JESHI la Polisi mkoani Mwanza
limeagizwa kuwasaka na kuwakamata mara moja majambazi wanaofanya mauaji na
uporaji kwa kutumia silaha.
Mbali na hilo,
wameagizwa kuhakikisha wanavunja makundi ya mitandao saba ya uhalifu inayodaiwa
kuwepo Mwanza.
Agizo hilo
limetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, mjini
Misungwi, jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Kitwanga alitoa
agizo hilo muda mfupi baada ya kukabidhi baiskeli 118, zenye thamani ya sh. milioni
21.2, kwa makatibu wa CCM wa matawi 118, ya jimbo lake, ikiwa ni utekelezaji wa
ahadi yake ya kuimarisha Chama.
Agizo hilo alilitoa
kufuatia uporaji wa fedha kwenye maduka ya miamala ya fedha (M-Pesa) na mauji
mfululizo, yaliyotokea kuanzia mwezi uliopita hadi juzi, jijini hapa, na
kusabaisha watu sita kupoteza maisha na zaidi ya 10, kujeruhiwa katika maeneo
ya Shede, Nyegezi, Bugarika na Temeke Nyakato, wilayani Nyamagana.
“Polisi na serikali
yetu chini ya Rais Dk John Magufuli, tunawahakikishia wananchi kuendelea
kuwatumikia kwa vitendo na kukomesha uhalifu huo ili wananchi waendelee na
shughuli za kujiletea maendeleo bila hofu. Tumebaini kuwepo mitandao saba ya
uhalifu na tayari miwili tumeivunja, nawaagiza polisi mitano iliyosalia
isambaratishwe haraka,”alisema
Alisema kuendelea
kwa uhalifu na mauaji kunawapa hofu wananchi juu ya usalama wao na mali zao, hivyo ni lazima jeshi hilo liendelee kupambana
na watu wanaoendesha matukio na vitendo vya uhalifu vinavojitokeza ili wananchi
waishi bila hofu.
Aliwaonya askari
wachache wanaodaiwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu, ikiwemo kushirikiana na
majambazi waache mara moja.
“Sisi wananchi ni wengi, wahalifu ni wachache,
tutashinda na nawambia ole wao,” alisisitiza.
Akizungumzia
utekelezaji wa Ilani ya CCM na ahadi yake ya kuwawezesha usafiri makatibu hao,
alisema alitoa ahadi hiyo mwaka jana, lakini kutokana na mchakato wa uchaguzi mkuu,
alishindwa kuitekeleza kwa kuhofia kuwa ingeonekana ni moja ya kuwashawishi
viongozi hao wampigie kura.
Alisema nyenzo
hizo siyo mali ya mtu binafsi, ni mali ya Chama, hivyo viongozi hao wazitunze
ili ziwawezesha kutekeleza majukumu yao, ikiwa ni pamoja na kuimarisha uhai wa
CCM, kwa kuwatembelea mabalozi, wanachama na kutatua kero za wananchi.
Akimpongeza kwa
hatua ya kuimarisha Chama na kutekeleza Ilani, Katibu wa CCM mkoani Mwanza,
Miraji Mtaturu, alisema Kitwanga ni mfano wa kuigwa na wana-CCM wengine wenye
uwezo, kwani ushindi wa CCM katika chaguzo zote hutokana na viongozi wa mashina
na matawi.
Mtaturu aliahidi
kuwa CCM mkoani Mwanza itaendelea kuwathamini viongozi wake wote, hususan wa
ngazi hizo na kuhakikisha wanawawekea mazingira mazuri ya utendaji kazi,
tofauti na vyama vingine vya msimu kama wa maembe.
No comments:
Post a Comment