Monday 4 April 2016

TPA YATAKA KODI YA MIZIGO YA NJE IPUNGUZWE




MAMLAKA ya Bandari Tanzania (TPA, imeiomba serikali kuchukua hatua za haraka kunusuru tatizo la kupungua shehena za mizigo kutoka nchi jirani linaloongezeka kwa kasi.
Kwa kipindi cha mwaka mmoja, shehena ya magari yaliyokuwa yakipitishiwa bandari ya Dar es Salaam na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), imepungua kwa asilimia 50, huku shehena ya Zambia ikipungua kwa asilimia 49.
Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari nchini hivi karibuni, Kaimu Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Habel Mhanga, alisema moja ya sababu zinazochangia kupungua kwa kasi kwa shehena ya mizigo ni pamoja na utozaji kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika mizigo ya nje.
Meneja huyo alisema kuanzishwa kwa mfumo wa utozaji kodi, kumezua manung’uniko miongoni mwa watumiaji wa bandari, hususan kutoka nje ya nchi, wanaosema kutokana na utaratibu huo, wamekuwa wakilipia ushuru mara mbili.
Alisema wamekuwa wakipokea malalamiko juu ya VAT kwamba, wafanyabiashara hutozwa kodi mara mbili, ambapo mbali na kulipia Tanzania, pia hulazimika kulipia kodi kama hiyo katika nchi zao.
“Kutokana na madai hayo, wanaamua kutafuta bandari zingine, ambazo ni washjindani wetu, ambazo hazina utaratibu wa kutoza VAT na kusababisha kupungua kwa mizigo yao hapa wetu,” alisema.
Kwa mujibu wa meneja huyo, sababu nyingine inayochochea kupungua kwa mizigo bandarini hapo ni kutokana na mfumo wa ulipaji kodi pamoja (Single Custom Territory), unaomlazimu mteja kulipia ushuru hapa Tanzania kwa asilimia 100.
Mhanga alisema hatua hiyo inalalamikiwa kuwabana wafanyabiasha, hususan kutoka nje ya Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), ambao hulazimika kwenda kulipia tena kodi katika nchi zao.
“Baadhi ya wateja wanaamua kuacha kupitisha mizigo yao Dar es Salaam, badala yake wanatazama bandari zingine kama Durban (Afrika Kusini) na Beira (Msumbiji), ambazo hazipo kwenye mfumo huo,”alisema.
Mbali na sababu hizo, nyingine ni kushuka kwa thamani ya Randi ya Afrika Kusini, ambapo wafanyabiashara hutumia fedha kidogo kwenye malipo kwa kuwa Bandari ya Durban hutoza ushuru kwa kutumia Randi.
Akifafanua, alisema Tanzania imekuwa ikitumia dola kutoza ushuru, hivyo muda wote gharama husimama kama zilivyo, tofauti na nchi hiyo, ambako iwapo randi itashuka thamani, mfanyabiashara hutumia dola chache kulipia ushuru.
“Tunaiomba serikali itazame maeneo yenye changamoto yaliyo ndani ya uwezo wake ili itusaidie kurudisha kasi ya upokeaji shehena kutoka nje.
“Iwapo hatua hazitachukuliwa, tutaendelea kukabiliwa na changamoto huku washindani wetu wakitumia mwanya huo kutushinda katika huduma za bandari,” alisema.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Aloye Matei, alisema bandari kwa sasa imejiimarisha katika utoaji huduma mbalimbali kisasa, baada ya kupokea maombi kutoka kwa wateja wake.
Matei alisema hivi sasa kila kitu kinafanyika kiutaalamu zaidi, ikiwa ni pamoja na kufanya malipo kwa njia ya kielektroniki.

No comments:

Post a Comment