Tuesday, 12 January 2016
MAKADA 27 WAJITOSA KUWANIA UENYEKITI WA CCM ARUSHA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Arusha, kimefunga rasmi uchukuaji wa fomu za kugombea nafasi mbalimbali zilizoachwa wazi na makada waliokimbilia CHADEMA, wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.
Katibu Msaidizi wa CCM mkoani hapa, Omary Bilal, akizungumza na Uhuru jana, alisema katika mchakato huo, makada 27 walijitokeza kuchukua fomu za kuwania uenyekiti wa Chama mkoa.
Alisema makada 25 ndio walirudisha fomu za kuwania nafasi hiyo huku wawili wakishindwa kufanya hivyo.
Bilal aliwataja makada walioshindwa kurejesha fomu kuwa ni Shaban Massawe na Rajab Mshana, ambao mpaka jana saa 10 jioni, walikuwa hawajarejesha fomu hizo.
Alisema kati ya makada hao 25, wanawake watatu wamejitokeza kuwania nafasi hiyo ambao ni Agness Mollel, Benadeta Changuru na Veraikubda Urioh.
“Wanawake watatu wamejitokeza kuwania nafasi hii nyeti kwenye Chama ngazi ya mkoa, hii inaonyesha ni jinsi gani demokrasia inazidi kukua, lakini pia wanawake wameonyesha ujasiri mkubwa.
Napenda nichukue fursa hii kuwapongeza sana kwa ujasiri,” alisema
Bilal alisema makada wengine 33 wamejitokeza kuwania nafasi ya Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi na kurejesha fomu hizo kwa wakati, wakiwemo waandishi wawili wa habari, Shaaban Mdoe na Semmy Kiondo.
Alisema kwa mujibu wa ratiba iliyotoka Makao Makuu ya Chama, uchukuaji wa fomu ulianza Januari 6, mwaka huu hadi juzi, saa 10 jioni.
Kiongozi huyo alisema Januari 17, mwaka huu, Kamati ya Siasa ya Mkoa, itakutana kwa ajili ya kutoa mapendekezo ambayo yatajadiliwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa kwa ajili ya kuteua majina ya wagombea.
Alisema baada ya ya uteuzi wa majina hayo kukamilika, mkutano mkuu wa mkoa pamoja na wilaya husika, zitafanya uchaguzi kati ya Januari 26 na 28, mwaka huu.
Wakati huohuo, Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Said Yassin, amesema makada 20 wamejitokeza kuwania nafasi ya mwenyekiti wa umoja huo, lakini mmoja alishindwa kurejesha fomu yake kwa wakati
Yasini alimtaja kada huyo kuwa ni Godwily Macho, ambaye mpaka juzi, saa 10:00 jioni, alishindwa kurejesha fomu yake.
Katika nafasi ya ujumbe wa baraza la UVCCM, alisema makada 18 walijitokeza kuwania nafasi hiyo, huku mmoja akishindwa kurudisha fomu yake kwa wakati.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment