RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, amewaomba
wananchi kuendelea kuwa wavumilivu na wastahamilivu na waendelee na shughuli
zao za maisha za kila siku kwa amani, katika kipindi hiki ambacho wanasubiri
kutangazwa kwa tarehe nyingine ya marudio ya uchaguzi.
Amesema uchaguzi wa Zanzibar, ulifutwa Oktoba 28,
mwaka jana, baada ya kubainika kutokea kasoro kadhaa kama zilizoelezwa na Tume
ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na kwamba, uamuzi huo wa tume ulitangazwa katika
gazeti rasmi la serikali la Novemba 6, mwaka jana.
"Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ndio yenye jukumu
la kusimamia na kuendesha uchaguzi wa rais, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
na madiwani, hivyo nawaomba wananchi
waendelee kuishi kwa amani na kupendana
huku tukisubiri Tume ya Uchaguzi Zanzibar itangaze tarehe nyingine ya kurudia
uchaguzi," alisema.
Dk. Shein alisema baada ya uchaguzi huo kufutwa,
viongozi walishauriana wakutane ili wafanye mazungumzo ya kutafuta suluhu kwa
njia ya amani ili nchi iendelee kuwa ya umoja na mshikamano.
Akizungumza katika Maadhimisho ya Miaka 52 ya
Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, yaliyofanyika jana, katika Uwanja wa Amaan,
mjini hapa, Dk. Shein alisema mazungumzo hayo yanahusisha viongozi sita waliopo
madarakani, wastaafu na kwamba yeye ndiye mwenyekiti.
Dk. Shein alisema mazungumzo hayo bado yanaendelea na
taarifa ya pamoja ya mazungumzo hayo itatolewa na wajumbe mara yatakapokamilika.
“Katika kipindi hiki ni vyema wananchi wakaendelea
kuwa wavumilivu, wastahamilivu na waendelee na shughuli zao za maisha ya kila
siku kwa amani,” alisema.
Alisema kudumishwa kwa Mapinduzi ya Zanzibar, ni
lazima kuendelezwe na kudumishwa Muungano wa Tanzania, kwani ni kielelezo
muhimu cha umoja wa wananchi.
Alisema serikali ya awamu ya saba, anayoiongoza
itaendelea kuwa muumini wa dhati wa Muungano na kuyatekeleza kwa vitendo
malengo ya waasisi wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Karume.
MAFANIKIO
Dk. Shein alisema serikali imeongeza ufanisi katika
ukusanyaji wa mapato na kudhibiti uvujaji wa mapato hayo, ambapo katika kipindi
cha miezi sita ya kwanza ya mwaka wa fedha 2015/2016, mapato yalifikia sh.
bilioni 188.4.
Alisema serikali inaendelea na juhudi za kukusanya
mapato, ikiwa ni pamoja na kupunguza misamaha ya kodi katika baadhi ya miradi
ya uwekezaji na kufanya viwango vya ada mbalimbali.
Dk. Shein alisema juhudi za kufufua viwanda zilipata
mafanikio mwaka jana, ikilinganishwa na miaka iliyopita, ambapo bidhaa
zilizozalishwa viwandani, zikiwemo maziwa, sukari, maji ya kunywa, unga wa
ngano, juisi, sabuni, bidhaa za nguo na viungo zilikuwa na thamani ya sh. bilioni
136.0.
Alisema sekta ya utalii, ambayo ndio kiongozi kwa
uchumi wa Zanzibar, inaendelea kuboreshwa ili kuleta tija zaidi.
Dk. Shein alisema sekta ya kilimo imeimarishwa kwa
lengo la kuhakikisha kuwa uhakika wa chakula na lishe unakuwepo muda wote.
Kuhusu uendelezaji wa maliasili, alisema serikali
itaendelea kusimamia ulinzi na udhibiti wa misitu, ukiwemo msitu wa Jonzani
Unguja, msitu wa Ngezi Pemba na misitu mingine ya asili.
Akizungumzia miradi ya maji, Dk. Shein alisema
jitihada kubwa zilifanywa katika kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama kupitia
miradi mbalimbali ya maji mijini na vijijini, ambapo upatikanaji wa maji mijini
umefikia asilimia 87 na asilimia 70 vijijini.
Alisema serikali imeongeza bajeti ya dawa kutoka sh. bilioni
moja kwa mwaka 2013/2014, hadi kufikia sh. bilioni, 4.3 mwaka 2015/2016.
Dk. Shein alisema Zanzibar, imepiga hatua kubwa
katika kupunguza vifoo vya wajawazito na watoto, kutokana na wanawake
kujifungulia hospitalini na huduma za uzazi kusambazwa vijijini.
