ALIYEKUWA Mbunge wa Viti
Maalumu (CHADEMA), Leticia Nyerere amefariki dunia.
Leticia, alifariki juzi,
katika Hospitali ya Doctors Community, iliyoko Lanham, Maryland nchini
Marekani, saa mbili usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Mwanasiasa huyo, ambaye
Julai 27, mwaka jana, alitangaza rasmi kuihama CHADEMA na kujiunga na Chama cha
Mapinduzi (CCM), alilazwa kwenye hospitali hiyo akisumbuliwa na ugonjwa wa
kansa ya damu.
Pia, alikuwa miongoni mwa
wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, ambaye alikuwa mstari wa mbele kupigania
haki ya uraia wa nchini mbili kwa Watanzania waishio nje ya nchini (Diaspora).
Leticia, ambaye ni mtoto
wa Mzee Musobi Mageni, aliolewa kisha kutengana na mtoto wa Hayati Baba wa
Taifa, Madaraka Nyerere, mwaka 1996, ambapo walifanikiwa kupata watoto watatu.
Kufuatia kifo hicho, Rais
Dk. John Magufuli, jana, alifika nyumbani kwa mjane wa Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Nyerere, Mama Maria Nyerere kumpa pole.
Pamoja na kutoa mkono wa
pole kwa Mama Maria Nyerere, nyumbani kwake Msasani, Jijini Dar es Salaam, Rais
Magufuli pia amewapa pole wanafamilia wote na amewaomba kuwa wavumilivu katika
kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na ndugu yao.
Msemaji wa familia ya
Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, alimueleza Rais Magufuli kuwa, familia
inaendelea na taratibu za kuusafirisha mwili wa marehemu kutoka nchini Marekani
na itatoa taarifa baadaye.
Tangu Desemba 27, mwaka
jana, Leticia alikuwa amelazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi hospitalini
hapo na kuelezwa kuwa hali yake ilikuwa sio nzuri.
No comments:
Post a Comment