Saturday 16 July 2016

TANZANIA YAKABIDHI BAWA LA NDEGE YA MALAYSIA

SERIKALI ya Tanzania  imeikabidhi serikali Malaysia na Australia bawa la ndege linalohisiwa kuwa ni la ndege  ya Malaysia  aina ya MH370, iliyopotea mwaka 2014 ikiwa na watu 239.

Makabidhiano hayo yalifanyika  jijini  Dar es Salaam, jana  makao makuu ya  Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).

Akikabidhi bawa hilo kwa niaba ya serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dk. Leonard Chamuriho, alisema bawa hilo lilipatikana katika Bahari ya Hindi na mvuvi aitwaye Changua Hamad Changua, mkazi wa Zanzibar.

Alisema mvumvi huyo alilivua bawa hilo Juni mwaka huu na baadae kuwasiliana na kitengo cha kufuatilia ajali za ndege Wizara ya  Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Alisema timu ya wataalamu ilikwenda Zanzibar,  kwa ajili ya uchunguzi zaidi ambao ulibaini kuwa lilikuwa ni bawa la ndege.

Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari, alisema uchunguzi ulionyesha kuwa bawa hilo ni la ndege kubwa aina ya Boing 777.

“Kwa upande wa Tanzania  hatujawahi kupata ajali ya ndege kubwa ya aina hiyo, hivyo tulihisi pengine ni bawa la ndege ya Malaysia iliyopotea,”alisema Johari.

Alisema baada ya kulisafirisha bawa hilo kutoka Zanzibar,  serikali ya Tanzania iliwasiliana na nchi za Malaysia na Australia  kwa ajili ya uchunguzi zaidi, ambapo nchi hizo ziliahidi kutuma watalaamu wake kwa ajili ya kushughulikia suala hilo.

Katika makabidhiano hayo Malaysia iliwakilishwa na Mkaguzi Mwandamizi  wa Ajali za Ndege kutoka Wizara ya Uchukuzi ya nchi hiyo, Aslam Bash Khan, ambaye aliipongeza Tanzania na Watanzania kwa kuonyesha ushirikiano mkubwa wa kubaini ajali ya ndege hiyo.

Alisema bawa hilo litasafirishwa hadi nchini Australia ambako kuna maabara kubwa ya  kimataifa ya uchunguzi  wa ajali  ya ndege.

Khan alisema uchunguzi wa kubaini kama bawa hilo ni la ndege ya Malaysia iliyopotea, utafanywa chini ya jopo la wataalamu kutoka nchi saba ambazo ni Australia, Malaysia, Marekani, Ufaransa, China Uingereza na Singapore.

Mkaguzi Khan alisema hadi sasa hakuna mwili uliopatikana kutokana na ajali hiyo na kusema ni vipande 10 tu ndivyo vilivyopatikana  vikihisiwa kuwa ni vya ndege hiyo.

Alisema miongoni mwa vipande hivyo baadhi vilipatikana katika bahari ya Hindi katika kisiwa cha Madagascar kilichopo barani Afrika.

“Nashukuru kwa jitihada kubwa zilizofanywa na serikali ya Tanzania na wananchi katika kushughulikia suala hili. Tunaomba wananchi waendelee kutusaidia hususan pale wanapoona mabaki ambayo wanahisi ni ya  ndege,”alisema Khan.

Alisema, wanahisi vipande na masalia ya ndege hiyo vilisukumwa na maji hadi upande wa Mashariki mwa bahari ya Hindi.

“Upatikanaji wa vipande hivi utatusaidia kwa kiasi kikubwa katika uchunguzi wetu juu ya ajali hiyo,”alisema Khan.

Katika makabidhiano hayo, Australia  iliwakilishwa na Balozi wake anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki John Feakes na ofisa kutoka nchini humo, Diana Simpson.

Fakes aliipongeza Tanzania kwa ushirikiano mkubwa ilioutoa kukabidhi bawa hilo utakaosaidia kufanikisha uchunguzi wa ajali ya ndege hiyoya Malaysia.

“Tunampongeza  mwananchi aliyeopoa bawa hili Changua kwa kutoa taarifa za haraka baada ya kulipata. Naomba ushirikiano huu uendelee ili kufanikisha  kazi hiyo,”alisema  Fakesa.

Bawa hilo la ndege lilisafirishwa jana hiyohiyo kwenda nchini Australia  kupitia kampuni ya kimataifa ya usafirishaji mizigo ya DHL, ambapo gharama za usafirishaji kwenda nchini humo zitatolewa na serikali ya  nchi hiyo, huku gharama za kulisafirisha bawa hilo kutoka Zanzibar kuja Tanzania Bara zilitolewa na serikali ya Tanzania.

Ndege hiyo ilipotea mwaka 2014 iliporuka kutoka nchini humo ikilielekea nchini China ikiwa na watu 239. Tangu wakati huo hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyepatikana akiwa hai au maiti.

No comments:

Post a Comment