Amiri Jeshi Mkuu,Rais Dkt Magufuli akiwasikiliza wananchi kwa makini alipopita maeneno ya Sanawali kuwasalimia wakati akielekea Wilayani Monduli. |
Baadhi ya Wananchi wa Maeneo ya Sanawali wakishangilia ujio wa Rais John Pombe Joseph Magufuli,alipokuwa akielekea Wilayani Monduli mapema leo asubuhi. |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 21 Januari, 2016 amewasili Mkoani Arusha ambapo keshokutwa tarehe 23 Januari, 2016 atatunuku kamisheni kwa maafisa wanafunzi wa kundi la 57/15 katika chuo cha mafunzo ya kijeshi (TMA) Monduli mkoani hapa.
Rais Magufuli amewasili Mjini Arusha akitokea Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) alikotua kwa ndege akitokea jijini Dar es salaam na kupokelewa na mamia ya wananchi.
Akiwa uwanjani hapo Rais Magufuli amewashukuru wananchi kwa mapokezi makubwa aliyoyapata na amewaeleza kuwa uchaguzi umekwisha, kilichobaki ni kazi tu.
"Nawashukuru sana ndugu wananchi kwa mapokezi haya makubwa, naomba kuwahakikishia kuwa uchaguzi umekwisha na sasa kilichobaki ni kuchapa kazi tu" Alisema Rais Magufuli.
Akiwa njiani kutoka uwanja wa ndege wa KIA, Rais Magufuli amesimamishwa na wananchi wa njiapanda ya KIA, Kikatiti, Usa River, Tengeru na Mount Meru Mjini Arusha ambapo huko kote pamoja na kusisitiza kuwa uchaguzi umekwisha na kilichobaki ni kuchapa kazi, amewahakikishia kuwa hatawaangusha.
Dkt. Magufuli ametoa wito kwa watanzania kumuombea ili aendelee kuwashughulikia wote wanaofanya ubadhilifu wa fedha za umma kupitia kampeni yake ya kutumbua majipu.
"Nataka niwahakikishieni kuwa nitaendelea kutumbua majipu yote mpaka yaishe, na naomba mniombee ili kazi hii ya kutumbua majipu ifanyike kwa mafanikio" Alisisitiza Mheshimiwa Magufuli.
Aidha Rais Magufuli amesema tayari serikali imeanza kutoa fedha kwa ajili ya kugharamia elimu ya Msingi na Sekondari baada ya kufuta ada na akaonya kuwa watumishi wa umma hususani wakuu wa shule watakaothubutu kufanya ubadhilifu wa fedha hizo watashughulikiwa.
Amesema yote aliyoyaahidi kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha na watanzania kwa ujumla ikiwemo ujenzi wa barabara za Arusha, kulipa fidia za wananchi na kufuta ada ya shule za msingi na sekondari yanatekelezwa.
Rais Magufuli amesisitiza kuwa serikali yake haitawabagua watanzania kwa dini zao wala makabila yao na wala haitawabagua kwa milengo ya vyama vyao na kanda zao na kuwataka watanzania wote kuiweka mbele Tanzania na kushirikiana kuiendeleza.
Gerson Msigwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Arusha.
21 Januari, 2016
No comments:
Post a Comment