Saturday, 23 January 2016

SERIKALI YAJADILI ADHABU MBADALA





MRUNDIKANO wa wafungwa na mahabusu kwenye magereza nchini, umeendelea kuiumiza kichwa serikali, ambapo imesema itaongeza vifungo vya nje kama sehemu ya mkakati.
Imesema mbali na wafungwa kupewa adhabu za nje, ikiwemo kutumikia jamii, pia itaongeza kasi ya kutoa elimu kuhusiana na madhara ya uhalifu ili kupunguza matukio ya uhalifu nchini.
Serikali pia imeitaka Mahakama kuendesha kesi haraka ili kupunguza idadi ya mahabusu, ambayo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa mlundikano kwenye Magereza.
Hayo yameelezwa jana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Yahya Simba, wakati akizungumza na watendaji wa Jeshi la Magereza.
“Ili kupunguza changamoto katika malengo ya kuelekea uchumi wa kati ifikapo 2025, kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza, tunakusudia kuwapeleka wahalifu kutoa huduma za jamii, badala ya kuwafunga magerezani,” alisema.
Alisema kuchelewa kusikilizwa kwa kesi katika mahakama hapa nchini, ni miongoni mwa sababu ya mlundikano magerezani, hivyo alizitaka mahakama kuendesha kesi zake haraka.
Balozi Simba alisema ni mbinu muhimu kutoa elimu kwa jamii juu ya kuacha uovu ili kuipunguzia serikali mzigo wa kugharamia  mahabusu na wafungwa na kupunguza msongamano magerezani.
Hata hivyo, alilipongeza jeshi hilo kwa kuwa licha ya kutunza wahalifu, limekuwa likijitahidi kuwapatia elimu hiyo.
Kuhusu kuanzisha miradi, alisema ameishauri Magereza kuwekeza kwenye hoteli za kitalii fukweni ili kujiongezea kipato.
Alisema tayari jeshi hilo limeanzisha kilimo kwa ajili ya chakula na biashara, ikiwemo kufanya mikakati ya soko.
Akifafanua kuhusu suala hilo, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, John Minja, alisema wanamiliki jumla ya hekta 130,000, wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani, lakini tayari wamelima takribani hekta 60.
“Tunakusudia kupanua kilimo katika maeneo yetu mbalimbali nchini ili pia kukabiliana na tatizo la uvamizi wa ardhi. Tayari ipo migogoro ya ardhi kutokana na wananchi kufahamu umuhimu wa ardhi,” alisema.
Alisema, msongamano wa mahabusu upo katika baadhi tu ya nagereza nchini. Hata hivyo, alisema haiwezekani kuhamisha wafungwa kuwapeleka kusiko na msongamano kutokana na sheria kutaka mtu afungwe alipofanya makosa.
Minja alisema uwezo wa magereza ni kuhifadhi wahalifu 29,552 kwa siku, lakini wamekuwa wakipokea zaidi ya wahalifu 34,000.

No comments:

Post a Comment