Monday, 25 January 2016
MAJIPU YAZIDI KUTUMBULIWA, KIGOGO WA SERIKALI, MKANDARASI WASHIKILIWA NA POLISI
JESHI la Polisi linawashikilia watumishi wanane wa Halmashauri ya Mji wa Kahama na mkandarasi wa Kampuni ya Noble Cliff ya Dar es Salaam, kwa madai ya kughushi nyaraka na kuisababishia serikali hasara ya sh. bilioni 1.6.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Mika Nyange, alisema watumishi hao na mkandarasi huyo wanaendelea kuhojiwa kuhusu tuhuma za ubadhirifu zinazowakabili na kwamba watakaobainika watafikishwa mahakamani leo.
Aliwataja wanaoshikiliwa kuwa ni mkandarasi wa Kampuni ya Noble Cliff Ltd ya Dare s Salaam, Alexander Kilama, Luchanganya Nkonongumo, Michael Nzingura, Joseph Maziku na Kulwa Stephen.
Wengine ni Joachim Henjewele, Anastazia Manumbu, Gervase Rugodisha na Elius Morell, ambao wanatuhumiwa kutenda kosa hilo katika kipindi cha Juni, 2014/2015.
Kamanda Nyange alisema jitihada za kuwapata wengine wanne zinaendelea kwa kuwa watuhumiwa wanatakiwa kuwa 12, wakiwemo wakuu wa idara mbalimbali.
Kukamatwa na kuhojiwa kwa watu hao kunatokana na maagizo ya kamati maalumu ya uchunguzi kuhusu ubadhirifu wa fedha za serikali wilayani humo, ambapo kamati hiyo iliagiza waliokuwa viongozi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, kurudishwa wilayani humo kwa ajili ya kuhojiwa kuhusu hasara hiyo.
Awali, katika kikao cha baraza la madiwani la halmashauri hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Vita Kawawa, wakati akisoma taarifa ya uchunguzi ulioanzishwa Desemba, mwaka jana, wa kuchunguza ubadhirifu ulioibuliwa na baraza la madiwani, aliagiza wahusika wachukuliwe hatua.
Kawawa alisema viongozi waliotakiwa kurudishwa ni aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji, Felix Kimario, ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Longido na Mhandisi Musumba Musoka, aliyehamishiwa Nanyumbu mkoani Mtwara.
Pia, Kawawa aliitaka Bodi ya Zabuni ya Halmashauri ya Mji wa Kahama na timu ya tathmini, iwajibishwe huku watumishi wa idara mbalimbali walioshiriki kuitia hasara ya sh. bilioni 1.6 serikali wilayani humo, kuwajibishwa kwa matumizi mabaya ya ofisi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment