Monday 4 April 2016

JPM: TUIOMBEE NCHI AMANI NA UTULIVU




RAIS Dk. John Magufuli, amewataka Watanzania kuendelea kuliombea taifa ili liendelee kuwa na amani na utulivu.
Dk. Magufuli yuko mapumzikoni nyumbani kwake, Lubambangwe, katika Kijiji cha Mlimani, Wilaya ya Chato mkoani Geita.
Alitoa wito huo jana, alipoungana na waumini wenzake wa Kanisa la Bikira Maria Parokia ya Chato, kusali ibada ya Jumapili ya Pili ya Pasaka.
“Niwaombe Watanzania wote tuendelee kushirikiana na kushikamana kwa umoja wetu na siku zote tumtangulize Mwenyezi Mungu.
“Wakati tunaadhimisha wiki moja baada ya kufufuka kwa Bwana Wetu Yesu Kristo, Yesu Kristo alikufa kwa sababu ya dhambi zetu, sisi wote tujitahidi kufuata matendo ya Yesu Kristo ya kusameheana, kupendana, kushirikiana na tusibaguane,” alisisitiza Rais Magufuli.
Ibada hiyo pia ilihudhuriwa na mke wa Rais, Mama Janeth, Waziri Mkuu mstaafu wa Kenya, Raila Odinga na mkewe, Mama Ida, ambao ni familia rafiki wa Rais Magufuli.
Odinga na mkewe waliwasili Chato, juzi, kwa mapumziko wakitokea Nairobi, Kenya.
Katika salamu zake kwa waumini wa Parokia ya Chato, Odinga aliwashukuru Watanzania kwa uhusiano mzuri walionao na Wakenya.
Alitoa mfano wa jinsi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alivyojitoa kupigania uhuru wa mataifa mengi ya Afrika, ikiwemo Kenya.
Odinga alitoa mfano wake kuwa Mwalimu Nyerere alimpatia pasi ya kusafiria ya Tanzania, aliyoitumia kwa miaka mitatu kwa ajili ya kwenda kusoma nje ya nchi, baada ya utawala wa kikoloni wa Kenya kukataa kumpa pasi.
Kuhusu urafiki wake na Rais Magufuli, Odinga alisema ulianza tangu Rais Magufuli alipoteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi na yeye kuwa waziri mwenye dhamana ya ujenzi wa Kenya.
Alisema mara kadhaa walibadilishana uzoefu na kushirikiana katika mipango ya miradi ya ujenzi wa barabara na kwa umuhimu huo, alitoa wito kwa nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki kuendeleza ushirikiano na mshikamano ulioasisiwa na Mwalimu Nyerere.
Katika hatua nyingine, Rais Dk. Magufuli, alitoa mchango wa sh. milioni 10 kwa Kanisa la Bikira Maria Parokia ya Chato, mkoani Geita, kwa ajili ya kuchagia upanuzi wa kanisa hilo.
Fedha hizo zilikabidhiwa na Kaimu Mnikulu, Ngusa Samike, katika misa ya pili ya Ibada ya Jumapili ya Pili ya Pasaka, iliyofanyika kanisani hapo, jana.
Katika misa hiyo, Paroko wa Parokia ya Chato, Padri Henry Mulinganisa, alisema kanisa hilo linatarajia kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake baadaye mwaka huu.
Alisema maadhimisho hayo yanakwenda sambamba na upanuzi wa kanisa hilo, ambao unachangiwa na waumini wenyewe.
Padri Mulinganisa alimshukuru Rais Magufuli kwa mchango huo na aliahidi kuwa utatumika vizuri ili uendeleze upanuzi wa kanisa hilo na michango ya waumini wengine.

No comments:

Post a Comment