kuhakikisha fursa za ukopaji zinaongezeka na wakopaji wanakuwa na
nidhamu kwa mikopo waliyopata.
“Wanufaika wa
mikopo ya elimu ya juu, ambao wamekuwa wakilipa, watapata fursa ya kipekee ya
kujadiliana na taasisi za kifedha kuhusu viwango vya riba kwa sababu ya nidhamu
wanayoionyesha kwa mikopo yao,” alisema.
Aliongeza: ”Tumedhamiria
kuiunga mkopo HESLB katika kutekeleza majukumu yake, hususan yale ya ukusanyaji
mikopo iliyoiva.”
Hadi sasa, zaidi ya sh. trilioni 2.1
zimetolewa kwa Watanzania na kati ya hizo, sh bilioni 258, zimeiva, hivyo
kutakiwa kukusanywa kutoka kwa wanufaika.
No comments:
Post a Comment