RAIS wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein, amesema hatishwi na kauli zinazotolewa na wapinzani na kwamba, hawana ubavu wa kumuondoa kwenye nafasi hiyo.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ipo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar na kwamba, kama kuna mwenye shaka aende mahakamani badala ya kutoa kauli zenye kupotosha wananchi.
Dk. Shein, aliyasema hayo mjini hapa jana, wakati kilele cha Matembezi ya Vijana wa UVCCM katika viwanja vya Maisara mjini hapa, ambapo alisema yeye bado ni rais halali.
“Nipo madarakani kama Rais, Makamu wa Kwanza na Makamu wa Pili wa Rais wapo, mawaziri wote wapo na Baraza la Mapinduzi lipo, hivyo serikali inaendelea kama kawaida.
“Kelele na kauli za wapinzani hazina ubavu wa kuniondoa ndani ya Katiba maana hawana nguvu na hata wakitumia Katiba na Sheria ndio kabisa hawawezi,” alisema Dk. Shein.
Alisema hakuna mtu wala kikundi kinachoweza kumtisha kwa kuwa yeye ndiye rais halali na kamwe hana shaka na hilo.
Aidha, Dk. Shein amemjibu Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, kuwa kauli zake hazina mashiko.
Amesema ipo siku na yeye atawaita waandishi wa habari na kuwaeleza kwa undani kwa kuwa ana mengi, lakini kwa sasa ameamua kusikiliza tu.
Alitumia fursa hiyo kuwataka vijana kuendelea kuyaenzi Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kwani, ndio yaliyoleta ukombozi wa kweli kwa wananchi.
Seif: Hatima ya Z’bar kwa Magufuli
Wakati Dk. Shein akiweka msimamo huo, aliyekuwa mgombea
urais kwa tiketi ya CUF Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amemwomba Rais Dk.
John Magufuli, kuingilia kati mzozo wa kisiasa ulioko visiwani humo.
Mzozo huo ulijitokeza baada ya Mwenyekiti wa Tume ya
Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha, kufuta matokeo na uchaguzi mkuu wa
Oktoba 25, mwaka jana, kutokana na madai kuwa haukuwa wa haki, hasa upande wa
kisiwa cha Pemba.
Maalim Seif amedai kuwa tangu Oktoba 28, mwaka jana,
viongozi wa kisiasa nchini humo akiwemo yeye, wameendelea kufanya vikao vya
maridhiano vipatavyo nane.
Alisema sababu kuu ni kuwepo kwa mvutano wa kimaslahi
kwenye pande zote mbili na kwamba, muafaka hauonekani.
Maalim Seif alisema Zanzibar inatamani kuendelea kuwa
sehemu ya Tanzania yenye amani, hivyo siasa haipaswi kuwa chanzo cha machafuko.
Amesema kwa kuwa Dk. Magufuli tayari amekutana naye pamoja
na Rais Ali Mohammed Shein kwa nyakati tofauti, asirudi nyuma kuwasaidia.
Aliyasema hayo jana, Dar es Salaam, alipokutana na
waandishi wa habari, kwa lengo la kuzungumzia msimamo wake juu ya hali ya
kisiasa, ambapo alisema hatma ya mgogoro huo ipo mikononi mwa Dk. Magufuli.
“Rais Magufuli amefanya kazi kubwa ya kututia moyo
ili tukamilishe mazungumzo hayo kwa ufanisi, kwa kuzingatia matakwa ya Katiba
na Sheria, alikutana na mimi na baadaye Dk. Ali Mohamed Shein,”alisema Maalim
Seif.
Aliongeza kuwa Dk. Magufuli ndiye mtu pekee,
atakayeweza kulimaliza suala lao kwa kuwa mara baada ya kuzungumza naye siku
chache zilizopita, alizungumza pia na waandishi wa habari Ikulu, Dar es Salaam,
ambapo alisisitiza haja ya kukamilisha mazungumzo baina ya CCM na CUF Zanzibar.
“Tunaona ni wakati muafaka yeye mwenyewe aongoze
juhudi zenye lengo la kunufaisha hatua, ambazo zitaleta kufikia tamati kwa
maridhiano baina yetu kule visiwani, lakini suala la kurudiwa uchaguzi
halikubaliki,” alisema Maalim Seif.
Aliongeza kuwa upo umuhimu kwa uongozi wa juu wa
vyama vya CUF na CCM, kufanya mazungumzo ya haraka ya kukamilisha taratibu za
kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.
Hata hivyo, licha ya kutoa malalamiko lukuki akidai
kuonewa kwenye uchaguzi wa Oktoba, mwaka jana, kutokana na hatua iliyochukuliwa
na Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salum Jecha, msimamo wake haukuwa bayana.
Alikuwa akionyesha dhahiri kuwa na msimamo wake
binafsi tofauti na CUF, ambapo alidai CCM wanataka kumchezea mchezo mchafu,
ambao hata hivyo hakuutaja endapo uchaguzi utarudiwa visiwani Zanzibar.
Huku pia akikwepa kujibu kwa usahihi maswali ya
wanahabari waliohudhuria mkutano wake, Maalim Seif alisema anajiamini na kwamba
hata uchaguzi ukirudiwa, anaweza kushinda kwa kuwa wapiga kura wake wako pamoja
naye.
CCM yasisitiza uchaguzi kurudiwa
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, amesema pamoja na maneno ya
wapinzani, uchaguzi wa marudio upo pale pale.Alisema kuna njama za kuvishawishi vyama vingine vya upinzani visishiriki uchaguzi huo, lakini hata kama itabaki CCM pekee, uchaguzi utarudiwa kwani ndio utakaotoa demokrasia ya kupata kiongozi.
Balozi Iddi alisema haoni haja ya kuendelea na mazungumzo ya kutafuta suluhu kutokana na Maalim Seif kutoa siri za vikao kinyume cha taratibu na makubaliano.
Aliwataka wananchi wa Zanzibar kuisubiri Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), kutangza tarehe ya marudio ya uchaguzi na amewataka kuwapuuza wanaodai hakuna uchaguzi.
Alisema baadhi ya watu wanadai kuwa uchaguzi ukirudiwa watatumia nguvu ya umma, hivyo amewataka kujiandaa kubeba dhima kama kutatokea vurugu.
No comments:
Post a Comment