Saturday, 23 January 2016

NAPE: KASI YA MAGUFULI IMEMALIZA UPINZANI





KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, amesema ana hofu ya vyama vya upinzani kufa kutokana na kasi kubwa ya serikali ya CCM katika kuwatumikia Watanzania.
Amesema CCM na serikali yake imejipanga kuhakikisha kero zote zinazowakabili wananchi zinapatiwa ufumbuzi kwa haraka na uhakika zaidi.
Nape, ambaye pia ni Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, alisema jana kuwa, kasi ya utendaji ya Rais Dk. John Magufuli, tangu alipoingia madarakani, imevifanya vyama vya upinzani kukosa ajenga na kudorora kabisa.
“Upinzani kwa sasa hauna ajenda kabisa na vipo hatarini kupoteza uhai. Zile siasa za majitaka na propaganda za kuhadaa wananchi sasa zimekwisha kabisa. Wamebaki jina tu, wanajaribu kufurukuta, lakini wameshindwa,” alisema Nape.
Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kukagua Uwanja wa Michezo wa Namfua mjini hapa, ambako sherehe za miaka 39 ya kuzaliwa CCM zinatarajiwa kufanyika.
“Kuna dalili zote za kufa kwa vyama vya upinzani wakati wowote kuanzia sasa. Tunavipenda, hivyo tutafanya kila litakalowezekana ili kuhakikisha havifi na vinaendelea kuwepo kwa ajili ya kudumisha demokrasia,” aliongeza Nape.
Kuhusu Maadhimisho ya Miaka 39 ya CCM, Nape alisema ameridhishwa na maandalizi ya sherehe hizo, ambazo kwa mwaka huu zitahudhuriwa na viongozi wengi kutoka ndani na nje ya nchi pamoja na wananchi kwa ujumla.
“Sherehe za maadhimisho ya mwaka huu, zitakuwa za aina yake kwa sababu zitahusisha na kitendo cha Chama kushinda uchaguzi mkuu, mwaka jana, na kushika dola kwa mara nyingine tena.
“Kwa vyovyote wakazi wa mkoa huu na hasa wa mji wa Singida, wajiandae kunufaika na ugeni utakaokuja wakati huo, mgeni njoo mwenyeji akope,” alisema.
Alisema kuanzia mwisho wa mwezi huu, sherehe hizo zitatanguliwa na viongozi wa ndani na nje ya mkoa, kushiriki kazi za maendeleo, zikiwemo za kilimo, ujenzi wa taasisi za umma, ikiwemo maabara, vyumba vya madarasa, vyoo, kuzibua mifereji na kufanya usafi.
“Falsafa ya ‘Hapa Kazi Tu’ itatawala katika sherehe za mwaka huu. Zitafanyika shughuli nyingi za maendeleo ya wananchi, hivyo nitumie fursa hii kuwahimiza wananchi kila mmoja kwa nafasi yake, achape kazi halali kwa bidii na maarifa,”alisisitiza.

No comments:

Post a Comment