Saturday 16 July 2016

SERIKALI YAMJIBU DK. MWAKA NA WENZAKE

SERIKALI imetoa ufafanuzi  wa hatua iliyochukua baada ya kufungiwa baadhi ya vituo vinavyotoa huduma za tiba asili na tiba mbadala ambapo imedai vituo hivyo vimekua vikikiuka  taratibu na sheria.

Imesema kamati ya maadili ilikutana na baadhi ya matabibu Juni 17 -22 mwaka huu ambapo imebaini vimekua vikikiuka katika utoaji wa huduma hiyo na kujadili kwa kina ripoti ya matabibu waliotuhumiwa na kutoa maazimio ya kuzifungia.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Nsachri Mwamwaja, alisema maazimio hayo yalimkuta tabibu, Juma Mwaka, na kosa la mara kwa mara la kurusha matangazo zaidi ya yale aliyopewa kibali.

Alisema baraza huwa linalotoa idhini baada ya kupitia matangazo na kumuita, lakini hakufika na badala yake akamtuma mwakilishi ambaye hakua na utambulisho wala  utaaluma wa tiba mbadala.

Pia, alisema katika ripoti hiyo tabibu, John Lupimo, ana tabia ya kurudia makosa aliyoonywa na baraza katika matangazo yaliyorushwa na radio Ebon saa 3.15 usiku na katika kipindi cha chereko kinachorushwa na Shirika la Utangazaji [TBC] akielezea uzazi, shinikizo la damu na tatizo la choo kigumu ambapo ni kinyume na sheria.

“Kutokana na kuwa kinyume na sheria ya tiba asilia na mbadala, tabibu Abdallah alijitangaza kuwa yeye ni tabibu wa tiba asili na anaendelea kutangaza licha ya kupewa barua na baraza kusitisha matangazo  hayo mara moja”alisema Mwamwaja.

Mwamwaja aliwataja Castor Ndulu na Esbon Baroshigwa, ambao walikutwa na kosa la utoaji elimu ya tiba mbadala na tiba asili kinyume na tamko la Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee ambalo lilitolewa Januari mwaka huu na kwamba walikiri kosa lao na kupewa adhabu ndogo.

No comments:

Post a Comment