Akizungumzia ugonjwa wa kipindupindu, alisema
umedhibitiwa na kwamba hivi sasa umepungua kwa kiasi kikubwa.
Kuhusu tatizo la ajira, alisema serikali kupitia
mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi, imeongeza fedha za dhamana katika Benki
ya CRDB kutoka sh. milioni 100, hadi kufikia sh. milioni 150, katika mwaka
2015.
Dk. Shein alisema serikali inaendelea na matayarisho
ya uanzishwaji wa mpango wa pensheni jamii kwa wazee walio na umri wa miaka 70
na kuendelea.
Kuhusu watu wenye ulemavu, alisema tayari serikali
imechukua hatua ya kuhakikisha wanapatiwa haki zao na kuwekewa mazingira mazuri
yanayozingatia mahitaji yao pamoja na kushirikishwa katika masuala mbalimbali
ya kijamii.
BALOZI
IDI
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi,
alisema Sherehe za Mapinduzi
zilizinduliwa Januari 3, mwaka huu, na kufikia kilele chake jana.
Alisema jumla ya miradi 16 ya maendeleo ilizinduliwa
na miradi minane iliwekwa mawe ya msingi.
HALI
ILIVYOKUWA
Milango ya Uwanja wa Amaan ilifunguliwa kuanzia saa
12:00, asubuhi, ambapo wananchi walijitokeza kwa wingi kushuhudia sherehe hizo.
Aidha, viongozi mbalimbali walianza kuwasili kuanzia
saa 1:30, asubuhi na kupokelewa kwa shangwe na nderemo kutoka kwa wananchi.
Miongoni mwa viongozi waliohudhuria ni Rais Dk. John
Magufuli, ambaye anaandika historia ya kushiriki sherehe kubwa tangu kuapishwa
kwake.
Pia, Dk. Magufuli ameandika historia nyingine kwa
kusafiri kwa mara ya pili tangu kuapishwa, ambapo mara ya kwanza alisafiri
kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.
Viongozi wengine waliohudhuria ni marais wastaafu Ali
Hassani Mwinyi, ambaye aliambatana na wake zake, Benjamini Mkapa, akiwa na mke
wake, Jakaya Kikwete akiwa na mkewe. Pia Makamu wa Rais mstaafu, Dk. Mohammed
Gharib Bilal na Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.
Wengine ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan,
Waziri Mkuu, Kasimu Majaliwa, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula,
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa,
NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu
Ameri Kificho, Mkuu wa Majeshi, Jenerali, Davis Mwamunyange, Mkuu wa Jeshi la
Polisi, IGP Ernest Mangu na viongozi wengine wakiwemo, mawaziri wa Zanzibar na
Tanzania Bara na mabalozi.
JECHA
AIBUKIA AMAAN
Katika sherehe hizo, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi
ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, aliibuka na kuwa kivutio kikubwa.
Jecha, muda mwingi alionekana akiwa na furaha na
tabasamu huku akibadilishana mawazo na viongozi mbalimbali.
GWARIDE
Sherehe hizo zilipambwa kwa gwaride la vyombo vya
ulinzi na usalama, ambavyo vilipita
mbele ya rais kwa mwendo wa pole na wa haraka.
Gwaride liliingia uwanjani saa 3:00, asubuhi,
likiongozwa na kamanda wake, Luteni Kanali Mohamed Adamu.
Ilipofika saa nne, asubuhi, Dk. Shein aliingia
uwanjani akiwa kwenye gari la wazi la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),
akiongozwa na pikipiki 21 za askari polisi, ambapo alikuwa akiwapungia wananchi
mikono.
Baadaye rais alisimama kwenye jukwaa maalumu, ambapo
wimbo wa taifa ulipigwa pamoja na mizinga 21.
Aidha, katika sherehe hizo kikosi maalumu cha jeshi
kilipita mbele ya rais na kutoa salamu kikiwa kimevalia kivita.
MAANDAMANO
Sherehe hizo zilipambwa kwa maandamano ya wananchi wa
mikoa yote ya Zanzibar pamoja na maandamano ya wafanyakazi wa serikali na
mashirika ya umma.
USIKU
WA MAPINDUZI
Ilipofika saa sita kamili usiku wa Januari 12,
wananchi wa mji wa Zanzibar na viunga vyake walijitokeza kwa wingi kwenye
maeneo mbalimbali ambapo walikuwa wakishuhudia upigaji wa fataki kama ishara ya
sherehe hiyo.
Tukio hilo lilivuta hisia za wananchi wengi ambao
walikusanyika kwenye maeneo tofauti na kushangilia huku anga la mji wa
Zanzibar, likimeremeta.
No comments:
Post a Comment