Saturday 16 July 2016

MAKAMU WA RAIS KUHUDHURIA MKUTANO WA AU RWANDA

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, anatarajia kuondoka nchini kesho kwenda Kigali nchini Rwanda, kwa ajili ya kuhudhuria mkutano wa 27 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU).

Taarifa iliyotolewa jana na Ofisi ya Makamu wa Rais, ilisema Samia atamwakilisha Rais Dk. John Magufuli katika mkutano huo wa siku mbili ambao unatarajiwa kufanyika Kigali, Rwanda kuanzia kesho.

Katika Msafara wake, Makamu wa Rais, Samia atafuatana na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Zanzibar, Issa Haji Ussi.

Mkutano huo ambao utahudhuriwa na Makamu wa Rais utaanza kwa vikao vya ndani ambapo viongozi watajikita katika kujadili masuala ya kimkakati ikiwemo umuhimu wa kuliunganisha Bara la Afrika kibiashara kwa kuwa na soko la biashara huria ifikapo mwaka 2017 pamoja na mageuzi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Aidha, wajumbe wa mkutano huo wa 27 wa AU pia watachagua Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika pamoja na Makamu wake, makamishna wanane wa sekta mbalimbali na majaji wanne wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu.

Pia, watapitisha mapendekezo kuhusu gharama za uendeshaji wa umoja huo na bajeti ya fedha ya mwaka 2017.

Makamu wa Rais, Samia na ujumbe wake wanatarajia kurejea nchini Jumanne baada ya kumalizika kwa mkutano huo.

No comments:

Post a Comment